Lowassa kutikisa uchaguzi CCM

Monduli. Fikiria nguvu aliyokuwa nayo Edward Lowassa ndani ya CCM miaka mitatu iliyopita, siku moja baada ya kukihama chama hicho alifuatwa na wanachama 54 wa CCM wilayani Monduli.

Haikuwa Monduli tu, maeneo mbalimbali nchini wanachama wa CCM kuanzia wenyeviti wa mikoa, wilaya, vijiji na makada wa kawaida walimfuata Chadema. Sasa amerejea CCM baada ya kuhudumu Chadema kwa siku 1,312.

Mbali na kutangaza kurejea CCM, kada huyo aliyewahi kushika nafasi kadhaa za uongozi serikalini na kwenye chama hicho, amewataka Watanzania zaidi ya milioni sita waliompingia kura katika Uchaguzi Mkuu 2015 wamuunge mkono Rais John Magufuli.

Kurejea kwake huenda kukatikisa viongozi kadhaa wa CCM Wilaya ya Monduli walioingia madarakani kipindi Lowassa akiwa upinzani, hasa katika kupitisha majina ya wagombea wa CCM kwenye uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.

Kwa kiasi fulani kurejea kwake CCM, kunaweza kuyatikisa hata maeneo mengine kwani makada ambao wamekuwa wakihama kwa kufuata upepo wake, wanaweza kumfuata tena jambo ambalo litaleta ushindani katika chama hicho kwenye uchaguzi wa serikali za mtaa mwaka huu na uchaguzi mkuu.

Taarifa zinasema waliohama na Lowassa baadhi yao wataingia kwenye kinyang’anyiro cha kugombea nafasi za uongozi ngazi za serikali za mitaa, vijiji, udiwani na ubunge.

Lowassa alijiengua CCM Julai 28 mwaka 2015, baada ya jina lake kuenguliwa katika urais na hivyo akajiunga na Chadema na kupewa fursa ya kugombea urais akiungwa mkono kupitia muungano wa Ukawa ulioundwa na NCCR Mageuzi, NLD, CUF na Chadema.

Katika uchaguzi huo wa 2015, Lowassa alishika nafasi ya pili nyuma ya Rais Magufuli kwa kupata zaidi ya kura milioni sita ambazo ni nyingi kuliko mgombea mwingine yeyote wa upinzani tangu mfumo wa vyama vingi urejee nchini 1992.

Lakini, uchunguzi uliofanywa na Mwananchi wilaya Monduli umebaini kuwa tangu Lowassa kuondoa CCM mwaka 2015, chama hicho Wilaya ya Monduli kimekuwa na mgawanyiko, baada ya viongozi wengi waliokuwa na waziri mkuu huyo wa zamani kujiengua CCM, akiwapo aliyekuwa mwenyekiti wa wilaya hiyo, Reuben Ole Kuney.

Hali hiyo ilitikisa maeneo mbalimbali nchini kiasi kwamba viongozi na makada kadhaa wa CCM walijikuta wakisimamishwa, kufukuzwa au kuonywa na chama hicho kwa madai ya usaliti.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, makundi ya viongozi wa CCM wilayani Monduli, wakiwamo waliokuwa wamejiengua baadhi yao walikuwa wamevalia sare za chama hicho na kukabidhiwa kadi huku wakitakiwa kufuata utaratibu rasmi wa kujiunga tena na chama hicho.

Mbunge wa Jimbo la Monduli, Julius Kalanga alikiri kuwa kuondoka kwa Lowassa, kulileta mgawanyiko ambao haukuwa na sababu katika jimbo hilo, lakini sasa mshikamano unatarajiwa kurejea.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Loata Sanare akizungumza wakati wa kumpokea Lowassa alisema CCM ambayo aliiacha imeimarika zaidi na alimkaribisha huku akimuhakikishia CCM mkoa kushirikiana naye katika utekelezaji wa Ilani ya chama.

“ Tumewaona hapa watu waliokuwa wamejiengua, lakini sasa wamevaa sare za CCM, lazima wafuate utaratibu kama Lowassa, kwanza kuomba kurejea kupitia ngazi ya tawi na baadaye kujadiliwa na vikao vya tawi baadaye vikao vya kata na kikao cha kamati ya siasa ya wilaya,” alisema.

Sanare ambaye aliwahi kuwa katibu mwenezi wa CCM Wilaya ya Monduli, pia amekuwa akitajwa pamoja na watoto wa hayati Edward Moringe Sokoine, Namelock Sokoine na Joseph Sokoine huenda wakajitokeza kugombea ubunge katika jimbo hilo mwaka 2020.

Katika uchaguzi uliopita mwaka 2015, Namelock alichuana na Julius Kalanga ambaye alikuwa Chadema na kushindwa.

Kabla ya Kalanga kugombea ubunge kupitia upinzani, aliwahi kuwa diwani wa CCM kata ya Lepurko na mwenyekiti wa jumuiya ya vijana wa CCM Wilaya ya Monduli. Mwaka jana Kalanga alihamia CCM na kushinda tena kiti cha ubunge.

Kurejea CCM kwa Lowassa kunarejesha mchuano mkali kwa wanaCCM Monduli mwaka 2020, kwani Lowassa ambaye alikuwa mbunge kwa zaidi ya miaka 25 anaushawishi mkubwa kama itakavyokuwa katika maeneo mbalimbali.

Akizungumza na umati wa wanaCCM, ambao walifika kumpokea wilayani Monduli, Lowassa alieleza kufurahi kurejea nyumbani, huku akiwataka wote kushirikiana kumuunga mkono Rais John Magufuli ambaye anafanya kazi nzuri kuliletea maendeleo taifa.

Katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole licha ya kumpongeza Lowassa kwa ukomavu wa kisiasa kwa kutanguliza mbele masilahi ya taifa aliwataka wanaCCM kusameheana na kushiriki kukijenga chama hicho.

Polepole alisema Taifa kwa sasa linataka amani, mshikamano, umoja na kusonga mbele