Utata wizi taa za barabarani Mara

Nguzo taa za barabarani wilayani Bunda zikiwa zimenyofolewa betri na kufunguliwa taa. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mara, Vedastus Maribe amesema wizi wa taa za barabarani na betri umekuwa ukiisababishia Serikali hasara.

Musoma. Zaidi ya taa 40 za barabarani zenye thamani ya Sh200 milioni zimeibwa na watu wasiojulikana mkoani Mara ndani ya miaka mitatu iliyopita.

Swali la haraka linaweza kuwa wizi huo unafanyikaje na muda gani? Hata hivyo, inaelezwa kuwa wezi hao wamekuwa wakipanda juu ya nguzo ya taa na kufungua betri pamoja na taa huku wakiacha nguzo zikiwa zimesimama tu, mithili ya mlingoti usio na bendera.

Katika baadhi ya matukio hasa ya Mji wa Tarime, nguzo za taa zilifunguliwa na kuangushwa chini kabla ya wahusika kuondoka na betri pamoja na taa.

Moja ya nguzo ya taa za  barabaranii wilayani Bunda ikiwa imenyofolewa betri na kufunguliwa taa. Picha na Beldina Nyakeke

Akizungumza na Mwananchi Digital, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mara, Vedastus Maribe amesema hali hiyo kwa namna moja au nyingine imekuwa ikiisababishia Serikali hasara huku wananchi wakiwa kwenye hatari ya kukosa manufaa yaliyokusudiwa.

Maribe amesema kipindi hicho cha miaka mitatu Serikali imetumia Sh2.8 bilioni kufunga taa 608  za barabarani  katika maeneo mbalimbali ndani ya mkoa huku kukiwa na matarajio ya mwaka huu kufunga taa zingine 336 katika maeneo mengine yaliyosalia.

Maribe amesema taa hizo zinazotumia nguvu ya jua (solar)  kwa sasa zinafungwa  maeneo ya miji na wilaya huku mchakato wa kufunga zingine ukiendelea.

Maeneo yanayopewa kipaumbele ni kwenye miji na sekta zenye mikusanyiko mikubwa ya watu.

Amesema baada ya kuibuka kwa mtandao wa watu wanaohusika na wizi huo wa taa, waliamua kubadili utaratibu wa ufungaji wake kwa hiyo, betri pamoja na taa zinakaa juu kabisa mwisho wa nguzo.

Maribe amesema kwa kufanya hivyo waliamini mtu hawezi  kufika juu kwenye nguzo aidha kwa kuogopa au kwa kuona ni usumbufu, lakini hali hiyo haikuzuia kitu chochote kwa watu kutoka kanda hiyo maalumu (ya kipolisi) kwa kuwa wizi umekuwa ukiendelea siku hadi siku.

"Tulidhani kwa taa za awali ambazo betri ilikuwa inafungwa kwa chini au katikati ya nguzo zilikuwa zikiwashawishi watu hawa kwa vile zilikuwa zinafikika kwa urahisi, hivyo tukabadili aina na kuanza kufunga betri juu kabisa, mwishoni mwa nguzo pamoja na taa lakini hata hizo naona bado wanapanda na kufungulia huko huko juu," amesema Maribe.

Kutokana na hali hiyo, amesema wametoa taarifa kwenye vyombo vya usalama  ili kuweza kubaini mtandao unahusika na wizi huo ili hatua zichukuliwe.

Wananchi wazungumza

Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mara wamesema vitendo vya wizi wa taa za barabarani ni uhujumu uchumi, huku wakiahidi kusaidiana na Serikali kuwasaka wahalifu ili hatua zichukuliwe dhidi yao.

"Hizi taa zina manufaa makubwa sana kwetu sisi, kwanza zinasaidia katika suala la ulinzi na usalama wa raia na mali zao, lakini zinapendezesha mji wetu, nitoe tu wito kwa wananchi wenzagu hili suala la wizi tulisimamie kwa pamoja tulitokomeze," amesema Anthony Okello, mkazi wa Musoma.

Nguzo ya taa za barabarani ikiwa imeangushwa na kunyofolewa betri na taa Wilaya ya Tarime. Picha na Beldina Nyakeke

Akizungumzia hilo, Annastazia Chacha amesema taa hizo zimewasaidia hasa kinamama na vijana wanaojishughulisha na biashara za mbogamboga na matunda pamoja na bodaboda kufanya shughuli zao hadi usiku na kuongeza kipato.

Amesema sio jambo jema kwa wakazi hao kukaa kimya huku vitendo vya hujuma vikifanyika.

"Nasikia zinatumika kwenye masuala ya uvuvi ndio maana wimbi la wizi limezidi, lakini hali hii inaweza kukomeshwa endapo wananchi tutashirikiana na Serikali kwa sababu wezi wanatoka miongoni mwetu, katika jamii na familia zetu," amesema Erasto Matienyi, mkazi wa Musoma.

Fazel Janja amesema betri za taa hizo hutumika hasa maeneo ya kwenye uvuvi kutokana na uwezo wale wa kukaa na umeme kwa muda mrefu.

Amefafanua kuwa shughuli zinazofanywa na betri hizo ni kufungwa kwenye  taa za wavuvi pamoja na taa za watu wanaofanya shughuli za kupiga muziki katika maeneo ya visiwani.

"Wanazifunga kwenye taa za uvuvi na zile za kwenye disko vumbi kwa sababu zinakaa na umeme muda mrefu, kwa hiyo wavuvi wakiingia ziwani wanakuwa na uhakika wa mwanga hasa nyakati za usiku na kwenye disko wakiziweka wanakuwa na uhakika wa mwanga hadi watakapomaliza kupiga muziki," amesema Janja.

Mwenyekiti wa mtaa

Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyiendo Mjini Bunda, Musa Maduka amesema walibaini taa nne za mtaani kwao kuibwa na watu wasiojulikana hivi karibuni.

"Hizi taa zilikuwepo jana, hadi tunakwenda kulala zilikuwa zinawaka ila watu wamezifungua usiku wa manane na tunaamini hao watu kabla ya kuiba wanafanya utafiti ili kuwa na ufahamu wa kutosha katika mazingira husika, haiwezekani mtu apande mpaka kule juu  kama hana uelewa wa mazingira ya hapa," amesema Maduka.

Amesema ipo haja ya Jeshi la Polisi kufanya operesheni katika maeneo mbalimbali yanayoweza kuwa maficho ya watu hao akitolea mfano wa jengo ambalo halijaisha lililopo kando ya barabara katika mtaa wake.

Maduka amesema  jengo kwa namna moja au nyingine, limekuwa likitumika kama maficho ya wahalifu.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vicent Naano amekiri kukithiri kwa vitendo hivyo katika wilaya yake na kwamba tayari hatua kadhaa zimechukukiwa kwa ajili ya kukomesha vitendo hivyo.

"Kwa sasa kuna mtandao tunaufuatilia nisingependa kuongea kwa undani kwa sababu tunachunguza tukimaliza tutasema," amesema Dk Naano.

Pia, amesema tayari wameishirikisha jamii katika kutambua mtandao wa wizi huo, lengo likiwa ni kuukomesha ili taa hizo ziweze kutumika kwa manufaa ya jamii kama ilivyo kusudiwa.

Amesema ushirikishaji huo utakwenda sambamba na utoaji wa Sh1 milioni kwa kila mtu atakayetoa taarifa zitakazochochea kukamatwa kwa wahusika wa mtandao huo huku akiahidi kuwepo kwa usiri na ulinzi wa watoa taarifa.

Dk Naano amesema vitendo vya wizi vimekithiri katika wilaya hiyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kukosekana kwa ushirikiano.

Amesema mhalifu akikamatwa hakuna mwananchi anayekubali kwenda kutoa ushahidi.

"Mtu anapanda hadi kule juu anaiba na hakuna taarifa inatolewa mfano jana wameiba ya pale karibu na Kanisa Katoliki yaani mtu anapanda na kufika kule juu kabisa kwenye taa na kushusha ya kwanza, ya pili ya tatu ina maana hakuna mtu aliyepita akamuona hata bodaboda hapiti?  Maana hakuna taarifa kabisa inayotolewa," amesema Dk Naano.

Ameeleza namna taa hizo zinavyoibiwa akisema mtuhumiwa anapanda juu ya nguzo ya taa kisha kufungua betri na kuondoka nayo na kwamba betri ikiondolewa taa haiwezi tena kufanya kazi.

"Hapa Bunda kitu kikiibwa walioona hawatoi taarifa, aliyeuziwa hatoi taarifa na hii imesababisha wizi kukithiri kila mahali kwa sababu wanaofanya uhalifu ni watoto wetu, uhalifu haitakiwi kufichwa kwa namna yoyote ile, uhalifu ni lazima ushughulikiwe," amesema Dk Naano.

Amesema zipo sababu zinazochochea vitendo vya wizi katika wilaya hiyo huku akitaja baadhi kuwa ni uvutaji wa bangi, vitendo vya kamari huku vijana wakiwa hawataki kujishughulisha na shughuli za kimaendeleo.

Polisi wanena

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salim Morcase amesema tayari ofisi yake inafanyia kazi taarifa za uwepo wa vitendo hivyo katika mkoa.

"Huu wizi wa betri za sola za taa za barabarani  unafanyiwa kazi, mfano kuna betri nne za sola ziliibwa hivi karibuni katika Barabara ya Bulamba - Kisorya kule Bunda," amesema Kamanda Morcase.