Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mawakili wadai washitakiwa wawili hawahusiki tuhuma za utakatishaji fedha

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Igunga, Athuman Msabila akipanda ndani ya gari kwa ajili ya kurudishwa mahabusu baada ya kumalizika kwa kesi katika Mahakama ya Wilaya Kigoma leo.  Picha na Happiness Tesha

Muktasari:

  • Washitakiwa 11 wanakabiliwa na mashtaka 11  likiwamo la utakatishaji wa Sh463.5 milioni

Kigoma. Mawakili wa upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili  watuhumiwa 11 akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Igunga, Athuman Msabila wamewasilisha hoja  ya kuwatoa kwenye kosa la utakatishaji fedha  washtakiwa namba mbili na tatu kwa madai ya kutohusika na shitaka hilo namba 10.

Washtakiwa hao wanaodaiwa kutohusika na kosa hilo ni Aidan Mponzi na Tumsifu Kachira kutoka Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) Dodoma.

Katika kesi hiyo, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 11 likiwamo la utakatishaji wa Sh463.5 milioni.

Kesi hiyo imefika leo katika Mahakama ya Wilaya Kigoma kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mfawidhi  wa Mahakama ya hiyo, Hassan Momba.

 Wakiwasilisha hoja hiyo, mawakili wa utetezi wakiongozwa na wakili Sadiki Aliki anayemtetea mshtakiwa wa kwanza, wa pili, watatu, wa tano na wa tisa, amesema miongoni mwa mashitaka waliyokuwa wameshitakiwa watuhumiwa hao ni utakatishaji fedha.

 Amesema hoja yao ipo katika shitaka la utakatishaji fedha ambalo ni namba 10 kwenye hati ya mashitaka.

Wakili Aliki amesema kifungu cha 12 kifungu kidogo cha 1(a) cha Sheria ya Kuzuia Utakatishaji fedha kimeeleza  ili mtu ashitakiwe kwa kosa la kutakatisha fedha ni lazima awe amehusika na kosa lingine linalokuwa limesababisha kutakatisha fedha.

 Amedai kuwa hoja yao ni kwamba, ukisoma maelezo ya shitaka hilo la 10 inabainisha wazi kama ilivyo katika kifungu cha Sheria ya Kuzuia Utakatishaji Fedha na ukiangalia kwenye hati kuna kosa la kughushi ambalo lipo kwenye kosa la nne, tano na la sita katika hati hiyo ya mashitaka.

 Wakili Aliki amesema suala hilo liko wazi kwa kuwa mshtakiwa wa pili na wa tatu hawahusiki na kosa hilo namba 10 la utakatishaji fedha kwa sababu katika kosa la  nne, tano na sita ya kughushi wao hawajatajwa.

“Kwa msingi wa kifungu cha sheria nilichotaja cha kuzuia utakatishaji fedha hawapaswi kuwepo kwenye hilo kosa namba 10 la utakatishaji fedha, tumeona tuibue hii hoja mahakamani na kwamba mtu akiwa na kosa hilo hawezi kupewa dhamana na Mahakama,”amesema wakili Aliki.

 Pia, amesema madhara yake ni makubwa kwa kuwa mtu atakaa mahabusu muda mrefu wakati jambo hilo linaweza kuonekana kwa macho na kama washtakiwa hao hawana kosa, Mahakama inaweza kuliangalia hilo kwa kuwapa dhamana.

 Wakili Eliuta Kiviro akimuwakilisha mshtakiwa wa saba, wa nane na 11 ameomba upande wa jamhuri  kuharakisha upelelezi kukamilika ili shauri hilo lisikilizwe kwa kuwa athari za kutokamilika, shauri litakaa mahakamani muda mrefu bila kusikilizwa.

 “Kucheleweshwa kwa upelelezi huo ni kama unamuadhibu mtu pasipo kumkuta na hatia, kwa maana ya kukaa mahakamani au mahabusu kesi haisikilizwi kwa muda mrefu, ni kama anatumikia kifungo hata kabla hajatiwa hatiani, kwa hiyo tunaiomba Mahakama iwakumbushe upande wa jamhuri kufanya upelelezi mapema na kukamilisha kwa wakati,”amesema wakili Kiviro.

Upande wa jamhuri, uliwakilishwa na Wakili Flora Lukas akisema kuchelewa kwa shauri hilo kuna sababishwa na mazingira ya shauri hilo kwa kuhusiana na  mahesabu.

 Hakimu Mfawidhi Hassan Momba amesema hoja zilizowasilishwa mahakamani na upande wa utetezi zimepokewa na zitafanyia kazi.

Amesema ndani ya siku saba watatakiwa kuwasilisha hoja hizo kwa maandishi mahakamani hapo na Januari 26, 2024 uamuzi utatolewa.

 Washtakiwa watano ambao wametimiza masharti ya dhamana na wako nje ni Joel Shirima, Jema Mbilinyi, Kombe Kabichi na Frank Nguvumali wote kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na  Bayaga Ntamasambilo kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.

 Washtakiwa sita wanaoendelea kusota mahabusu ni Athuman Msabila, Aidan Mponzi na Tumsifu Kachira kutoka Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) Dodoma, Frednand Filimbi, Salum Juma na Moses Zahuye kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.

 Awali, shauri hilo lilifikishwa mahakamani hapo Novemba 7,2023 kwa tuhuma za kuhusika na makosa 11 yakiwamo ya kula njama kwa nia ya kutenda kosa, kughushi nyaraka, kutakatisha fedha na matumizi mabaya ya madaraka.