Jinsi Profesa Mathew Luhanga alivyoniingiza katika taaluma-1

Monday September 20 2021
Luhanga pc

Siku ya Jumamosi ya Februari 20, 1999 imebaki kuwa rejea katika maisha yangu. Hii ni siku ambayo Profesa Mathew Luhanga, wakati huo akiwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), aliponiita ofisini kwake asubuhi majira ya saa tatu.

Hii ilikuwa ni baada ya mimi kumaliza muda wangu wa uongozi wa Jumuiya ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, maarufu kama Daruso, kufuatia uchaguzi wa uongozi mpya uliofanyika siku ya Jumatano ya Februari 17, 1999.

Baada ya kumsalimia na kunikaribisha ofisini kwake, na baada ya kuwa nimeshaketi, aliniambia kuwa ameniita kunieleza jambo moja tu, na ninamnukuu kadri ninavyokumbuka maneno yake kwa kuwa hayajawahi kutoka kichwani mwangu:

“Wewe ni principled, usiache kuwa principled, utafika mbali sana”. Tuliongea naye kwa muda wa nusu saa hivi na tukaagana akinieleza kuwa alikuwa anaelekea Zanzibar. Tuliagana na Profesa Luhanga akinitakia kila la heri katika masomo na maisha yajayo baada ya kumaliza vizuri muda wangu wa uongozi.

lUHANGA PCC

Kwa wanaomfahamu Profesa Luhanga, watakubaliana nami kwamba kuitwa naye ofisini kwake kwa mtu yeyote aliyekuwa Udsm, awe mfanyakazi au mwanafunzi, wakati ule halikuwa jambo jepesi.

Advertisement

Profesa Luhanga alikuwa amejijengea heshima kubwa sana na wakati mwingine hata kuogopwa. Hivyo, hakuna mtu ambaye angetamani awe katika mazingira ya kuitwa naye tena ofisini kwake na tena siku ya Jumamosi.

Pengine kikubwa zaidi ni kupewa maneno mazuri kama yale kutoka kwa mtu muhimu sana kama Profesa Luhanga, lilikuwa jambo kubwa sana kwa kijana kama mimi wakati huo nikiwa naelekea kufikisha miaka 28, na ndio kwanza najipanga kuanza maisha baada ya chuo.

Nilijisikia fahari sana. Maneno yale yamebaki kuwa mwongozo muhimu katika maisha yangu binafsi, kitaaluma na sasa katika siasa.


Sifa ya kuwa principled

Ni matukio mawili makubwa yalimfanya Profesa Luhanga anione nipo ‘principled’. Tukio la kwanza ni mwaka 1998. Profesa Luhanga, akiwa VC (Makamu Mkuu wa Chuo).

Aliitisha mkutano na wanafunzi kwa lengo la kuelezea maendeleo ya programu ya mabadiliko na maboresho ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, maarufu wakati ule kama UDSM Institutional Transformation Programme (ITP) iliyokuwa inasimamiwa na hayati Profesa Tolly Mbwete.

Programu hii ililenga pamoja na mambo mengine, kuongeza idadi ya wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kwa kiasi kikubwa wanafunzi tulikuwa hatuungi mkono programu hii, kwa kuwa ilikuwa inasababisha msongamano mkubwa madarasani na kusisitiza kuwa hapakuwa msongamano wowote.

Kama kawaida yake, Profesa Luhanga akawa anatupa changamoto kwamba wanafunzi tulete ushahidi wa kisayansi, kama kweli kulikuwa na msongamano madarasani.

Kufuatia changamoto ambayo Profesa Luhanga alitupa mara kwa mara kuhusu ushahidi wa kuwepo msongamano madarasani, niliamua kujipa ‘homework’.

Katika wiki moja ya Februari 1998 niliandaa diary (shajara) nikawa ninarekodi madarasa yote yaliyokuwa yamejaza wanafunzi kuliko uwezo wake. Nilianzia vyumba vya semina vilivyopo eneo la majengo ya sayansi ya jamii, nikaenda majengo ya mihadhara ya ATA na ATB, mihadhara ya sayansi, Kitivo cha Sheria na nikamalizia na majengo ya mihadhara ya Kitivo cha Uhandisi, wakati huo maarufu kama FOE.

Nilifanya kazi hii kwa wiki nzima na nikakusanya taarifa kuhusu idadi ya wanafunzi ukilinganisha na viti na meza zilizokuwepo. Kila darasa nilirekodi vizuri idadi ya wanafunzi, idadi ya viti, somo gani na mwalimu gani alikuwa anafundisha.

Siku ya Jumamosi ya Februari 7, 1998 ilikuwa ndiyo siku ya mkutano kati ya VC na wanafunzi wote uliofanyika katika ukumbi maarufu wa Nkrumah. Nilikuwa nimejiandaa kikamilifu kushiriki katika mkutano huu nikiwa na ‘nondo’ zangu kikamilifu kabisa.

Wanafunzi wengi walichangia lakini bila data, na Profesa Luhanga, kama kawaida yake ukiongea bila data, aliwararua hasa huku akiwabeza kwa hoja zao nyepesi. Bahati yangu nikapata nafasi ya kuongea.

Niliposimama nilijitambulisha na kuanza kueleza jinsi ambavyo ITP ilikuwa imeleta shida na ilikuwa inaharibu kabisa sifa ya kitaaluma ya UDSM. ‘Nikamwaga’ data hatua kwa hatua nikitaja darasa moja baada ya lingine, muda, somo na mwalimu aliyekuwa anafundisha.

Wanafunzi walishangilia sana, Nkrumah nzima ikalipuka kwa shangwe kubwa. Kilichoshangaza wanafunzi wengi ni pale Profesa Luhanga aliposimama na kusifia sana mchango wangu, akisema huo ndio usomi anaotarajia kutoka kwa mwanafunzi wa Mlimani.

Baada ya hapo hakuchukua muda mrefu akafunga mkutano, akiahidi kwenda kuzifanyia kazi changamoto zilizoibuliwa, hasa za upungufu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa wasingeacha programu ya ITP kwa sababu ya changamoto, bali wataendelea kuitekeleza huku wakitatua changamoto hizo hatua kwa hatua.

Tukio la pili linahusu ziara ya Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyoifanya siku ya Jumanne ya Februari 16, 1999. Kufuatia taarifa za ujio wa Rais Mkapa chuoni, Profesa Luhanga aliniita ofisini kwake Februari 11, 1999 kwa malengo mawili.

Mosi, aliniita kunipa taarifa kuhusu ujio wa Rais Mkapa kama kiongozi wa wanafunzi.

Pili, alinitaka niwasilishe kwake majina ya wanafunzi ambao wangeuliza maswali siku hiyo na maswali ambayo wangeuliza ili wayawasilishe kwa Rais kwa ajili ya maandalizi.

Nilimshukuru kwa taarifa lakini nilikataa wazo lake la kuwasilisha majina ya wanafunzi na maswali watakayouliza. Nikamshauri kuwa maswali yaje tu ‘naturally’ pale pale ukumbini baada ya Rais kuhutubia.

Hatukukubaliana na tukaachana bila kuelewana kuhusu jambo hili. Aliendelea kunitafuta wiki nzima akisisitiza niwasilishe majina ya wanafunzi na maswali yao. Nami niliendelea kung’ang’ania msimamo wangu.

Hadi siku ya ziara ya Rais Mkapa, Jumanne ya Februari 16, 1999, hapakuwa na majina wala maswali kutoka kwa wanafunzi.

Hatimaye majira ya mchana saa nane Rais Mkapa aliwasili chuoni na kulakiwa na viongozi wa chuo, nikiwemo mimi kama Rais wa Daruso. Tukaingia ukumbi wa mikutano wa Baraza la Chuo (Council Chamber) kumpa Rais Mkapa taarifa za awali kabla hajaelekea ukumbi wa Nkrumah.

Katika maelezo yake Profesa Luhanga akashauri kuwa kungekuwa na kipindi cha maswali na majibu ambacho kwa ushauri wake ilikuwa ni kwamba, Rais angekiongoza mwenyewe na atakapoona inatosha atamaliza mkutano. Rais alikubaliana naye na tukaelekea Nkrumah.

Rais Mkapa alitoa hotuba nzuri sana na wanafunzi wakamshangilia, pamoja na kwamba hatukuridhishwa na maelezo yake kwamba kipaumbele chake kikubwa kilikuwa ni uchumi na sio elimu kama ambavyo sisi wanafunzi tungependa iwe. Ilipofika kipindi cha maswali na majibu Rais Mkapa alijibu kwa umahiri mkubwa.

Baadaye nilipokutana naye Profesa Luhanga, alicheka sana akaniambia kuwa mawazo yangu kuhusu wanafunzi kutowasilisha maswali yalikuwa sahihi, na kisha akanitania akisema kuwa ‘au ulikuwa unawasiliana naye’!!

Mpaka hapa tunaona kwamba Profesa Luhanga alikuwa ni kiongozi mlezi. Aliweza kuuona msimamo wangu na kuona kwamba, ni jambo jema hata kama hakukubaliana na msimamo wangu.

Itaendelea kesho

Advertisement