Uteuzi NEC waibua kilio cha Katiba

Muktasari:
- Siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya uteuzi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), hatua hiyo, imeibua upya kilio cha kudai Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.
Dodoma. Siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya uteuzi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), hatua hiyo, imeibua upya kilio cha kudai Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.
Madai hayo mawili yanatajwa kuwa ndio mwarubaini wa changamoto zinazojitokeza kwenye chaguzi.
Februari 26, 2023 Rais Samia alimteua Ramadhan Kailima kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, akichukua nafasi ya Dk Wilson Mahera aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu Tamisemi.
Kabla ya Dk Mahera, nafasi hiyo iliwahi kushikwa na Dk Athumani Kihamia ambaye alichukua wadhifa huo Julai 2018 kutoka kwa Kailima aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Akizungumza katika mjadala wa Twitter Space ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), uliobeba mada: Uteuzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) utaleta mabadiliko yoyote?, msemaji wa masuala ya Katiba wa chama cha ACT- Wazalendo, Victor Kweka, alisema ni muda mwafaka kwa Rais Samia kuendelea na mchakato wake wa maridhiano, kwa kuanza kuiunganisha Tanzania kwa kuipatia sheria mpya ya uchaguzi kabla ya 2025.
“Hii itawezesha watu kuona ni kweli maridhiano ambayo tumekuwa tukiyaimba kila mara yaweze kuonekana kwamba ana dhamira ya dhati ya kuwezesha hili. Mimi naamini kuwa hadi kufikia hapa tulipo ni utashi wake kwa sababu sio rahisi kufikia hapa,” alisema.
Hata hivyo, alisema ili kufikia mwisho mzuri na kuunganisha imani ya Watanzania hata katika ushiriki wa uchaguzi wanaamini ni muhimu kuwapatia tume huru ya uchaguzi na sheria mpya za uchaguzi zitakazotibu changamoto zilizopo.
Mifumo mipya inahitajika
Mchokoza mada na mhariri wa siasa wa MCL, Salehe Mohamed alishauri Katiba na sheria zifanyiwe marekebisho ili kutengeneza mazingira ambayo yatawezesha kila mmoja kutambua njia salama na kuwa kwenye mfumo ambao utamwezesha kufurahia matunda ya uhuru.
Alisema ili kupata maendeleo ni muhimu kwa Taifa kutengeneza mifumo mizuri kwa kuifanya Katiba kuwa wazi.
“Sisi tutengeneze mifumo ambayo itatufanya watendaji wetu wawe na uhuru zaidi. Kwenye rasimu ya pili ya mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji mstaafu Joseph Warioba, ilipendekeza kumpunguzia Rais madaraka ya uteuzi,” alisema Salehe.
Alisema hivi sasa Rais anateua hata mkurugenzi, mkuu wa wilaya, hivyo kumfanya kuwa na mambo mengi ya kufanya.
Aidha, Mohamed alishauri kuangaliwa kwa mfumo ambao utawezesha Taifa kuwa na amani, uhuru na utulivu.
Alisema uteuzi wa Kailima umekuwa ukipata maswali na kuwa na mjadala mkubwa, kwa sababu watu wana kumbukumbu na uchaguzi uliofanyika mwaka 2020 wakati Mahera akiwa mkurugenzi wa uchaguzi Nec.
Alisema tangu Tanzania iingie katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na kufanya uchaguzi mkuu wa kwanza mwaka 1995, uchaguzi mkuu wa 2020 ndio ambao idadi kubwa ya wagombea kutoka vyama vya upinzani walienguliwa kugombea.
Alisema baadhi ya wagombea hao walienguliwa katika hatua za awali kwa sababu ya kukosea kuandika herufi moja katika majina, huku wagombea zaidi 20 wa CCM wakipita bila kupingwa.
“Hii inawapa hofu wakati huo Mkurugenzi wa uchaguzi alikuwa ni Wilson Mahera ambaye sasa kapelekwa Tamisemi (Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa),”alisema.
Alisema uchaguzi unasimamiwa na wakurugenzi ambao wako chini ya Tamisemi ndio maana watu wanapata hofu aliyeondolewa NEC amepelekwa Tamisemi, hatua in
Kwa upande wake, mchangiaji Richard Kanje alihoji: ‘‘ Kwa nini Tanzania yenye watu milioni 60 inaongozwa na utashi wa mtu mmoja, kwa nini wasitengeneze Katiba ambayo inatambua haki na wajibu na kuheshimu haki za watu.
“Kwenye mfumo wa vyama vingi hii siyo haki, tunatakiwa kuwa na mfumo ambao hauingiliani na Rais ambapo Rais hahusiki kuteua mwenyekiti ama mkurugenzi anayehusika kusimamia uchaguzi, kwa sababu hapa kuna masilahi binafsi.’’
Alisema kwa uteuzi uliofanyika hivi karibuni hawategemei mabadiliko kulingana na muundo wa Katiba ulivyo.
Naye Mussa Moses alisema anahisi kuwapo kwa hali ya kuzungukana wakati huu ambao nchi iko katika maridhiano.
Alisema wakati wanasiasa wamo katika maridhiano ya kumaliza kero za uchaguzi, Rais kwa upande wake anateua mtu aliyedai kuwa hakufanya vizuri siku za nyuma.
‘‘Tunashindwa kufahamu kwa nini Rais ameamua kumrudisha Tume ya Uchaguzi,” alieleza Moses.