Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kilio ubambikiaji wa bili za maji kumalizika

Kilio ubambikiaji wa bili za maji kumalizika

Muktasari:

  • Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameagiza mchakato wa kufunga mita za maji za Luku uende haraka, ili kuondoa malalamiko ya ubambikiaji wa bili za ankara za maji nchini.

Dodoma. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameagiza mchakato wa kufunga mita za maji za Luku uende haraka, ili kuondoa malalamiko ya ubambikiaji wa bili za ankara za maji nchini.

Akizungumza juzi na wahariri wa habari mkoani hapa, Aweso alisema kutokana na malalamiko kutoka kwa wateja, hivi sasa wameamua kuja na mita za maji za Luku.

“Kikubwa, huu ni uthubutu ambao tumeona tunaweza tukafanya, tumeona kwenye umeme watu wana mita za Luku, kwa nini sisi wa maji tushindwe?” alihoji.

Alisema katika suala hilo, wamepata wadau wengi na teknolojia nyingi, hivi sasa wanafanya tathmini ya wadau hao na teknolojia.

Aweso alisema kikubwa wanachozingatia katika mchakato wa kutumia mita za Luku ni ubora na gharama halisi.

Hata hivyo, aliwaagiza wasaidizi wake kuhakikisha mchakato huo unakwenda kwa haraka ili wadau waweze kupatikana na kumaliza kero za ubambikiaji wa bili za maji.

Aidha, alisema hivi sasa hakuna sababu ya kumbambikia bili mteja kwa sababu wasomaji mita wanaweza kuwashirikisha wananchi katika usomaji wao.

Aliwataka wasomaji mita kote nchini kuzisoma kwa weledi kwa kuwashirikisha wananchi kabla ya kuwapelekea bili zao.

“Kama mwananchi ametumia maji ya Sh20,000 mwache alipe hiyo,” alisema.

Kuhusu uvujaji wa maji, Aweso alisema hilo ni jukumu la kila mmoja na kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa maji nchini.

Pia aliwataka wataalamu kutatua changamoto za wateja na kwamba, kiwango cha uvujaji wa maji kwenye mamlaka hakitakiwi kuzidi asilimia 20.

Waziri huyo alisema watakuwa na kampeni maalumu ya uvujaji wa maji kwa maana ya kuwapo kwa utoaji taarifa pamoja na uwepo wa kikosi kazi.

“Mwananchi anaweza kusema mimi naletewa bili kubwa, wanaweza wakaenda watu wetu kwa upande wetu mambo yakawa sawa lakini maji miundombinu ni chakavu,” alisema.

Aidha, aliwataka makandarasi watakaopewa miradi ya maji nchini kufanya kazi hizo kwa uaminifu ili iweze kukamilika.


Miradi kichefuchefu

Mkurugenzi wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira katika Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), Mkamwa Bwire alisema miradi 177 ilibainika kuwa ya kichefuchefu, lakini hadi kufikia Juni mwaka huu 115 ilikuwa imekamilika na kufanyiwa marekebisho.

Alisema miradi iliyobaki 62 inatarajiwa kurekebishwa ifikapo Desemba 2021 na hivyo kuwa na na ongezeko la upatikanaji maji.

Pia Mkamwa alisema Ruwasa imepata bajeti ya Sh450 bilioni na wanatarajia kutekeleza mikataba 1,176 katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Alisema kati ya miradi hiyo 779 itatekelezwa na wakandarasi na 397 itafanywa na wataalam wa ndani na kwamba kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza upatikanaji wa maji kwa asilimia 3.7.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Duwasa) Aron Joseph alisemautekelezaji wa miradi mbalimbali ya kuongeza uzalishaji wa maji jijini Dodoma umeongeza uwezo wa kuhudumia wateja na hivyo kupunguza mgao wa maji.

Alisema Januari hadi Mei mwaka huu walikuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi kwa saa tano kwa siku lakini hadi sasa saa 10.