Mbunge CCM acharuka uvamizi wa tembo

Mbunge wa Singida Mashariki (CCM), Miraji Mtaturu
Muktasari:
Changamoto ya tembo kuvamia makazi ya watu imemuibua Mbunge wa Singida Mashariki (CCM), Miraji Mtaturu ambaye ametaka utafiti wa kina kufanyika ili kutatua changamoto hiyo anayodai inaitia doa nchi.
Dodoma. Mbunge wa Singida Mashariki (CCM), Miraji Mtaturu amecharuka bungeni kuhusu uvamizi wa tembo katika maeneo ya makazi ya watu kuwa unaitia doa nchi.
Mtaturu ameyasema hayo leo Ijumaa Juni 3, 2022 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2022/2023.
Amesema hivi karibuni tembo wamevamia katika kijiji cha Ntuntu kilichopo wilayani Ikungu mkoani Singida na kumkanyaga mtoto mdogo.
“Eneo hili la Ikungi ni mbali sana na hifadhi, leo hii Ikungi tunaanza kuwa na uvamizi wa tembo lakini mnatuambia kuwa tembo wanakaribia 60,000, mnasema ni wachache wakifika 100,000 hadi 200,000 itakuaje nchi hii,”amehoji.
Amesema miaka ya sasa inawafanya watu wengi kuumia, kufa na mali zao kuharibiwa na tembo wanaozunguka kwenye maeneo mbalimbali.
“Inawezekana wanahitaji kula mazao fulani, inawezekana hakuna maji katika hifadhi. Wataalamu wetu watumike kupanda mazao yanayohitajika ndani ya hifadhi ili tembo wasitoke kuja mtaani. Kama maji nimachache wachimbe mabwawa katika hifadhi,”amesema.
Mtaturu ameshauri utafiti kufanyika katika eneo hilo ili waachane na stori za kwamba ni mapito ya tembo ambalo limekuwa likitolewa na Serikali miaka yote.
“Najiuliza kule Ntuntu walikuwa wanaenda wapi hawa tembo. Tembo wamekaa wiki mbili wanawafanya wananchi washindwe kufanya kazi zao za kawaida. Tutajikuta tunahamasisha watu wafanye kazi lakini wanashindwa kwasababu tembo wanazunguka ni hatari kwa wananchi,”amesema.
Amewataka kutengeneza mkakati wa kitaalamu na kuachana na misamiati ambayo haueleweki kuwa hayo ni mapito, lugha ambayo inawasumbua wananchi na kuwatia doa kama nchi.