Mfumo wa kidijitaji kutumika maombi mafao ya wastaafu
Muktasari:
- PSSSF kuwapunguzia mwendo wastaafu, sasa mafao kushughulikiwa kidijitali kupitia mfumo wa tehama utakaozinduliwa Septemba mwaka huu.
Dar es Salaam. Ni neema kwa wastaafu hivi ndivyo inavyoweza kuelezwa kufuatia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kutangaza ujio wa mfumo Tehama unaowawezesha kushughulikia masuala yote ya mafao kwa njia ya mtandao.
Mfumo huo wa kidijitali unatarajiwa kuzinduliwa Septemba mwaka huu, ukitarajiwa kurahisha uchakataji wa maombi ya mafao ili kuwaondolea mizunguko wastaafu.
Mkurugenzi Mkuu wa PSSF, Hosea Kashimba amesema kupitia mfumo huo mfanyakazi anayekaribia kustaafu ataweza kujaza taarifa zake akiwa ofisini na zikachakatwa kwenye mfumo kisha kukutana na fedha zake benki.
“Hakutakuwa na sababu ya mstaafu kuzunguka ofisini kufuatilia mafao, mtumishi atajaza maombi akiwa kwenye meza yake ofisini na taarifa atakuwa anazipata kwenye simu yake ya mkononi.
“Hii yote inafanyika katika kuhakikisha tunasogeza huduma kwa wastaafu na kuwaondolea adha ya kuzunguka huku na kule kufuatilia mafao yao, kupitia mfumo huu ndani ya muda mfupi baada ya kujaza taarifa zao zitachakatwa na watakutana na fedha zao benki,” amesema Kashimba.