Mwili wa mwalimu aliyeuawa kuzikwa Iringa

Baadhi ya waombolezaji wakiwa nje ya nyumba ya marehemu Herieth Lupembe (37) katika Kijiji cha Mbugani Kata ya Kiwanja Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.

Muktasari:

Tukio la mauaji  limeleta huzuni kubwa kwa jamii iliyokuwa ikiishi na  Herieth kwa upendo na kushirikiana katika mambo mbalimbali

Mbeya.  Mwili wa  Herieth Lupembe(37) aliyekuwa Mwalimu wa Shule ya Msingi Mbugani Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya  unatarajia kusafirishwa leo Aprili 2, 2024 kwenda Iringa kwa mazishi baada ya kufanyiwa uchunguzi.

Pia, mwili wa aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Isenyela, Tatizo Haonga (16) utazikwa katika Kijiji cha Mbugani Kata ya Kiwanja  wilayani humo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbugani Gedion Kinyamagoha ameiambia Mwananchi leo Jumanne Aprili 2, 2024 kuwa, “kwa sasa tunasubiri  taratibu za  uchunguzi wa madaktari  zikikamilika miili itakabidhiwa  kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi huku mwili wa mwalimu Herieth ukisafirishwa Mkoa wa Iringa kwa mazishi. ”

Mwalimu Herieth Lupembe

Amesema tukio hilo limeleta huzuni kubwa kwa jamii iliyokuwa ikiishi na  Herieth kwa upendo na kushirikiana katika mambo mbalimbali.

“Kwa kweli tumepoteza mtu muhimu sana katika jamii yetu kikubwa tuendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ampe pumziko la milele huko aendako,”amesema.

Baba mzazi wa Tatizo aliyekuwa akiishi na mwalimu huyo, Fackson Simchimba amesema baada ya mazishi ya binti yake  watasafirisha msiba kwenda Mkoa wa Songwe.

Machi  31 mwaka huu  mwalimu na mwanafunzi huyo walikutwa wameuawa ndani ya nyumba waliyokuwa wakiishi  katika Kijiji cha Mbugani Kata ya Kiwanja Wilaya ya Chunya.

Wakati huohuo, Haris Barnabas (5) amejeruhuwa na kitu butu kichwani na kukimbizwa katika Hosptali ya Rufaa Kanda kwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema tukio hilo limetokea Machi 31 mwaka huu saa 2.30 usiku.

Kuzaga amesema  watu wasiojulikana  walivamia nyumbani kwa Herieth kisha kuwashambulia kwa vitu vyenye kali  maeneo ya kichwani na kusababisha umauti huku Haris Barnabas, mwanafunzi wa darasa la kwanza  akijeruhiwa.

Amesema baada ya kutekeleza mauaji hayo walifunga mlango wa nyumba hiyo kwa nje na kisha kutoweka na funguo.

Kamanda Kuzaga amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi.

“Ilikuwa sio rahisi kwa mtu kigundua kama kuna mauaji yametokea, baada ya kufanya tukio hilo mlango wa nyumba yao ulifungwa kwa nje  tushukuru uhusiano mzuri na jamii ulisaidia kubaini tukio hilo, ”amewema Kuzaga.

Akizungumza na Mwananchi, Mery Joel amesema baada ya kuona duka la mwalimu huyo halijafunguliwa na simu yake ya kiganjani inaita bila kupokewa walilazimika kufika nyumbani kwake.

“Baada ya kufika  ndio tukagundua ameuawa pamoja na mtoto wa kike aliyekuwa akiishi naye ,”amesema.