Serikali yawalipa Sh4 trilioni wastaafu

Muktasari:
Serikalil pia imelipa Sh500 bilioni katika deni la Sh731.4 bilioni la mikopo ya miradi ambayo mifuko iliyounganishwa iliikopesha ili kutekeleza miradi mbalimbali kama vile Jengo la Bunge, Chuo Cha Serikali za Mitaa cha Hombolo, Nelson Mandela Institute of Science and Technology na Chuo kikuu cha Dodoma.
Mwanza. Serikali imelipa deni la Sh4.6 trilioni la michango ya wanachama wa uliokuwa Mfuko wa Penseni wa Watumishi wa Serikali (PSPF), deni lililokuwa likidaiwa zaidi ya miaka 20.
Akimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Hosea Kashimba leo Jumatano Septemba 13, 2023 wakati wa semina ya maandalizi ya kustaafu kwa wastaafu watarajiwa wa mfuko huo jijini Mwanza, Mkurugenzi wa sheria PSSSF, Vupe Ligate amesema uamuzi wa kulipa deni hilo umewezesha mfuko kulipwa Sh2.17 trilioni kupitia hatifungani maalum.
Amesema Serikalil pia imelipa Sh500 bilioni katika deni la Sh731.4 bilioni la mikopo ya miradi ambayo mifuko iliyounganishwa iliikopesha ili kutekeleza miradi mbalimbali kama vile Jengo la Bunge, Chuo Cha Serikali za Mitaa cha Hombolo, Nelson Mandela Institute of Science and Technology na Chuo kikuu cha Dodoma.
“Jambo la kulipa madeni ya Serikali katika mfuko, hususani lile la michango ya kabla ya mwaka 1999 lilichukua muda mrefu, takribani miaka 20. Hata hivyo, kupitia uongozi wa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan jambo hili limewezekana,”amesema
Ligate amesema kulipwa kwa madeni ya mfuko huo unaotarajia kuwa na wastaafu 11,000 mwaka wa fedha 2023/24 kumeongeza uimara kifedha na kuendelea kuwekeza kwa tija.
Akizungumzia utekelezaji wa majukumu ya PSSSF, amesema kwa kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wake mfuko umelinda na kuongeza thamani yake kwa asilimia 27.76 kutoka Sh5.83 Julai, 2018 hadi Sh8.07 trilioni Juni, 2023 ongezeko likiwa sawa na asilimia 6.72 kwa kila mwaka.
“Vile vile mfuko umeendelea kufanya uwekezaji kwa kufuata miongozo kiasi kwamba hadi kufika Juni, 2023, thamani ya uwekezaji ilikuwa Sh7.92 trilioni ikilinganishwa na Sh6.40 trilioni wakati ulipoanza, sawa na ongezeko la asimilia 23.5 ambayo ni wastani wa ongezeko la asimilia 4 kwa mwaka,”amesema
Akizungumzia Semina kwa wastaafu watarajiwa amesema wataelimishwa juu ya mafao yatolewayo na taratibu za kuomba mafao hayo, maeneo salama ya kuwekeza hasa kwa wasataafu watarajiwa, namna ya kuishi kwa raha baada ya kustaafu na jinsi ya kujikinga dhidi ya uhalifu na mashambulizi ya kimtandao.
“Hii si mara ya kwanza kwa semina hizi kufanyika kwani Juni na Julai, 2021 mfuko ulifanya semina kwa wastaafu watarajiwa 3,700 kwenye mikoa 11, ambapo wastaafu watarajiwa walielimishwa juu ya taratibu za kustaafu na umuhimu wa kujiandaa kustaafu”amesema
Amesema mpaka sasa wana wastaafu 739,000 akiwaahidi kuwa mfuko unaendelea kuimarika kifedha kutokana na usimamizi madhubuti wa bodi, utendaji wa menejimenti na wafanyakazi.
Akifungua semina hiyo Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Elikana Balandya amesema kutokana na ugumu wa maisha, kutapeliwa fedha na changamoto za uwekezaji baada ya kustaafu, baadhi ya watumishi wamekuwa na hofu ya kustaafu na kuomba waongezewe muda akidai mafunzo hayo yatawaonolea hofu hiyo.
“Tukianza kujiandaa katika uwekezaji itasaidia sana kuliko kusubiri hadi kustaafu ndo kuanza kutafuta fursa za uwekezaji,”amesema Balandya