Tozo laini za simu, miamala bado moto

Tozo laini za simu, miamala bado moto

Muktasari:

  • Wadau wa Bajeti wameeleza kuwa suala la kuanzishwa kwa tozo katika laini za simu na tozo ya miamala ni kutoza ushuru mara mbili kwa kile walichoeleza kuwa tayari Serikali inatoza kodi kitika maeneo hayo.

Dar es Salaam. Wadau wa Bajeti wameeleza kuwa suala la kuanzishwa kwa tozo katika laini za simu na tozo ya miamala ni kutoza ushuru mara mbili kwa kile walichoeleza kuwa tayari Serikali inatoza kodi kitika maeneo hayo.

Hayo yamebainishwa jana katika mdahalo wa wahariri wa vyombo vya habari kujadili mapendezo ya bajeti kuu ya mwaka 2021/2022, zikiwa zimebakia siku takribani 10 kabla ya kuanza kutumika kwa bajeti hiyo endapo itapitishwa na Bunge.

Katika bajeti mpya, Serikali inakusudia kutoza Sh10 hadi 200 kwa mwezi kwa kila anayeongeza muda wa maongezi (vocha) kulingana na matumizi ya mhusika lakini pia Sh10 hadi Sh10,000 itatozwa kwenye miamala ya fedha kulingana na kiwango cha thamani ya muamala.

Akizungumzia eneo hilo katika mdahalo huo ulioandaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), mtaalamu wa udhibiti wa fedha binafsi na mwanzilishi wa jukwaa la Let’s Talk Finance, Edmnd Munyagi, alisema tozo hiyo inaweza kuathiri ukuaji wa uchumi dijitali.

Alisema tayari Serikali inatoza kodi ya ongezeko la thamani na kodi ya bidhaa kupitia vocha na makato ya kufanya miamala, hivyo tozo hiyo inayopendekezwa itaongeza gharama za uendeshaji wa simu na kupunguza matumizi wakati Serikali ilipaswa kuwekeza kuvutia watu kutumia zaidi simu ili ikusanye zaidi.

Mtaalamu wa Uchumi, Lawrance Mlaki alisema bajeti hiyo iliyosomwa siku kadhaa zilizopita inamgusa kila mwananchi na katika kila ongezeko la kodi Serikali imeeleza madhumuni yake ambayo kwa mtazamo wake anaona kuwa yana manufaa kwa ustawi wa nchi.

Alisema matumizi ya Serikali ambayo imekusudia kuyafanya kupitia tozo na kodi mpya yatachochea ukuaji wa uchumi kwa kuboresha huduma za kijamii, ikiwemo afya, miundombinu ya barabara na elimu, lakini pia kuinua wakulima kupitia vivutio vya kikodi katika viwanda vinavyotumia malighafi za kilimo zinazozalishwa nchini.

“Miradi ya kuzalisha umeme ambayo itapunguza gharama za umeme kutachochea uzalishaji viwandani, ambavyo vitaongeza ajira za watu lakini pia ulipaji wa madeni ya Serikali ya ndani kutaongeza mzunguko wa fedha kwa shughuli za kiuchumi,” alisema Mlaki.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa TEF, Bakari Machumu ambaye alikuwa mwongozaji wa mdahalo huo, alisema lengo lao ni kuangalia namna ambavyo vyomba vya habari vinakuwa sehemu ya maendeleo ya Taifa kwa kuibua mijadala yenye tija kwa jamii.