Bomoa bomoa yashika kasi KIA

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu akizungumza na wakazi wa Kata ya Kia baada ya kutembelea eneo walilohama kuona shughuli za bomoa bomoa. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Ni baada ya wananchi kufidiwa, RC Kilimanjaro atoa wiki moja waliosalia waondoke
Hai. Wakati kazi ya kuwaondoa wananchi wanaodaiwa kuvamia eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ikiendelea, imeelezwa zaidi ya asilimia 95 ya waliolipwa fidia wameshaondoka.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanajro, Nurdin Babu amesema wanaopaswa kuondoka upande wa Wilaya ya Hai ni kaya 1,061.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Mei 11 2024 amesema katika Kijiji cha Sanya Station kuna kaya 596, Tindigani (402) na Chemka (62).
Babu amesema Sh7.2 bilioni zimeshatumika kulipa fidia.
Jeremiah Laizer, mkazi wa Kata ya KIA, amesema hawawezi kubishana na Serikali kwa kuwa maendeleo ni ya kila mmoja, hivyo ameiomba kuhakikisha wanakohamia wanapata huduma muhimu za kibinadamu kama maji na umeme.
"Hatubishani na Serikali, tunaomba mtupe ulinzi na ushirikiano ili wakati tunabomoa nyumba zetu tuweze kuhamisha vitu vyetu vikiwa salama. Tupewe muda kwa sababu fidia tumeshapewa angalau tuondoke Jumanne," amesema.
Lighteness Laizer, aliishukuru Serikali kwa kuwalipa fidia akisema awali hawakuwa wakijua cha kufanya.
Katika maeneo hayo jana baadhi ya nyumba wakazi wake wameshahama na zingine zikiendelea kuvunjwa kwa kutumia tingatinga.
Babu aliyetembelea eneo hilo jana alisema wananchi wenye changamoto, ikiwamo ya mirathi fidia zao hazikulipwa, na kwamba, sasa wameanza kujaza fomu na watalipwa baada ya kesi kumalizika.
"Serikali ina ubinadamu, ina utu na inajali haki zote za binadamu, ndiyo maana tumefanya zoezi hili kwa umakini tangu mwanzo, tumewashirikisha viongozi wote wa hapa Hai," amesema Babu.
"Hakuna aliyelazimishwa kuondoka hapa, isipokuwa, kwa sababu eneo hili lina hati ya Serikali kwenye kiwanja hiki na watu walikuwa hawajui wakaingia kwenye eneo hili la uwanja wa ndege, ndiyo maana Serikali ikakubali kutoa fedha zaidi ya Sh11.5 bilioni kulipa watu wote," amesema.
Alisema hadi jana wananchi ambao hawajalipwa ni 34 ambao baadhi wamepeleka shauri lao kwenye vyombo vya sheria.
Babu amesema mambo yao yamekwisha na tayari wamejaza fomu, hivyo amemwagiza Mkurugezi wa Viwanja vya Ndege ahakikishe wanalipwa fedha zao.
Babu amesema wiki moja kwa wananchi waliolipwa fidia na hawajaondoka eneo la KIA akisema waondoke kupisha upanuzi wa uwanja.
Diwani wa KIA, Tehera Mollel amesema Serikali imetumia utu kuwaondoa wananchi katika eneo hilo kwa kufuata utaratibu na kuhakikisha kila moja analipwa fidia.
"Hakuna mwananchi wa KIA ambaye amevunjiwa na kubomolewa nyumba akiwamo ndani, tulitoa nafasi ya watu kuondoka,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Amiri Mkalipa amesema, "zoezi hili limeenda vizuri maana tuna timu nzuri ambayo inafanya kazi kwa utu, uzalendo na kwa weledi, kwa kuzingatia haki za binadamu.”