'Lowassa hakutafuta Kura milioni 6 pekee yake'

Muktasari:

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Lowassa alipokewa kwa shangwe nyumbani kwake wilayani Monduli mkoani Arusha baada ya kurejea CCM na kuwaomba Watanzania waliompigia kura katika uchaguzi mkuu uliopita kumuunga mkono, Rais John Magufuli.

Dar es Salaam. Ikiwa ni siku chache tangu waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ajitoe Chadema na kurudi CCM huku akijivunia kuwa na mtaji wa kura milioni sita, wasomi na wanasiasa wamezungumzia mwelekeo wa kura hizo sambamba na umaarufu wake kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Lowassa alipokewa kwa shangwe nyumbani kwake wilayani Monduli mkoani Arusha baada ya kurejea CCM na kuwaomba Watanzania waliompigia kura katika uchaguzi mkuu uliopita kumuunga mkono, Rais John Magufuli.

“Nimerudi nyumbani msiniulize nimerudi kufanya nini, nimerudi nyumbani,” alisema Lowassa huku akiwapungia mkono wafuasi wa CCM walioripuka kwa shangwe na vigelegele.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa siasa wanaona Lowassa kama ameshuka kisiasa na amebaki kujifariji. “Namuonea huruma sana Lowassa kwa sababu ameshachoka kisiasa,” alisema Deus Kibamba ambaye ni mchambuzi wa masuala ya siasa na mwanaharakati wa mabadiliko ya Katiba.

“Anaongea utafikiri zile kura milioni sita alizitafuta peke yake. Kule Chadema alikokwenda hakukuta sifuri hata Rais hawezi akasema kura zake zimuunge mkono fulani,” alisema.

Akifafanua zaidi, Kibamba alisema kuna vigezo kadhaa vya watu kupiga kura miongoni mwake ni kumpenda mgombea ambaye ana asilimia 10; watu kukipenda chama husika; kupenda muungano wa vyama vya siasa na wengine kupiga kura za mgomo kuonyesha chuki kwa mgombea mbadala.

“Kigezo kingine ni mazingira yaliyopo leo. Mfano ukiitisha kura leo watu wamepigika, hawaruhusiwi kufanya mikutano, wamebanwa, itakuwa tofauti na mwaka 2015. Kingine watu hupenda kupigia kura upande unaoelekea kushinda,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu alisema mikakati ya mapambano yao ni siri na wana uhakika inaisumbua CCM.

“CCM wanajua ndiyo maana wanahangaika hawalali tuko imara na tutawashangaza katika uchaguzi huu,” alisema Mwalimu.

Hata hivyo, mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dk Richard Mbunda alisema katika kura milioni sita za Lowassa kunaweza kukawa na baadhi ya watu wenye mapenzi naye hata kama hatagombea.

“Kuna asilimia fulani itaendelea kumuunga mkono, lakini kuna kura za wapinzani alizopata sidhani kama watamfuata. Kuna wengine walipiga kura kutokana na mazingira ya wakati ule wakitaka tu CCM iondoke madarakani.

“Kimsingi Lowassa hawezi akasema bado ana kura milioni sita, kwanza yeye siyo mgombea,” alisema Dk Mbunda.

Miongoni mwa watu waliokuwa bega kwa bega na Lowassa tangu akiwa CCM ni aliyekuwa kiongozi wa kundi la For U Movement ambaye sasa hivi ni mkuu wa idara ya uenezi makao ya Chadema Hemed Ali ambaye alikiri Lowassa kuwa mlezi wake kisiasa tangu wafahamiane.

“Lakini ningependa kumbukumbu itunzwe kuwa katika kujiunga kwetu binafsi nikiwa naongoza vuguvugu (movement) la vijana maarufu kama 4U Movement - Friends of Lowassa tulitangulia Chadema baada ya mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya CCM na kukata jina lake,” alifafanua Ali.