Kesi ya maofisa usalama feki yakwama kusikilizwa kwa mara ya tano

Muktasari:
- Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imekwama kuendelea kusikiliza ushahidi katika kesi ya kujifanya maofisa Usalama wa Taifa inayomkabili mfanyabiashara Joshua Kamalamo (37) na Yahaya Kapalatu (31) baada ya upande wa mashtaka kutokuwa na shahidi.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imekwama kuendelea kusikiliza ushahidi katika kesi ya kujifanya maofisa Usalama wa Taifa inayomkabili mfanyabiashara Joshua Kamalamo (37) na Yahaya Kapalatu (31) baada ya upande wa mashtaka kutokuwa na shahidi.
Hii ni mara ya tano kesi hiyo ya jinai namba 99 ya mwaka 2021 kuahirishwa ndani ya mwezi mmoja ikiwa katika hatua ya usikilizwaji kutokana na upande wa mashtaka kutokuwa na shahidi.
Juni 8, 2022 kesi hiyo iliahirishwa baada ya upande wa mashtaka kutokuwa na shahidi, Juni 14, Juni 15, Juni 16 na leo Juni 20, 2022 kesi hiyo pia imeshindwa kuendelea kwa sababu hiyo.
Kamalamo na Kapalatu wanadaiwa kujitambulisha kwa kurugenzi wa mashtaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu na naibu wake, Joseph Pande kuwa wao ni maofisa wa usalama wa Taifa wakati wakijua kuwa ni uongo.
Wakili wa serikali mwandamizi, Grace Mwanga leo Jumatatu Juni 20, 2022 ameiieleza mahakama hiyo mbele ya hakimu mkazi mfawidhi, Godfrey Isaya kuwa shauri hilo liliitwa kwa ajili kuendelea na ushahidi lakini kwa bahati mbaya wameshindwa kupata shahidi hivyo kuomba ahirisho fupi hadi Juni 28,2022.
Mwanga baada ya kueleza hayo wakili wa utetezi, Marietha Mollel amedai hana pingamizi juu ya ombi lililotolewa na upande wa mashtaka.
Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, Isaya ametaka upande wa mashtaka kuhakikisha siku hiyo wanakuwa na mashahidi ya kutosha na kasha kuahirisha kesi hiyo.
Tayari shahidi mmoja wa upande wa mashtaka ameshatoa ushahidi dhidi ya washtakiwa hao.
Katika kesi ya msingi washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 99/2021 ambapo wanadaiwa kutenda makosa hayo Juni 12, 2021 katika ofisi za DPP zilizopo katika jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani.
Inadaiwa siku hiyo washtakiwa wakiwa katika ofisi hiyo, walijitambulisha kwa Mwakitalu na Pande kwamba wao ni maofisa usalama wakati wakijua kuwa ni uongo.