Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi amjeruhi mwanaye kwa kushindwa hisabati

Muktasari:

  • Taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Blasius Chatanda imesema Januari 15, Nkalango alimchapa fimbo mwanaye huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Gappa baada ya kukagua madaftari yake na kugundua makosa.

Bariadi. Jeshi la Polisi mkoani Simiyu linamshikilia askari mwenye namba H.4178 PC Abati Nkalango (27) aliyemshambulia kwa fimbo na kumsababishia majeraha mtoto wake Benedicto Abati (7).

Taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Blasius Chatanda imesema Januari 15, Nkalango alimchapa fimbo mwanaye huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Gappa baada ya kukagua madaftari yake na kugundua makosa.

“Siku hiyo alikagua madaftari ya mtoto na kugundua alikuwa amekosea baadhi ya maswali ya hisabati aliyokuwa amepewa shuleni hivyo alimchapa viboko vingi ambavyo hakumbuki idadi na kumsababisha kutokwa damu mgongoni,” alisema Chatanda.

Baada ya kufanya ukatili huo, mtuhumiwa alimpaka dawa na kumtibu wakiwa nyumbani.

“Hadi sasa mtuhumiwa amekamatwa na anashikiliwa na Jeshi la Polisi wakati taratibu nyingine za kisheria na kinidhamu zinakamilishwa dhidi yake,” alisema.

Taarifa iliyotolewa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Somanda ya mjini Bariadi, Dk Emmanuel Constantine ilisema mtoto huyo alipokelewa akiwa na majeraha makubwa mgongoni, kichwani na masikioni, mapya na ya zamani.

“Kwa sasa anaendelea na matibabu, amelazwa katika wodi ya watoto na hali yake inazidi kuimarika,” alisema Dk Costantine.

Taarifa ya kujeruhiwa kwa mtoto huyo iliibuliwa Januari 19 na mwalimu wake wa darasa aliyesema mahudhurio yake yalikuwa hafifu kwani hakwenda shuleni kwa siku tatu.

“Aliletwa na mama yake mlezi akiwa amechelewa saa za masomo, mwalimu aliona haandiki, hana raha hivyo mwalimu wa darasa akamuita mwalimu mlezi (patron) na wakaingia naye chumba maalumu kumkagua, wakakuta ana majeraha yasiyo ya kawaida,” alisema mwalimu huyo wa darasa.

Baada ya kuiona hali hiyo, walimwita mwalimu mkuu wakati mama mlezi akiwa bado yupo ambapo walimbana na kuwaeleza ukweli kuwa kapigwa na baba yake mzazi kwa kutumia waya.

Mwalimu mkuu alisema walimchukua mtoto huyo, mama mlezi na mwalimu mlezi kuelekea Kituo cha Polisi Bariadi lakini wakiwa njiani alipigiwa simu na baba wa mtoto ambaye alimtaka mwalimu mkuu wayamalize na asimpeleke mtoto polisi.

Mama mlezi huyo, Vumilia Mahega alisema mtoto huyo alipigwa na baba yake Jumapili ya Januari 15 kwa kosa la kutokuandika shuleni na walimpeleka shuleni Alhamisi.

“Mimi ni mke ila huyo mtoto si wa kwangu. Sikufurahishwa na kitendo hicho,” alisema Vumilia.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Janeth Jackson alisema wanasimamia kuhakikisha mtoto huyo anatibiwa mpaka kupona majeraha yake na kumtafuta mtu atakayemlea kwa usalama.