Mabaki yanayodaiwa ni mwili wa mwalimu aliyepotea 2006 yapatikana
Muktasari:
- Alison Mcharo, mkazi wa kijiji cha Mpinji wilayani Same mkoani Kilimanjaro, alipotea mwaka 2006 baada ya kupokea mafao yake ya kustaafu ualimu lakini sasa imebainika kuwa aliuawa na kuzikwa katika makaburi ya familia yake.
Moshi. Inawezekana likawa ni moja ya tukio la nadra kutokea nchini. Alison Mcharo aliyepotea mwaka 2006 imebainika kuwa aliuawa na kuzikwa katika makaburi ya familia yake.Mcharo aliyekuwa mkazi wa Kijiji cha Mpinji, Kata ya Mamba Myamba wilayani Same, alipotea baada ya kupokea mafao yake ya kustaafu kazi ya ualimu.
Inadaiwa kuwa Mcharo alitoweka baada ya kufika nyumbani na hakuonekana tena.
Jana, Polisi Mkoa wa Kilimanjaro walisema kuwa wamewatia mbaroni mkewe, Nasemba Alison (80) na mtoto wake, Orgenes Alison (45) wakiwatuhumu kwa mauaji hayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Hamis Issah alisema mabaki ya mwili wa Mcharo yaligunduliwa Jumapili iliyopita, jirani na kaburi la baba yake mzazi.
Kamanda Issah alidai kuwa uchunguzi wa awali uliofanywa na polisi unaonyesha kuwapo kwa ushiriki wa mkewe katika kupanga na kutekeleza mauaji hayo kwa kile alichodai ni tamaa ya fedha.
Haikufahamika mara moja kiasi cha fedha ambacho marehemu alilipwa baada ya kustaafu.
“Uchunguzi wetu wa awali umebaini marehemu aliuawa baada ya kukabidhiwa mafao yake na waliohusika waliingia tamaa baada ya kuona fedha nyingi alizokuwa amekabidhiwa.
“Baada ya kupokea mafao yake na kurudi nyumbani, ndipo aliuawa lakini taarifa ikatolewa kuwa amepotea. Mkewe baada ya kuhojiwa amejieleza vizuri...,” alidai kamanda huyo.
Alisema ripoti ya kupotea kwake ilitolewa polisi mwaka 2006 na kipindi chote cha miaka 12, alitafutwa bila mafanikio hadi Jumapili iliyopita mabaki ya mwili wake yalipoonekana.
Mwili wake uligundulikaje?
Kugundulika kwa mabaki ya mtu anayedaiwa kuwa ni Mcharo kulianzia kwenye kifo cha mama yake mzazi ambaye alikuwa ameacha wosia kuwa azikwe jirani na alipozikwa mumewe.
Kamanda Issah alisema ndugu na jamaa walikwenda kuchimba kaburi eneo ambalo marehemu aliacha wosia, lakini walishtuka kukuta mabaki ya mwili wa mtu mwingine katika eneo hilo.
“Kulikuwa hakuna alama yoyote kama kuna kaburi, lakini cha ajabu walikuta mabaki ya mtu, hapo waliacha kuchimba kaburi na kutoa taarifa Polisi kwa sababu ukikuta kaburi huwezi kuendelea kuchimba.
“Baada ya polisi kupata taarifa hizo tuliomba kibali cha Mahakama na tulipochimba eneo lile, kweli yalionekana mabaki ya mwanadamu na kulionekana kuna tai na shati.
“Hizo nguo zilitambuliwa kuwa ni za mwalimu Mcharo ambaye alidaiwa kupotea na alikuwa hajulikani alipo tangu mwaka, 2006.
“Jambo lingine lililotushangaza tulipofukua kaburi, tulikuta mabaki yale yamekaa mkao ambao si wa maiti inavyozikwa. Ilikuwa kwenye mkao ambao si wenyewe kama taratibu za maziko zilivyo,” alidai Kamanda Issah.
Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi wa kisayansi ikiwamo kuchukua sampuli za mifupa ili kuthibitisha kisayansi kuwa ni ndiye.