PSSSF, NSSF zalipa mabilioni kwa wastaafu, wategemezi

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza bungeni leo

Muktasari:

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema NSSF umekusanya Sh1,278.15 bilioni kutoka kwa waajiri na wanachama wake.

Dodoma. Mifuko ya hifadhi ya jamii imelipa mabilioni ya fedha kwa wastaafu, wategemezi na wanufaika wengine katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Februari, 2024.

Mbali na hilo, mifuko hiyo ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), imelipa pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu.

Vilevile, mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umelipa mafao ya fidia na pensheni jumla ya Sh12.1 bilioni kwa wanufaika wa mfuko.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Aprili 3, 2024 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotoa taarifa bungeni ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2024/2025.

Majaliwa amesema PSSSF umelipa mafao kwa wastaafu, wategemezi na wanufaika wengine wapatao 29,806 yenye thamani ya Sh927.17 bilioni.

Mifuko hiyo pia imelipa pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu 168,072 kwa wastani wa Sh70.08 bilioni kila mwezi.

“Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umelipa mafao ya Sh577.7 bilioni kwa wastaafu, wategemezi na wanufaika wengine 89,795.” amesema

“Kati ya kiasi hicho, Sh79.8 bilioni zililipwa kama pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu 30,756 ikiwa ni wastani wa Sh9.98 bilioni kila mwezi,” amesema.

Kuhusu WCF, amesema umelipa mafao ya fidia na pensheni jumla ya Sh12.1 bilioni kwa wanufaika wake.

Majaliwa amesema katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Februari, 2024, PSSSF umekusanya Sh906.46 bilioni sawa na asilimia 53.91 ya lengo la mwaka la kukusanya Sh1,681.56 bilioni.

“Mfuko huo umesajili wanachama wapya 29,698 sawa na asilimia 97.55 ya lengo la mwaka la kusajili wanachama wapya 30,444. Usajili huu wa wanachama kwa kiwango hiki kikubwa umetokana na Serikali kuajiri watumishi wengi Agosti 2023,” amesema.

Waziri Mkuu amesema NSSF umekusanya Sh1,278.15 bilioni kutoka kwa waajiri na wanachama wake.

“Mfuko wa WCF umekusanya michango kutoka kwa waajiri jumla ya Sh62.73 bilioni sawa na asilimia 67.45 ya lengo la mwaka la kukusanya Sh93.64 bilioni,” amesema.

Amesema Serikali kupitia NSSF inaendelea na maboresho ya mpango wa hifadhi ya jamii kwa wananchi waliojiajiri na walio katika sekta isiyo rasmi wanaweza kujiunga na kuchangia kwa hiari kwenye mfuko, ili kuwawezesha kupata huduma za hifadhi ya jamii kama wanavyonufaika wanachama walioajiriwa.

“Hadi kufikia Februari 2024 jumla ya wanachama 356,741 wameandikishwa kwenye skimu ya uchangaji wa hiari ya sekta isiyo rasmi,” amesema.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan alielekeza kurejesha michango ya watumishi wote walioondolewa kazini kwa kughushi vyeti.

“Utekelezaji wa maelekezo hayo ulianza Novemba, 2022, hadi sasa jumla ya watumishi 14,940 wamerejeshewa michango yao yenye thamani ya Sh45.5 bilioni kupitia mifuko ya PSSSF na NSSF,” amesema.

Mwaka wa fedha wa 2022/2023

Akiwasilisha bungeni taarifa ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Majaliwa amesema mwaka wa fedha wa 2022/2023, PSSSF ililipa mafao kwa wastaafu, wategemezi na wanufaika wengine wapatao 41,939 yenye thamani ya Sh1.074 trilioni na pensheni ya kila mwezi ya Sh507.28 bilioni sawa na wastani wa Sh63.41 bilioni kila mwezi kwa wastaafu 158,351.

Amesema NSSF imelipa mafao ya Sh438.32 bilioni kwa wastaafu, wategemezi na wanufaika wengine wapatao 66,628. Kati ya kiasi hicho, Sh72.3 bilioni zililipwa kama pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu 27,570 ikiwa ni wastani wa Sh9.04 bilioni kwa kila mwezi.