Sakata mtoto aliyeteketea Kaliua lachukua sura mpya

Muktasari:

  • Yaelezwa kuwa kuna hoja tisa zenye utata zinazohitaji uchunguzi wa kina kubaini ukweli wa chanzo cha kifo cha mtoto yule

Mwanza. Timu za uchunguzi kutoka ofisi ya Waziri Mkuu na Kamati Kuu ya Ulinzi Taifa zimetua Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora kuchunguza madai ya mtoto Nyanzore Ng’wandu (4) kuteketea kwa moto wakati wa operesheni ya kuwaondoa waliovamia Hifadhi ya Jamii Isawima wilayani humo.

 Habari zilizolifikia Gazeti la Mwananchi na kuthibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Abel Busalama zinaeleza timu hizo mbili zimetua tangu juzi.

“Kwa leo hakuna mwendelezo wowote kuhusu tukio hilo zaidi ya timu maalumu ya Waziri Mkuu na mamlaka nyingine za Serikali kufika hapa kufuatilia suala hilo,” alisema Busalama alipozungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana.

Tukio la mtoto kudaiwa kufariki dunia kwa kuteketea kwa moto wakati askari kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (Tawa) na Jeshi la Polisi walipokuwa wanatekeleza operesheni ya kuziondoa kaya zaidi ya 30 zilizovamia eneo tengefu ndani ya Hifadhi ya Jamii Isawimo lilitokea Juni 16.

Mtoto aliyefariki dunia ni mjukuu wa Ng’ombeikungire Ng’wandu, mkazi wa Kijiji cha Kombe wilayani Kaliua.

Hifadhi ya Jamii ya Isawima yenye ukubwa wa kilomita za mraba 314.87 ni ushoroba ya hifadhi za Taifa za Ugara na Muyowosi na mapori ya akiba ya Kihosi na Ruganzo-Tongwe inayomilikiwa na vijiji 11 vya Wilaya ya Kaliua.

Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya hiyo, Naibu Waziri Maliasili na Utalii, Mary Masanja akiongozana na watendaji wengine wa mamlaka za uhifadhi na wanyamapori, walitarajiwa kutembelea eneo la tukio juzi na kuzungumza na wananchi.

Hoja za kuchunguza

“Kuna hoja tisa zenye utata zinazohitaji uchunguzi wa kina kubaini ukweli wa chanzo cha kifo cha mtoto yule; japo siwezi kuzitaja zote kuepuka kuharibu uchunguzi, lakini moja ni hisia kuwa kifo cha mtoto yule kimetengenezwa kwa nia ya kusitisha operesheni,” alisema mkuu wa wilaya.

“Wakati wanafamilia wanadai mtoto aliyeteketea kwa moto alianguka mlangoni katika harakati za kukimbilia nje kujiokoa; mwili wa mtoto huyo ulikutwa zaidi ya mita mbili kutoka mlangoni.”

Alisema hata mkono wa kushoto wa marehemu ulikutwa umeungua hadi kubaki mifupa huku sehemu ya nyumba ambako mwili huo ulipatikana haukuonyesha kuteketea kwa kiwango kikubwa.

RPC azungumzia uchunguzi

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Saphia Jongo alisema hadi kufikia jana, uchunguzi wa tukio hilo ulikuwa umefikia zaidi ya asilimia 70 kubaini kiini cha kifo cha mtoto Nyanzore.

“Baadhi ya hoja za msingi tunazokamilisha uchunguzi wake, moja ni kubaini mtoto anayedaiwa kusalia ndani ya nyumba akiwa amelala, wakati mali zote, yakiwamo magodoro na shuka zilitolewa ndani kabla ya nyumba kuteketezwa?” alisema Kamanda Jongo.

Huku akizungumza kwa tahadhari ya kutotaka kuingilia undani wa suala hilo kuepuka kuharibu uchunguzi, Kamanda Jongo alisema Jeshi la Polisi pia linachunguza muda ambao mtoto huyo anadaiwa kuteketea kwa moto kwa sababu baadhi wanadai tukio lilitokea usiku wakati operesheni ilifanyika kati ya saa 2:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri.