‘Mlinzi wa Mbowe’, wenzake watatu walivyoachiwa huru

Muktasari:

  • Miongoni mwa washirika wanne wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya walioachiwa huru juzi usiku na Mahakama baada ya kukiri kosa, ni aliyekuwa mlinzi wa Mwenyekiti wa ChademaTaifa, Antero Assey.


Moshi. Miongoni mwa washirika wanne wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya walioachiwa huru juzi usiku na Mahakama baada ya kukiri kosa, ni aliyekuwa mlinzi wa Mwenyekiti wa ChademaTaifa, Antero Assey.

Antero alikuwa mlinzi wa Mbowe kati ya mwaka 2011 na 2019 ambapo 2019 aliondoka kwenye idara ya ulinzi ya Chadema hicho na kwenda kugombea ubunge Babati Mjini kupitia Chadema na kuangushwa katika kura za maoni.

Washirika hao wa Sabaya waliachiwa huru baada ya kukubaliana na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) na kukiri makosa yao juzi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Moshi, Salome Mshasha na kutiwa hatiani.

Baada ya kukiri makosa ya uhujumu uchumi na kutiwa hatiani, kila mmoja aliamriwa kulipa Sh50,000 na Sh1 milioni kama fidia kwa muathirika ambaye ni Alex Swai na washitakiwa walilipa fedha hizo na kuachiwa huru.

Walioachiwa ni mhandisi Silvester Nyegu ambaye alikuwa msaidizi wa Sabaya, John Odemba, Nathan Msuya na Assey ambao ni wafanyabiashara.

Awali, wakisomewa hati mpya ya mashtaka ya kesi namba 32 ya mwaka 2022 baada ya kukiri kosa, wakili mwandamizi wa Serikali na mkuu wa mashtaka mkoa kutoka ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Mkoa wa Kilimanjaro, Halid Nuda alieleza kuwa washtakiwa wote wanne wanashtakiwa kwa makosa mawili.

Alisema kosa la kwanza ni kujitwalia madaraka pasipo uhalali kinyume na kifungu cha 99 (B) kifungu cha 35 cha sheria ya kanuni ya adhabu, sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

“Silvester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antero Assey pamoja na Lengai Ole Sabaya ambaye hajashtakiwa kwenye hati ya mashtaka inayoeleza mnamo Januari 19,2021 katika eneo la Mbosho Masama wilayani Hai, walitenda kosa hilo la upekuzi katika duka na nyumba ya Alex Swai wakiwa hawana mamlaka ya upekuzi,”alisema Nuda.

Washtakiwa hao kama iivyokuwa azma yao ya kujadiliana na DPP, walikiri kutenda kosa hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo,Salome Mshasha.

Alilitaja kosa la pili waliloshtakiwa nalo ni la kula njama ya kukandamiza haki. Alidai Januari 19,2021 na Machi kwa tarehe tofauti na maeneo tofauti wilayani Hai, Hoteli ya Tulia na Grand Melia Arusha, walimsababishia madhara Alex Swai.

“Mnamo Januari 19,2021 washtakiwa waliombwa na rafiki yao Sabaya, wakati sio watumishi wa umma na sio sehemu ya vikosi vya ulinzi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya upelelezi wa kukwepa kodi nyumbani na dukani kwa Alex Swai,”alisema Nuda.

“Mshtakiwa wa kwanza, pili, tatu na nne walimkamata Alex Swai kwa tuhuma za kukwepa kulipa kodi na kumfikisha kwa Lengai Ole Sabaya,majira ya jioni, tarehe hiyo hiyo washtakiwa pamoja na Sabaya walifika dukani kwa Alex Mbosho Masama na kufanya upekuzi katika duka na nyumba,”

“Walikamata fedha taslimu Sh16 milioni ,tablet 1,saa ya mkononi ,cheni ya shingoni ya dhahabu na hereni ndani ya nyumba ya Alex Swai na baada ya kivikamata walimkabidhi Lengai Ole Sabaya,”

Alieleza baada ya kivikamata vitu hivyo, Sabaya aliwaomba washtakiwa hao kumkamata mke wa Alex Swai, mama mzazi pamoja na dada yake ambapo walifanya hivyo, na baada ya kuwakamata waliwafikisha katika Kituo cha Polisi Bomang’ombe.

Mnamo Januari 23,2021 washtakiwa walimsaidia Sabaya kukutana na Godbless Swai (ndugu wa Alex) nyumbani kwake, ambapo Sabaya aliomba hongo ya Sh50 milioni ili atoe dhamana kwa Alex na ndugu zake.

“Washtakiwa hao kwa kujifanya ni maofisa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Idara ya Usalama wa Taifa (Tiss), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)na Jeshi la Polisi na kusema wanaweza kufanya tuhuma za kukwepa kodi kwa Alex Swai asishtakiwe,ambapo siku hiyo Sabaya alipokea Sh30 milioni kutoka kwa Godbless Swai,”

“Februari 2,2021 katika ofisi ya Sabaya walijifanya wao ni maofisa wa umma kutoka TISS,TRA,Takukuru na Jeshi la polisi na kumsaidia Lengai Ole Sabaya kujipatia Sh15 milioni kutoka kwa Godbless Swai na Februari 3 wakijifanya ni maofisa wa umma walimsaidia Sabaya kupata Sh8 milioni kutoka kwa Godbless,”

Alieleza kuwa katika tarehe isiyojulikana Februari 2021 katika Hoteli ya Grand Melia washtakiwa walimsaidia Sabaya kumshawishi kupokea rushwa ya Sh25 milioni kutoka kwa Godbless kwa kujifanya wao ni Maofisa kutoka TISS,Takukuru,TRA na Jeshi la Polisi kwamba wangeweza kumsaidia Alex Swai asishtakiwe kwa kosa la kukwepa kodi.

“Februari 9,2021 katika Hoteli ya Tulia washtakiwa walimsaidia Sabaya kujipatia Sh14 milioni kutoka kwa Godbless, ambapo waliisaidia familia ya Alex kupata dhamana Februari 24,2021 baada ya kuachiliwa Alex Swai aliripoti Takukuru ambapo upelelezi ulifanyika na Sabaya na wenzake kukamatwa,”alisema.

Baada ya maelezo hayo washtakiwa walikiri makosa hayo mbele ya hakimu Mshasha na kutiwa hatiani kwa makosa hayo mawili, ambayo walishtakiwa nayo mahakamani hapo na kutakiwa kulipa fidia ya Sh1 milioni kwa kila mshtakiwa na Sh50,000 kama adhabu ya fidia kwa kila mmoja.

“Washtakiwa wamekiri kosa na nimezingatia makubaliano kati yao na upande wa mashtaka, Mahakama inatoa amri kwa kila mmoja atalipa faini ya Sh50,000 kama adhabu na Sh1 milioni kwa kila mshtakiwa kama fidia kwa mhanga,niwatakie kila la kheri,”alisema Hakimu.

Wanasheria wafunguka

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanasheria mkoani Kilimanjaro walisema kuachiliwa kwa washtakiwa hao hakutaathiri kesi ya Sabaya kwa kuwa yapo makosa ambayo anatuhumiwa kuyafanya yeye kama yeye na aliyoshirikiana nao.

Akilizungumzia hilo, Wakili Patrick Paul alisema kukubali kosa kwa waliotenda kosa hakumtii hatiani mtenda kosa na badala yake ni kwamba inawarahisishia upande wa mashtaka kutekeleza kazi zao.

“Upande wa mashtaka umepata urahisi kwenye kumuweka Sabaya hatiani, lakini kwa makosa ambayo Sabaya anadaiwa alishirikiana na hao wanne upande wa mashtaka wanapata urahisi zaidi, lakini huo urahisi wakizembea unaweza kuwagharimu kwa sababu kuna sehemu Sabaya anasimama yeye kama yeye na sehemu nyingine ameshirikiana na wenzake,”alisema.

Kwa upande wa Wakili, Elia Kiwia alisema “Kuachiwa kwa washtakiwa hao hakuathiri kesi ya Sabaya kwa kuwa yapo makosa anayoshtakiwa nayo yeye kama yeye.

“Sabaya ana shtaka kubwa ndio lililomzuia labda haliruhusiwi kufanya makubaliano ya kukiri kosa, kwa hiyo hii haiwezi kuathiri kesi yake kwa sababu waliothibitisha shtaka sio washtakiwa ni Jamhuri,” alisema.