‘Utafiti utumike kutatua changamoto za uhifadhi’
Muktasari:
- Serikali imewataka wadau wanaojihusisha na uhifadhi wa wanyamapori nchini, kutumia utafiti uliofanywa na watafiti wakiwamo kutoka Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Afrika (Mweka), kutatua changamoto za uhifadhi
Moshi. Serikali imewataka wadau wanaojihusisha na uhifadhi wa wanyamapori nchini, kutumia tafiti mbalimbali kutatua changamoto za uhifadhi.
Amesema mfano mzuri wa tafiti ni pamoja na uliofanywa na watafiti kutoka Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Afrika (Mweka).
Hayo yamesemwa jana Novemba 20, 2023 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula alipokuwa akifungua kongamano la siku tatu la kimataifa la miaka 60 ya uhifadhi wa wanyamapori barani Afrika, linalofanyika Mweka.
Amesema Serikali inajitahidi kadri inavyowezekana kuongeza fedha kwenye maeneo ya utafiti ili kuwawezesha watafiti kufanya kazi kwa weledi zitakazotoa jawabu kwenye changamoto za uhifadhi.
"Upo umuhimu wa kutumia tafiti ukiwamo uliofanywa hapa Mweka ili kuleta manufaa kwa nchi zetu.
“Pia tuwashauri watu waliopo katika sekta hizi kutumia tafiti inawezekana kuboresha sekta hii ya maliasili na utalii," amesema Kitandula.
Amesema "Leo tunaposema sekta ya maliasili na utalii inachangia zaidi ya asilimia 20 kwenye pato la Taifa ni kwa sababu imefanyika kazi kubwa ya kuhifadhi maliasili tulizonazo, hivyo ni lazima kila siku tukumbushane kuzilinda kwa wivu mkubwa kwa sababu uhai wetu unategemea uwepo wa maliasili hizi.
Naye Mkuu wa chuo hicho, Profesa Jafary Kideghesho amesema tangu kianzishwe mwaka 1963 kimefanya tafiti nyingi katika kutatua changamoto za uhifadhi na kimezalisha wahitimu zaidi ya 11,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani.
"Kwa miaka hii 60 tangu kuanzishwa kwa chuo hiki, kwenye masuala ya tafiti tumefanya mambo mengi ya ubunifu, ugunduzi na katika siku za hivi karibuni kupitia watafiti wetu tumegundua mimea dawa ambayo inasaidia kutibu mimea na wanyama.
“Aina mpya ya nyuki mchavushaji ambaye amegundulika mlima Meru, ugunduzi wa paka wa dhahabu ambaye hajawahi kuonekana Afrika ambaye mtafiti wetu amemgundua katika msitu wa Minziro kule Kagera," amesema.
Pamoja na mambo mengine, Profesa Kideghesho amesema kongamano hilo limelenga kutathmini nini kilichofanyika kwa miaka 60 tangu kuanzishwa kwa chuo hicho, na kuweka mpango mkakati kwa ajili ya uhifadhi siku zijazo.
Kwa upande wa Naibu Mkuu wa chuo hicho, anayeshughulikia taaluma, utafiti na ushauri, Profesa Alex Kisingo amesema wamefanikiwa kufanya tafiti mbalimbali katika masuala ya usimamizi wa wanyamapori na uhifadhi.
Akizungumza kwenye kongamano hilo, Mkurugenzi wa utafiti na mafunzo nchini, Dk Edward Kohi amesema Serikali kwa kutambua umuhimu wa utafiti imeongeza bajeti kuhakikisha watafiti wanafanya kazi zao ili kuleta mabadiliko chanya katika taasisi za vyuo na za utafiti.