Tozo mafuta pasua kichwa

Monday September 06 2021
Tozo pc
By Sharon Sauwa
By Ephrahim Bahemu

Dodoma/Dar. Wakati wingi wa tozo kwenye mafuta ukitajwa kuleta maumivu kwa wateja wa bidhaa hiyo nchini, Serikali imesema kamati iliyoundwa kuchunguza kupanda kwa bei ya petroli na dizeli, itawasilisha ripoti yake kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Septemba 16.

Kamati hiyo iliundwa baada ya mafuta bei kupanda mwezi huu. Hata hivyo, mabadiliko hayo ya bei yalidumu kwa siku moja kabla Serikali haijaisitisha bei hiyo mpya na kuelekeza iendelee kutumika bei iliyokuwepo awali yaani mwezi Agosti.

Akizungumza jana na wanahabari, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema kamati hiyo iliyoundwa Septemba 2 imepewa wiki mbili kukamilisha kazi hiyo na kutoa ripoti yake itakayofanyiwa kazi.

Alisema kamati hiyo itaangalia tozo zilizopo kwenye mafuta, kampuni zinazoagiza mafuta na utaratibu ambao umewekwa katika bandari za Dar es Salaam na Mtwara kujua sababu za kupanda kwa bei.

Soma hapa:Ukweli kupanda bei ya mafuta kujulikana Septemba 16

“Serikali inafanyia kazi kupanda kwa mafuta na kuangalia kama kuna maeneo ambayo yanaweza kushughulikiwa ili Watanzania waendelee kupata mafuta kwa bei ya chini.

Advertisement

“Kamati itatoa taarifa ya nini imebaini katika mchakato huo wa kuangalia bei ya mafuta,” alisema japo hakuweka bayana kuhusu athari zinazosababishwa na ongezeko la bei hizo katika sekta nyinginezo zikiwamo usafiri, usafirishaji, uzalishaji na hata kupanda kwa gharama za maisha.


Wadau waeleza machungu

Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa) Raheem Dosa alisema walistuka kuona bei ya mafuta ikipanda Septemba, wakati katika soko la dunia, bei imepungua hivyo wanaipongeza Serikali kwa kuingilia kati.

“Kwa sisi wasafirishaji, bei ya mafuta inatuumiza. Julai bei katika soko la dunia ilipungua kutoka Dola 75 (Sh172,500) kwa pipa hadi Dola 65 (Sh149,500); tunashangaa bei imepandaje tulitarajia itapungua au kubakia kama ilivyokuwa,” alisema Dosa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wauzaji wa Mafuta Tanzania (Taomac) Raphael Mgaya, aliupongeza uamuzi wa Serikali, lakini alishauri ili bei ya mafuta ibaki katika utulivu, zabuni za kuagiza mafuta hayo zifanywe na kampuni za kigeni ili kupata unafuu.

Soma hapa:Bei ya mafuta pasua kichwa

“Mwezi uliopita (ambao mafuta yake ndio yanatumika sasa) Serikali ilitoa tenda ya uagizaji wa mafuta kwa kampuni za ndani, lakini inakuwa gharama kwa kuwa kampuni hizo zilitozwa kodi ya mapato ya kampuni na tozo mbalimbali jambo ambalo liliongeza bei,” alisema Mgaya.

Alisema Serikali inapaswa kutengeneza utaratibu unaoratibu ustahimilivu wa bei ya mafuta kama wanavyofanya Zanzibar na Kenya, ambapo tozo huwekwa kipindi bei inapopungua sokoni na kiasi hicho kuja kutumika baadaye kupunguza bei inapoongezeka.


Mchanganuo wa tozo

Taarifa ya mabadiliko ya bei iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za Nishati na Maji (Ewura) Juni na Julai, haikuonyesha mchanganuo wa bei ya mafuta kwa lita moja, lakini kwa mujibu wa taarifa yao ya Julai Mosi baada ya kuanzishwa kwa tozo mpya ya mafuta ilionyesha kuwa jumla ya tozo na kodi za Serikali ni takribani asilimia 50 ya gharama yote ya lita moja ya mafuta.

Kutokana na mchanganuo huo wa Julai, gazeti hili limefanya uchambuzi wa gharama halisi ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa katika soko la dunia, baada ya gharama za usafiri, bima na forodha, kabla ya tozo za Serikali na gharama halisi baada ya makato yote.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ewura bei ya mafuta sokoni kwa lita ni Sh1,087.27, dizeli Sh1,050.47 na mafuta ya taa ilikuwa Sh945.32. Gharama za usafiri, forodha na bima (CIF) mpaka Bandari ya Dar es Salaam kwa petroli ni Sh75.02, dizeli Sh47.12 na mafuta ya taa Sh116.59.

Kwa hesabu hiyo maana yake kabla ya kodi na tozo mbalimbali gharama ya petroli ikiwa Dar es Salaam ilikuwa Sh1, 162.29, dizeli Sh1,097.59 na mafuta ya taa Sh1,061.91, lakini gharama za ziada katika mafuta haziishii hapo tu na huenda ni miongoni mwa bidhaa zenye tozo na kodi nyingi.

Kwa taarifa ya sasa ya Ewura, bei ya mafuta pamoja na bima (CIF) kabla ya kodi na tozo nyingine za Serikali, mafuta yanayopita katika bandari ya Mtwara gharama yake ilikuwa Sh1,179.91 kwa petroli, dizeli Sh1,126.30 huku bandari ya Tanga petroli ikiwa ni Sh1,219.67 na dizeli Sh1,143.29.

Kwa mujibu wa mchanganuo huo, kama Serikali ingekuwa haitozi kodi na tozo zingine mbalimbali kupitia taasisi zake, pengine gharama za mafuta zingekuwa na ahueni kwa wananchi.

Kwa kuwa Serikali inahitaji tozo na kodi mbalimbali kwa ajili ya kuhudumia wananchi, katika kila lita moja ya petroli Serikali huongeza Sh892, dizeli Sh768.00 na mafuta ya taa Sh715.00.

Kiwango hicho ni tofauti na tozo nyingine ambazo hutozwa na mamlaka za Serikali pamoja na gharama za usafiri.

Mbali na makato ya kodi, baadhi ya tozo ni pamoja na gharama za ghala, maendeleo ya reli, gharama za kushughulikia masuala mpakani, vipimo vya uzani, TBS, Tasac, Ewura, gharama za kuchelewa kwa meli, gharama ya uvukizi kwa, upotevu wa mafuta baharini na nyinginezo kadhaa ambazo zinatajwa kuongeza mzigo wa gharama na kusababisha bei kubwa juu na kuleta maumivu kwa watumiaji.

Advertisement