‘Uhusiano na mawasiliano kada muhimu za maendeleo’

Maofisa uhusiano wakiwa kwenye utoaji tuzo za umahiri zilizotolewa na Chama cha Maofisa Uhusiano wa Umma Tanzania (PRST)

Muktasari:

Rais wa PRST, Asah Mwambene amesema tayari mchakato kwa ajili ya kuanzisha, sheria ya kusimamia taaluma ya maofisa habari serikalini umeanza

Dar es Salaam. Kada ya maofisa uhusiano na mawasiliano, imetajwa kuwa muhimu kutokana na mchango wake katika ukuzaji wa uchumi.

Hayo yameelezwa jana Aprili 5, 2024 na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca  Mahundi wakati wa utoaji tuzo za umahiri zilizotolewa na Chama cha Maofisa Uhusiano wa Umma Tanzania (PRST) kwa mwaka 2023.

Amesema sekta hiyo imekuwa na mchango mkubwa, endapo tuzo hizo zitaendelea kutolewa kila mwaka wale wanaofanya kazi kwa mazoea wataongeza juhudi na kujituma kwa manufaa ya Taifa.

Mahundi amesisitiza kuwa tuzo hizo zikiendelea kutolewa kwa kufuata misingi ya haki na weledi zitaondoa malalamiko baina ya washiriki.

 “Yapo mambo ambayo chama kimewasilisha wizarani ikiwamo kuanzisha chombo cha ithibati, maelekezo yameshatolewa tutafanya jitihada kipatikane,” amesema Mahundi.

Kuhusu mkutano wa PRST wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha Septemba mwaka huu, Mahundi amesema licha ya kuwa makao makuu, utaongeza tija kwa Serikali ikiwamo kuongeza fedha za kigeni.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amewataka maofisa uhusiano na mawasiliano kuwa wabunifu na kutumia teknolojia itakayoongeza ufanisi katika majukumu yao.

Amesema sio rahisi kudhibiti teknolojia mpya kwa kuwa inafungua uwanja mpana uliozalisha watu wengi.

 “Sio rahisi kudhibiti teknolojia kutokana na watu wengi kuzaliwa nayo, huko nyuma ilikuwa ni lazima kutafuta waandishi wa habari lakini hivi sasa watu wanatumia vyombo ambavyo hatujavizoea,” amesema Matinyi.

Rais wa PRST, Asah Mwambene amesema tayari mchakato kwa ajili ya kuanzisha, sheria ya kusimamia taaluma ya maofisa habari serikalini umeanza.

Amesema sheria hiyo itafanya taaluma hiyo kuwa bora zaidi kwa taasisi za umma na binafsi.

 “Tayari mchakato umeanza baada ya kuwasilisha rasimu wizarani kwa ajili ya kuanzisha chombo cha udhibiti, kitakachofanya taaluma hii kuwa bora zaidi,” amesema Mwambene.

Rais huyo amesema katika makubaliano yao na PRST Afrika Mashariki, wamekubaliana kufanyika kwa mkutano mkuu Septemba mwaka huu  Arusha.

“Makubaliano mengine ni mawaziri wa sekta za habari katika nchi za Afrika mashariki kuwa walezi wa vyama hivi katika nchi zao, bado baadhi ya nchi mchakato huo hujakamilika,” amesema Mwambene.

Katika tuzo hizo, taasisi mbalimbali ziliibuka washindi ikiwamo Benki ya CRDB, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Shirika la Bima la Taifa (NIC), Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Shirika la Hifadhi Tanzania (Tanapa).