Simulizi ya mtoto wa mitaani aliyefanikiwa kuhitimu chuo kikuu

Agustino Mboya

Muktasari:

 Agustino ni mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro, aliamua kuingia mtaani akiwa na umri wa miaka saba

Moshi. Maisha ni siri nzito. Ndivyo unavyoweza kueleza kisa cha Agustino Mboya (28) aliyenyanyuka kutoka mtaani tangu akiwa na umri wa miaka saba hadi sasa anapohitimu shahada yake ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).

Agustino ni mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro, aliamua kuingia mtaani akiwa na umri wa miaka saba na alikuwa akizunguka kutafuta vyuma chakavu na kwenda kuviuza ili apate pesa za kujikimu kimaisha kutokana na ugumu wa maisha katika familia yake.

Anasema baba yake alikuwa mlevi kupindukia na alikuwa akirudi nyumbani usiku na kuanza kumpiga mama yake bila sababu huku akiwa hajali familia yake kwa kuwapatia mahitaji muhimu katika maisha yao.

Kutokana na vituko vya baba yake aliamua kuondoka nyumbani, akaacha shule na kwenda kuwa mtoto wa mtaani.

Kijana huyo ambaye sasa ni mhitimu wa shahada ya kwanza ya uchumi na fedha ya MoCU, anaeleza kuwa akiwa mtaani aliamua kujitafutia kipato kwa kutafuta vyuma chakavu na kwenda kuviuza, kwa siku aliweza kupata kati ya Sh1,500 na Sh2,000 baada ya kuuza vyuma hivyo.

Agustino anasimulia kwamba maisha ya familia yake ndiyo yalimsababishia kwa asilimia kubwa kuwa mtoto wa mtaani kutokana na ugumu wa maisha waliokuwa nao ambao uliosababishwa na ulevi.

Anasema kukosekana kwa ada na mahitaji muhimu kama chakula, kulimfanya aingie mtaani akiwa bado mdogo ili aondokane na tabu za familia kwa kuwa kelele za baba yake na ugomvi wa usiku ilikuwa ni kero kwake.

“Nilikwenda mtaani kutokana na maisha wazazi wangu waliyokuwa wakiishi, baba yangu alikuwa ni mlevi sana, kila akirudi nyumbani usiku alikuwa anampiga mama, siku moja baba alimpiga mama mpaka akapoteza fahamu bila sababu.

“Ilifika mahali mama akaondoka nyumbani kabisa, wakati huo mama alikuwa na watoto saba, na aliweza kuondoka na mimi pamoja na mdogo wangu, tukarudi nyumbani kwa bibi mzaa mama huko Kikafu, wilaya ya Hai. Ni kutokana na manyanyaso ya baba, walikuwa hawatupatii mahitaji yetu ya msingi kama chakula, mavazi na malazi,” anasema.

Agustino anasema maisha ya kijijini nayo yalimshinda, hivyo akalazimika kurudi walikokuwa wanaishi Mwanza na kwamba baba yake aliendelea kuwa mlevi na maisha yakawa magumu zaidi, ambapo alilazimika kurejea tena mtaani.

Baada ya kuingia mtaani, anasema alianza kufanya kazi ya kutafuta vyuma chakavu ili uaze apate fedha. Anasema haikuwa kazi rahisi kwake kwa kuwa kuna wakati alikuwa anapata na wakati mwingine anakosa kabisa.

“Kwa siku unaweza uzunguke usipate chochote na hata ukipata sio zaidi ya Sh2,000, wakati mwingine baada ya kupata hela, narudi zangu nyumbani tuweze kununua chochote ili tule, kwa hiyo nilikuwa nampa mama anatafuta chochote tunakula,” anasema.

Anasema wakati akiwa mtaani alikutana na kijana mmoja ambaye alikuwa akifanya kazi na Shirika la Amani Centre for Street Children linalosaidia watoto wa mtaani na wale wanaotoka katika mazingira magumu.

 Anasema alimbeba na kwenda naye kwenye shirika hilo ambalo lipo Moshi mjini ili asaidiwe.

“Wakati nipo mtaani nilikutana na mmoja wa wafanyakazi wa Amani Centre for Street Children, akanambia shirika lao linasaidia watu kama sisi, hivyo sikusita nilienda naye moja kwa moja kwenye hilo shirika,” anasimulia.

Anasema baada ya kufika kwenye shirika hilo alianza kupewa elimu ya Memkwa na alipofika darasa la nne, walinipeleka shule moja ya msingi Shirimatunda iliyopo Moshi alikomaliza darasa la saba na akafaulu vizuri.

“Nikachaguliwa kwenda kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Karanga baadaye shirika lilimhamisha na kumpeleka shule ya bweni ya Orkolili iliyopo Hai.”

Anasema baada ya kumaliza kidato cha nne na kupata daraja la pili, alipangiwa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Uyumbu, alisoma kwa kipindi cha miezi sita na kutokana na changamoto ya uhaba wa walimu, alimjulisha mlezi wake na alihamishwa na kupelekwa Shule ya sekondari Majengo.

Anasema alisoma hadi kufanikiwa kuhitimu kidato cha sita na baada ya matokeo ya kidato cha sita kutoka, alifaulu na kupata daraja la tatu.

“Baada ya kumaliza kidato cha sita, nilipata nafasi ya kwenda Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mkoa wa Kigoma, kambi ya Kanembwa, nilimaliza mafunzo yangu ya miezi mitatu, nikapata cheti, nikarudi nyumbani. Matokea yangu a kidato cha sita yalipotoka, nilifaulu ambapo nilibahatika kwenda Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU),” anasema.

Kijana huyo anaeleza kwamba baada ya kumaliza chuo mwaka 2021 alipambana kutafuta kazi lakini ilikuwa ni changamoto kuipata, aliomba kufanya kazi ya kujitolea Sido na hadi sasa anajitolea, anaishukuru Amani Centre kwa kumpatia mwangaza katika maisha yake na kumtoa mtaani.

Neno kwa wazazi

Agustino anasema katika mazingira ya kila siku, wazazi wamekuwa chanzo cha watoto kuchukua uamuzi mgumu ambao baadaye huharibu malengo yao na kugharimu maisha yao na mwisho wa siku kuishia kuwa watoto wa mtaani.

“Wazazi wanapaswa kujua kwamba kulea na kutunza watoto ni jukumu lao, kwa vyovyote vile wanapaswa kuwapatia watoto mahitaji yao ya msingi ya kila siku na wasikimbie majukumu yao kama wazazi, maana wao ndio waliowazaa,” anasema.

Akizungumza kazi wanazofanya, mkurugenzi wa programu wa Shirika la Amani Centre for Street Children, Daniel Temba anasema shirika hilo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001, limeweza kuwaokoa na kuwasaidia watoto 2,500 kutoka mtaani.

“Shirika la Amani Centre for Street Children, lilioanzishwa mwaka 2001, limekuwa likifanya kazi na watoto hawa wanaoishi na kufanya kazi mitaani kwa kuwaokoa, kuwapa matumaini na kubadilisha maisha yao kwa kuwawezesha kutimiza ndoto zao. Shirika hili limefanikiwa kusaidia watoto kutoka mitaani 2,500 kwa kuwaokoa na kuwaunganisha na familia au jamii zao ili waimarike na kujitegemea,” anasema.

Anasema sababu zinazochangia watoto wa mtaani ni pamoja na umasikini wa kaya, uzazi usiojali, ukatili wa kijinsia, ukatili dhidi ya watoto, ukatili wa majumbani, shuleni na kutowajibika kwa wazazi, migogoro ya kifamilia na vifo vya wazazi.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na changamoto ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani, tatizo hilo lilianza miaka ya 1990 kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo umaskini wa kaya, ukatili wa majumbani, shuleni, kutowajibika kwa wazazi.

Sababu nyingine ni migogoro ya kifamilia, biashara haramu ya binadamu kwa watoto, utandawazi, vifo vya wazazi, kutengana kwa wazazi, malezi ya mzazi mmoja, uzazi wa kambo, janga la Ukimwi pamoja na kutokuwepo kwa mpango au mkakati wa kitaifa wa kuwawezesha watoto na vijana waliokosa fursa za elimu ya sekondari baada ya kuhitimu elimu ya msingi.