Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi wachunguza malalamiko dhidi ya askari wake

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) David Misime

Muktasari:

  •  Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) David Misime, amesema watashirikisha wataalamu wengine wa haki jinai kuchunguza malalamiko hayo

Moshi. Jeshi la Polisi limesema linafanyia kazi tuhuma zilizotolewa na watu wawili kupitia mitandao ya kijamii wakiwalalamikia askari wa jeshi hilo.

Mmoja wa walalamikaji amejitambulisha kuwa mtumishi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) anayedai jopo la askari lilivamia nyumbani kwake usiku wa manane likimtuhumu kuvunja kwa wizi wa simu aina ya Infinix na baadaye kumbambikia kesi ya kuvunja kituo cha polisi ofisi ya vidhibiti.

Msemaji wa jeshi hilo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) David Misime, amesema wanafanyia kazi madai hayo yaliyotolewa kupitia video zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii.

Taarifa ya maandishi na ya video iliyotolewa leo, Desemba 21, 2023 kupitia mtandao wa Jeshi la Polisi Tanzania, Misime amesema: "Katika mitandao miwili tofauti ya kijamii, zimeonekana taarifa za wananchi wakilalamika kuwa wamefanyiwa vitendo vilivyo kinyume cha sheria na haki za binadamu, na baadhi ya askari polisi. Wananchi hao ni pamoja na Getrude Masanja anayelalamika kufanyiwa hivyo huko mkoani Kilimanjaro."

 “Jeshi la Polisi tumeziona video za malalamiko hayo na tumeanza kuyafanyia uchunguzi kwa uzito mkubwa ili kuhakikisha haki inatendeka."

Misime amesema watashirikisha wataalamu wengine wa haki jinai kuchunguza malalamiko hayo, hivyo mwenye ushahidi kulingana na malalamiko yaliyowasilishwa na walalamikaji asisite kujitokeza ili uchunguzi huo ukamilike mapema, hatua nyingine za kisheria zifuate.

Desemba 20, 2023 video ilisambaa mitandaoni ikimuonyesha Getrude Masanja akililalamika kuwa polisi mkoani Kilimanjaro wamembambikia kesi ya kuvunja kituo kikuu cha polisi Moshi.

Alipozungumza na Mwananchi Digital leo Desemba 21,2023 Getrude amesema yeye ni mfanyakazi wa TRC, kitengo cha huduma kwa wateja katika Stesheni ya Moshi.

Amedai mara kadhaa amekuwa akisumbuliwa na askari hao na wakati mwingine kumkosesha amani yeye na familia yake kutokana na matukio ambayo yamekuwa yakitokea.

Awali, kupitia mtandao wa X, Getrude analalamika kuwa jopo la askari likiongozwa na mkuu wa upelelezi wa kituo hicho walimvamia usiku nyumbani kwake wakimtuhumu kwa wizi wa simu aina ya Infinix.

Amewataja askari sita kwa majina akidai waliingia nyumbani kwake kwa fujo na kufanya upekuzi bila kuwa na kibali hali iliyozua mvutano.

Anadai alimtaka kiongozi wa askari hao kutoa taarifa kwa viongozi wa eneo analoishi kabla ya kufanya upekuzi lakini alikataa.

Getrude anadai waliendelea na upekuzi kwenye nyumba yake hadi chumba alimokuwa amelala mtoto mwenye wa miaka miwili na nusu, ambaye walimtoa kitandani ili kuinua godoro.

Baada ya upekuzi wa saa moja anadai hakuna kilichopatikana.

"Mwisho wa siku wakanambia lengo na dhumuni halikuwa kuja kukukagua simu, bali walikuja kunikamata na kwamba niko chini ya ulinzi, nikituhumiwa kwa kesi ya kuvunja kituo cha polisi ofisi ya vidhibiti,” anadai.