TMDA kufanya tathmini matumizi ya P2

TMDA kufanya tathmini matumizi ya P2

Muktasari:

  • Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imeanza kufanya tathmini ya kina kuhusu matumizi yasiyo sahihi ya vidonge vya ‘Emergence Contraceptive Pills’ maarufu kama P2 ambavyo humezwa kama njia ya kuzuia ujauzito.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imeanza kufanya tathmini ya kina kuhusu matumizi yasiyo sahihi ya vidonge vya ‘Emergence Contraceptive Pills’ maarufu kama P2 ambavyo humezwa kama njia ya kuzuia ujauzito.

Uamuzi huo unakuja ikiwa ni miezi mitatu tangu gazeti la Mwananchi lilivyoanza kuripoti kuhusu matumizi yasiyo sahihi ya dawa hiyo ambavyo yamekuwa yakifanywa nchini, hasa kwa wanafunzi kuanzia miaka 14.

TMDA imesema imeanza kufanya tathmini ya kina ya kufahamu ni nini kinachosababisha dawa hiyo isitumike inavyopaswa na jamii.

Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo aliyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku nne ya wakaguzi 59 wapya wa dawa na vifaa tiba, yaliyoandaliwa na mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO).

“Tunafahamu kwamba kuna matumizi yasiyo sahihi ya P2 na tunafanya tathmini ya kina kufahamu nini kisababishi cha dawa hii isiuzwe inavyopaswa.

“P2 inapotolewa lazima kuwe na cheti cha daktari ndipo mtu aweze kuitumia kwa jinsi ambavyo imekusudiwa, kwa hiyo tunafanya tathmini tuone kama ni kweli, kuna taarifa kwamba inafanyika ndivyo sivyo na tukikamilisha tathmini tutakuja na majibu sahihi na tutafahamu maamuzi yapi tutachukua kudhibiti hali hiyo,” alisema Fimbo.

Msajili wa Baraza la Famasia Tanzania, Elizabeth Shekalaghe alisisitiza P2 ni dawa ya cheti ambayo inaruhusiwa kuuzwa katika famasi baada ya kutolewe cheti cha daktari na baraza limeanza pia kufanya ukaguzi wa bidhaa hizo nchini.

“Sisi wenyewe tuna mbinu na tutakuja na majibu katika hili, kwa kuwa mbali na hizi famasi kubwa ambazo zinapigiwa kelele tunabaini sasa hata maduka ya kawaida yameweka bidhaa hizo,” alisema Shekalaghe.

Shekalaghe alisema pamoja na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika udhibiti wa uuzwaji holela wa dawa, imebainika kwamba dawa hatarishi, ikiwemo P2 zimekuwa zikitumika kinyume na makusudio ya Serikali.

Mei 27 mwaka huu, Serikali ilisema itaanza kufanya ukaguzi kwa maduka ya dawa muhimu na yatakayobainika kuuza vidonge vya P2 na zile za kutoa mimba ‘misoprostol’ pasipo kuwa na cheti cha daktari, yatachukuliwa hatua.

Hata hivyo, licha ya tamko hilo, Mwananchi limethibitisha pasipo shaka kwamba vidonge hivyo vimeendelea kuuzwa katika maduka ya dawa bila tahadhari.

Katika uchunguzi wake, Mwananchi lilibaini kila duka lililofikiwa lilikuwa likiuza bidhaa hizo bila kudai cheti cha daktari.

Uchunguzi huo ulibaini aina saba ya vidonge vya P2 vinavyozalishwa na viwanda mbalimbali vikiwa vinauzwa kwa bei ya Sh5,000 na vingine Sh10,000.

Madhara

Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama kutoka Hospitali ya Aga Khan, Dk Jane Muzo alishauri wanawake kutotumia kabisa dawa hizo au kutumia kwa dharura iwapo daktari ameshauri na si vinginevyo.

“Ni dawa ambayo inabidi kama ukiitumia uchukue tahadhari ili ujizuie usitumie tena kwa sababu watumiaji wengi wanalalamika kwamba hedhi zao zimebadilika,” alisema Muzo.