Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

’Usipompa pesa mkeo akapendeza ni ukatili wa kiuchumi’

Muktasari:

  • Hiyo ni kauli ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Sanya Juu wilayani Siha, Janeth Mvungi, aliyoitoa  katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na kueleza kuwa upo ukatili wa kiuchumi kwa mwanamke ambao hauzungumzwi sana.

Moshi. Hivi unajua usipompa pesa mkeo akavaa vizuri na akapendeza ni ukatili wa kiuchumi? hii ndio kauli iliyotolewa na Hakimu Mfawidhi mahakama ya Mwanzo Sanya Juu wilayani Siha, Janeth Mvungi, alipozungumzia siku 16 za kupinga ukatili.

Washiriki wa maadhimisho ya siku 16 ya kupinga ukatili wa kijinsia wakifanya igizo katika maadhimisho hayo yaliyofanyika katika mji wa Sanyajuu wilayani Siha na kuhudhuriwa pia na wafugaji wa Jamii ya Kimasai. Picha na Mpiga Picha Wetu

Akizungumza katika maadhimisho hayo leo Desemba 11, 2023 huko Sanya Juu, , Mvungi amesema kuna ukatili wa kijinsia ambao unasahaulika nao ni ukatili wa kiuchumi.

“Kuna ukatili ambao huwa unasahaulika sana nao ni ukatili wa kiuchumi na watu wanaongelea tu kipengele cha mwanamke kupewa nafasi ya kumiliki mali. Naomba niseme hata mke wako usipompa pesa unamkatili kiuchumi,”amesema.

“Sheria ya ndoa inasema mwanamume ana wajibu wa kumtunza mke wake na familia. Japo mwanamke naye anakuwa na huo wajibu kama amemzidi mwanamume kipato lakini mara nyingi familia zetu mwenye kipato ni baba,” amesema.

“Kwa mila na tamaduni zetu mwanamume ndiye anayesimamia familia. Mama Yeyooo (kinamama wa Kimasai) mnapewaga eeh?. (sauti zikasika hapanaaaa). Wanasema hamtowi. Jamani tubadilike,”alisema Hakimu huyo na kuongeza:

“Kina baba kutowapa kina mama hela na matunzo ni ukatili wa kiuchumi naomba tubadilike mhakikishe mama anaoga vizuri, anakula vizuri anapaka mafuta mazuri anapendeza kwa pesa ambayo umeitoa wewe mwanamume,” amesema.

“Sio atumie tu pesa ambayo amehangaika nayo juani. Kuna matukio wengine kinamama wakitoka sokoni mnawanyang’anya hela. Jamani kweli hii ni haki? Najua sio wote lakini wapo.Unamnyang’anya pesa unaenda kunywa pombe,”ameeleza.

Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na taasisi ya kutetea haki za wanawake na watoto Mkoa wa Kilimanjaro (Kwieco) kwa ufadhili wa taasisi ya FNF, Afisa Ustawi wa Jamii Siha, Peter Msaka, amewataka watu wazima kujitafakari.

“Sisi watu wazima tunapaswa kujitafakari. Kama tunaweza kuchangia asilimia 80 ya ya matukio ya ukatili iko haja ya kukaa chini, kutafakari na kuja na majibu,”amesema Ofisa huyo katika wilaya ya Siha.

“Kwa mfano, ndoa za utotoni. Tunapozungumza ndoa za utotoni asilimia kubwa sio za mtoto na mtoto bali mtoto na mtu mzima. Sasa nani tatizo hapo? Mtu mzima. Lakini unakuja suala la wazazi kuwalipia watoto chakula shuleni,”

“Kuna watoto wanakosa mahitaji muhimu, halafu wako watu wanaoweza kuwapatia ambao sio wazazi wao. Inawezekana mtoto yuko tayari kupatiwa mahitaji muhimu na mtu mwingine yeyote ndani yake kuna ukatili,”amesema.

Akisoma ripoti ya utekelezaji mradi wa Jamii Salama kwa maendeleo yetu, mwanasheria wa Kwieco anayeshughulikia haki za binadamu na Jinsia, Elizabeth Mushi amesema kwa kushirikiana na FNF, walitoa mafunzo kwa viongozi wa mila 42.

Mbali na mafunzo hayo, lakini walitoa mafunzo ya ujuzi katika ujasiriamali na uchumi  kwa wanawake 120 yaliyohusisha pia usimamizi wa fedha, uanzishaji vikundi vya kijamii na walipewa elimu ya sheria ya kuwalinda.