Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sagini awapa somo watumishi wapya Ofisi ya Mashtaka Taifa, DPP asema…

Muktasari:

  • Watumishi wapya 143 wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wamefundwa kuhusu misingi ya maadili, uwajibikaji na utendaji wenye tija na ufanisi huku Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini, akisema kuwa taasisi hiyo ni mhimili wa haki za kijamii hivyo lazima wafanye kazi kwa weledi.

‎Iringa. Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne  Sagini ametoa onyo kwa watumishi wapya 143 wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka akiwataka kuzingatia miiko, maadili na utendaji wenye weledi wakati wote wa kazi zao ili kulinda heshima ya ofisi hiyo muhimu kwa mustakabali wa haki nchini.‎

‎Sagini ameyasema hayo leo Alhamisi Julai 2, 2025 katika semina maalumu ya mafunzo kwa watumishi hao wapya iliyofanyika ofisi za mkuu wa Mkoa wa Iringa. ‎

‎Aamesema ofisi hiyo ni chombo nyeti chenye jukumu la kutafuta haki kwa niaba ya umma hivyo haiwezi kuwa mahala pa uzembe au matumizi mabaya ya dhamana ya umma.‎

‎“Mnawajibika kisheria na kimaadili. Ofisi hii ndiyo mlango wa haki katika mashauri ya jinai nchini na ukifanya kazi kwa mazoea au bila uadilifu, unahatarisha haki za watu na kuharibu taswira ya Serikali,” amesema Sagini huku akisisitiza kuendelea kujifunza na kusoma sheria kwa bidii.‎

‎Naibu Waziri huyo amesema Serikali ya awamu ya sita imejipanga kuhakikisha inaboresha utendaji katika sekta ya sheria kwa kuimarisha taasisi zake, hivyo ni wajibu wa kila mtumishi mpya kuhakikisha anafanya kazi kwa bidii na nidhamu ya hali ya juu.‎

‎Katika hotuba yake, Sagini pia amewataka viongozi waandamizi wa ofisi hiyo kuwa mfano wa kuigwa na kuhakikisha wanawaongoza vijana hao kwa maadili na kushirikiana nao kikamilifu katika kuwahudumia wananchi.‎

‎“Mabadiliko tunayoyahitaji hayawezi kuja kwa maneno, bali kwa vitendo," amesisitiza.

‎Awali, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Sylvester Mwakitalu amesema semina hiyo inalenga kuwawezesha waajiriwa hao kuielewa vizuri dhima ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na namna ya kushiriki ipasavyo katika kutoa haki kwa umma.

‎‎“Tumewakutanisha hapa ili kabla hamjaingia rasmi kazini, muijue falsafa ya ofisi yenu, hatuwezi kukubali kufanya kazi kwa mazoea, tunataka matokeo. Sheria ziko wazi, lakini dhamira ya mtumishi ndiyo msingi wa utekelezaji wake,” amesema Mwakitalu.

‎‎Akiangazia maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Mwakitalu amewakumbusha wananchi kuepuka makosa ya jinai yanayoweza kujitokeza kipindi hicho, akisema ofisi yake itakuwa makini zaidi katika kushughulikia mashauri ya ukiukwaji wa sheria za uchaguzi.

‎‎“Tunajua kipindi cha uchaguzi kuna changamoto nyingi hivyo tunawaomba wananchi wote wawe makini, tutachukua hatua kali,” ameonya Mwakitalu.

‎‎Katika semina hiyo, baadhi ya waajiriwa wapya wameeleza namna mafunzo hayo yatawapanua uelewa kuhusu wajibu wao, weledi na jinsi ya kushughulikia mashauri kwa haki na bila upendeleo.‎

‎‎Mafunzo hayo yameanza Juni 30, 2025 na yanatarajiwa kumalizika kesho Ijumaa Julai 4, 2025.