Betri chakavu za kompyuta sasa ni lulu

Muktasari:
- Ukitupacho wewe kwa wengine kina maana kubwa. Huu ni msemo unaobeba maana kuwa wakati wewe ukimaliza kutumia kitu fulani na kuona hakifai, kuna mwingine ndiyo kwanza hukiona kama kipya na kina fursa kwake.
Dar es Salaam. Ukitupacho wewe kwa wengine kina maana kubwa. Huu ni msemo unaobeba maana kuwa wakati wewe ukimaliza kutumia kitu fulani na kuona hakifai, kuna mwingine ndiyo kwanza hukiona kama kipya na kina fursa kwake.
Usemi huu unasadifu kile anachokifanya Gibson Kawago (27) mzaliwa wa mkoa wa Iringa ambaye anatumia betri za kompyuta mpakato mbovu kuzalisha bidhaa mpya, ikiwemo vitunza chaji (power bank).
Mbali na vifaa vya kutunza chaji pia huzalisha betri zilizo na uwezo wa kuwasha taa katika nyumba na vifaa vingine vinavyohitaji nishati ya umeme kama runinga, hivyo kuwezesha baadhi ya nyumba kuondokana na matumizi ya vibatari.
Kawago ambaye ni mhitimu wa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) katika fani ya uhandisi wa umeme, anasema wazo hilo alilipata akiwa nyumbani kwao wakati ambao familia zilikuwa zikilazimika kutumia mbinu za ziada ili waweze kuchaji simu zao.
Alisema kutokana na kukosekana kwa nishati ya umeme katika kijiji alichokuwapo, watu walikuwa wakilazimika kutumia muda mrefu kufuata umeme ulipo, ili waweze kuchaji simu zao za mkononi.
Kwa wakati huo akiwa shule ya msingi, alikuwa akipenda kutengeneza vitu kama redio, simu za watu ndivyo wazo la kutafuta namna ya kuchaji simu ilimfikia na kuamua kujaribu.
“Kwa wakati ule niliamua kutengeneza ‘powerbank’ kwa kutumia betri, lakini haikuwa na uwezo wa kuchaji simu hadi ijae, ndipo niliamua kuendelea kutafuta ufanisi zaidi.”
Udadisi katika kile alichokifanya ulizidi kuongezeka zaidi kadiri alivyokuwa akisonga mbele kielimu.
Alipofika chuo, alihisi kuwa betri za laptop zinaweza kufanya kazi kwa ufanisi, ndipo alianza kuziokota katika maeneo ya soko la Kariakoo na Machinga Complex, alipozipata alizivunja ili kuzifanyia utafiti zaidi.
Baadaye aligundua endapo zikifanyiwa urejelezeshaji, zinaweza kuzalisha powerbank yenye nguvu.
“Nikawa kila nikitengeneza najaribu na marafiki zangu, nyingine zilikubali, nyingine zilikataa na nilipomaliza chuo niligundua namna ya kutengeneza kwa kutumia kompyuta na aina tofauti za soketi,” anasema Kawago.
Ikiwa ni wazo lililodumu kwa zaidi ya miaka 12 sasa tangu aanze kulifanyia kazi, baadaye aligundua kuwa kupita betri hizo anaweza kutengeneza betri kubwa zilizo na uwezo wa kutumika katika nyumba, watu kuwa na uwezo wa kuwasha taa, kuangalia runinga, kusikiliza redio na kuchaji simu zao.
Betri hizo hupatikana kwa kuunganisha pamoja na betri za laptop na kupata moja kubwa ambayo ambayo huweza kuunganishwa katika kifaa kiitwacho ‘inverter’. Betri hizo huweza kuchajiwa kwa sola (umeme jua) na baadaye mtu akatumia umeme katika kuwasha vifaa tofauti ndani ya nyumba yake.
Hadi sasa nyumba saba zimenufaika na huduma hiyo ambayo bado anasema anaendelea kufanyia uboreshaji.
Alisema ukuaji wa wazo hilo umekuwa wa taratibu kwa kile alichokieleza kuwa kila kitu hulazimika kusoma mtandaoni.
Wanufaika wengine
Mbali na powerbank, pia wapo baadhi ya wanufaika wa kile anachokifanya Kawago na miongoni mwao ni watu wanaomiliki pikipiki za umeme za kuchaji.
Hao amekuwa akiwasaidia kwa kuwabadilishia betri pindi zile zilizokuja na bidhaa husika zinapoisha nguvu au kufa.
“Kuna wale ambao pia wana spika za ‘bluetooth’, miongoni mwao pia wamekuwa wakija kwangu kubadili betri pindi zinapoishiwa nguvu,” anasema Kawago.
Nini kinafanyika sasa?
Kwa sababu bado hajaingiza bidhaa hizo sokoni rasmi na kuwa kibiashara, alisema kwa sasa anatengeneza mazingira ambayo ataweza kuzalisha kitu kizuri kitakachokuwa kimekidhi vigezo na masharti yote.
Hadi kufika hapo alipo, alilazimika kuacha kazi kama meneja wa kituo cha sayansi kwa ajili ya kusaidia vijana kufanya vitendo vya sayansi na teknolojia mkoani Tanga ili aweze kujiajiri.