Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

 TRA yaanzisha kampeni wananchi kudai risiti

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, James Kaji

Muktasari:

  • Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga imezindua kampeni ya 'Tuwajibike' yenye lengo la kuhamasisha  wafanyabiashara na wananchi kuwa na utamaduni wa kutoa na kudai risiti za kielektroniki.

Tanga. Mkuu wa Wilaya ya Tanga, James Kaji amewaonya wakazi wa Tanga dhidi ya kupuuza kudai risiti za kieletroniki (EFD) wanaponunua bidhaa akisema, tabia hiyo ni sawa na kuhujumu jitihada za serikali za kukusanya kodi.

Onyo hilo amelitoa wakati  akizindua kampeni maalum ya kuelimisha wafanyabiashara juu ya umuhimu wa kutoa risiti za EFD kwa upande mwingine, umma kwa ujumla juu ya umuhimu wa kudai risiti za EFD kutoka kwa wafanyabiashara.

Kaji pia alitoa wito kwa wafanyabiashara wakiwemo wamiliki wa maduka wanaouza bidhaa zao katika masoko ya wazi na bucha kutumia mashine za EFD ili kuhakikisha serikali inakusanya fedha za kutosha kuhudumia miradi ya maendeleo ya umma.

Mkuu huyo wa wilaya aliwataka maofisa wa TRA kuwa wakweli na kuacha kuwa vyanzo vya ukwepaji kodi.

"Hatupaswi kusimama hapa na kuhamasisha wafanyabiashara na umma kwa ujumla juu ya kulipa kodi wakati huohuo kuwa chanzo cha ukwepaji wa kodi, wananchi hawatatuelewa,” ameonya.

Aliwataka maofisa wa TRA kuepuka kujenga hofu kwa wafanyabiashara jambo linalojenga mazingira ya rushwa. "Lazima tulenge kuhakikisha kuwa watu wanalipa kodi kwa hiari na siyo kwa nguvu," amesema.

Akizungumza kujibu ombi lililotolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya

Wafanyabiashara Tanga (JWT), Ismail Masoud ambaye amependekeza eneo la kati la Jiji la Tanga kati ya Mtaa namba 12 na 15 liruhusiwe kufanya kazi kwa saa 24, Kaji alisema ombi hilo linatekelezeka na alitoa wito kwa wafanyabiashara kuwa waaminifu kulipa kodi ili kuhakikisha kwamba ombi linatimizwa na serikali.

Kiongozi huyo wa JWT alikuwa ameomba kuruhusu eneo la kati la Jiji la Tanga kufanya kazi kwa saa 24 kitu ambacho alisema kitaongeza wigo wa mauzo ambayo yataongeza makusanyo ya kodi.

"Serikali inahitaji fedha kupitia kodi, kodi ni kama damu kwa wanadamu.

Bila damu mwanadamu hukoma kuwepo. Ni sawa na serikali. Bila kodi Serikali haiwezi kuwepo,” amesema.

Awali, Meneja wa TRA Tanga, Thomas Masese alisema ukaguzi wa biashara ulionyesha changamoto kadhaa za matumizi ya mashine za EFD ikiwa ni pamoja na kutoa risiti zisizoonyesha bei halisi zinazotozwa kwa wateja.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni kutoa taarifa zisizo sahihi za mauzo, kuuza risiti za EFD kwa watu wasio na mashine hizo, kusajili mashine za EFD kwa majina ya wafanyabiashara wengine.

Alisema kampeni hiyo inalenga kuwaelimisha wafanyabiashara na umma kwa ujumla umuhimu wa kulipa kodi na jukumu muhimu la stakabadhi za EFD katika ukusanyaji wa kodi.