‘Nyongeza mshahara kila mwaka ni muhimu’

Muktasari:
- Wakati nyongeza ya mshahara ya kila mwaka ikirejea kwa watumishi wa umma, sekta binafsi nayo imeshauriwa kuangalia maslahi ya watumishi wake kwani gharama za maisha zinapanda kila siku.
Dar es Salaam. Kaimu mhariri wa uchumi gazeti la Mwananchi, Ephrahim Bahemu amesema nyongeza ya mshahara ni kila mwaka ni kitu cha muhimu kwani gharama za maisha zinapanda kila siku.
Amesema kilichofanywa na Serikali pia kinapaswa kuangaliwa na sekta binafsi kwani watu wote wanaishi katika mazingira ya aina moja ambayo gharama zake zinaongezeka kila kukicha.
Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza kurejesha nyongeza ya mishahara ya kila mwaka kwa wafanyakazi wa umma katika maadhimisho ya Mei Mosi ikiwa ni miaka saba tangu kuondolewa kwa mfumo huo na Rais wa Awamu ya tano, Hayati John Pombe Magufuli mwaka 2016
Ameyasema hayo leo Jumatano Mei 3 katika Mjadala wa Mwananchi Twitter Space ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communication Limited ukijadili mada isemayo, ‘Nini maoni yako juu ya hotuba ya Rais Kuhusu maslahi ya wafanyakazi nchini.’
Bahemu amesema kurejeshea kwa nyongeza ya mshahara kila mwaka ndiyo jambo lililowafurahisha wengi.
Hiyo ni kwa sababu nyongeza ya mshahara ya asilimia 23 kwa kima cha chini inawanufaisha zaidi wale wanaopata mshahara mdogo tofauti na wale wenye mshahara mkubwa.
"Nyongeza ya mshahara kila mwaka ni jambo la muhimu kwa kuwa mfumuko wa bei umekuwa ukiongezeka kila mwaka. Kwa kuwa kuna mfumuko wa bei, nyongeza ya mshahara haiepukiki. Kwa sasa mfumuko wa bei umefikia 4.9," amesema Bahemu.
Bahemu amesema kunapokuwa na maboresho ya maslahi hata ari ya kufanya kazi inaongezeka, huku akiongeza kuwa kwa bahati mbaya suala la nyongeza ya mshahara linaonekana kugusa zaidi sekta ya umma ingawa kwa uhalisia ilipaswa kugusa hata sekta binafsi.
"Kwa kuwa gharama za maisha ni zile zile. Suala la kuboresha maslahi kwa wafanyakazi ni jambo ambalo halitakiwi kusubiri utashi wa kiongozi bali kuangalia uhalisia wa hali ya maisha.
Katika hotuba yake katika maadhimisho ya sikukuu ya Mei Mosi iliyofanyika kitaofa mkoani Morogoro, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa ufafanuzi wa nyongeza hiyo.
“Mishahara kwa mwaka huu mbali na upandishaji wa posho nilizosema tumejiandaa pia kupandisha madaraja, vyeo vitaendelea kupandishwa, kutenganisha makundi na madaraja mserereko wale ambao hawakupata mwaka jana watapata mwaka huu.
“Niseme pia kuna nyongeza za mishahara za mwaka ambazo kwa muda mrefu zilikuwa zimesitishwa, nikaona kwa mwaka huu tuzirudishe kwa wafanyakazi wote kuna nyongeza za mishahara tunaanda na tutaendelea kama tulivyokuwa tunafanya zamani,” amesisitiza.
Rais Samia amesisitiza kuwa mwaka jana Serikali ilipandisha mishahara kwa asilimia 23.3 ambayo si kila mtu alifaidika ila lengo ilikuwa kuwainua wa kima cha chini na wengine wachache lakini kuna kindi kubwa halikuguswa.