VIDEO: Lowassa: Msiniulize kwa nini nimerudi

Monduli. Safari ya maisha ya wanasiasa nguli, Edward Lowassa ndani ya CCM ilianza rasmi jana baada ya kukabidhiwa kadi na kusema, “Nimerudi nyumbani (CCM), msiniulize nimerudi kufanya nini, nimerudi nyumbani.”

Kelele za shangwe zilitawala katika viwanja vya CCM Wilaya ya Monduli mkoani Arusha ambako alikabidhiwa kadi ya CCM baada ya kuiweka kando Julai 28, 2015 alipotimkia Chadema.

Shughuli ya kumpokea ilianza tangu asubuhi alipopokewa katika Uwanja wa Ndege Arusha kisha safari ya kwenda Monduli, nyumbani kwake kuanza huku akisindikizwa na makumi ya bodaboda na na magari.

Lowassa ambaye ni waziri mkuu wa zamani alitimkia Chadema baada ya kutoridhishwa na mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya CCM. Baada ya kuhamia huko alipitishwa kugombea urais akiungwa mkono na vyama washirika wa Ukawa.

Hatua ya Lowassa kwenda upinzani, ilitoa ushindani mkubwa kwa CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015 kwani mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli aliibuka mshindi kwa kupata kura milioni 8.88 sawa na asilimia 58.46 huku Lowassa akipata kura milioni 6.72 sawa na asilimia 39.97, tofauti ya kura ambayo haikuwahi kutokea tangu uchaguzi ulioshirikisha vyama vingi vya siasa ulipoanza mwaka 1995.

Hata hivyo, safari ya Lowassa kubaki upinzani ilikoma Machi Mosi katika ofisi ndogo za CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam alipotangaza kurudi nyumbani mbele ya viongozi wa chama hicho wakiongozwa na mwenyekiti wake, Rais Magufuli.

Jana, akiwahutubia mamia ya wanaCCM akiwa amekaa katika ofisi za chama hicho Wilaya ya Monduli alisema, “Nimerudi nyumbani (CCM), msiniulize nimerudi kufanya nini, nimerudi nyumbani. Narejea nyumbani kwa sababu zilezile zilizonifanya niondoke miaka takriban minne iliyopita; kupigania mabadiliko yenye dhamira ya kujenga umoja wa kitaifa.”

Mbunge huyo wa zamani wa Monduli alisema, “Nawashukuru sana Chadema na neno langu ni moja tu, nasema asante msinilishe maneno.”

Hakuishia hapo, huku akishangiliwa alisema, “Nimekuja kuwaomba wote mumuunge mkono Rais John Magufuli, mimi niligombea urais uchaguzi uliopita, nilipata kura milioni sita sio kidogo, nawaomba mlionipigia kura mumpe kura hizo Rais John Magufuli.”

Alisema kuna maneno mengi yatasemwa lakini kikubwa ni kumuunga mkono Rais Magufuli na kumpa ushirikiano ili aweze kuendelea na kazi.

Lowassa alisema amerudi CCM baada ya kushawishika na kazi nzuri ambazo anazifanya Rais Magufuli huku akiwashukuru sana Chadema.

Alikemea ubaguzi wa kidini na kisiasa akisema unaanza kujitokeza akisema ni jambo baya linalopaswa kukemewa.

Lowassa ambaye alisindikizwa na mke wake, Regina na mwanaye, Fred kwenye mkutano huo, alisema uamuzi wake wa kurejea CCM haukueleweka haraka kwa mkewe.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alitaka watu kusamehe yaliyopita huku akimpongeza Lowassa kwa ukomavu wa kisiasa.

“Kitendo alichokifanya ndugu Lowassa ni ukomavu wa kisiasa, ametangaza tutangulize mbele masilahi ya taifa hili na kuilinda amani yetu,” alisema

Katika mkutano huo, mbunge wa zamani wa Longido (Chadema), Onesmo Ole Nangole alirejea CCM pamoja na wanachama wa upinzani zaidi ya 30.

SAHIHISHO

Katika toleo la jana, tuliandika habari iliyomkariri Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shaaban Mdoe akimtaja Meya wa Arusha, Calist Lazaro kuwa miongoni mwa viongozi wa upinzani ambao wangejiunga na chama hicho kumuunga mkono Lowassa ni. Hata hivyo, tumejiridhisha kwamba Mdoe hakutoa taarifa hiyo badala yake alieleza kwa ujumla kwamba wanachama wengi wa upinzani wangejiunga na CCM jana. Tunaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza kutokana na kosa hilo. Mhariri