Siri minyukano ya vigogo serikalini

Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla akizungumza na aliyekuwa Katibu mkuu wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda walipokutana jijini Mwanza kumaliza tofauti zao kama walivyoagizwa na Rais John Magufuli. Picha na maktaba
Dar es Salaam. Ubinafsi na kukosekana kwa mawasiliano miongoni mwa viongozi wa umma ni miongoni mwa mambo ambayo yametajwa kuwa sababu za mivutano kati ya mawaziri na wasaidizi wao wizarani.
Hayo yamebainishwa siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa “onyo la mwisho” kwa mawaziri, naibu mawaziri na makatibu wakuu alipokuwa akiwaapisha Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma juzi.
Kauli hiyo imeibua tatizo la siku nyingi ndani ya Serikali, la kuwepo kwa mgongano wa viongozi wa umma katika wizara mbalimbali, baadhi ikielezwa waziwazi na mingine ikiendelea chini kwa chini.
Akizungumzia migongano hiyo, Katibu Mkuu mstaafu aliyehudumu muda mrefu katika Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Dk Laurian Ndumbaro alisema sababu kubwa ni ubinafsi na kushindwa kutafsiri majukumu.
“Wakati mwingine ni personalities (ubinafsi) kwa sababu hata wewe unaweza kuwa umezaliwa nyumba moja na mdogo wako lakini mkagombana kwa personalities tu na wakati mwingine inawezekana una tafsiri tofauti mujukumu yako,” alisema.
Akifafanua zaidi kuhusu suala hilo alisema, “unaweza kukuta katika wizara hiyo watu wakafanya vizuri, hakuna migongano, lakini wakawekwa wengine wakagongana kwa sababu ya personalities.”
Kuhusu utatuzi wa migongano hiyo, Dk Ndumbaro alisema inapotokea, Rais aliyewateua ndiye huamua.
“Mara nyingi Katibu Mkuu kiongozi ndiye anakuwa mamlaka ya nidhamu kwa wale wateule wa Rais na kwa mawaziri na manaibu waziri Rais mwenyewe anashughulikia (migogoro yao) na kuna njia nyingi anazitumia.”
Alisema Rais anaweza kutoa maelekezo kwa mamlaka yoyote ikaenda kuwashauri.”
Akifafanua kuhusu mipaka ya majukumu katika wizara, Dk Ndumbaro alisema kila mtu anakuwa na majukumu yake na katika wizara mwenye ofisi ni waziri.
“Hivyo, naibu waziri anapewa majukumu na waziri kwa kumwandikia. Kwa hiyo kila mtu anakuwa na majukumu yake. Lakini ukimkabidhi mtu majukumu haina maana kwamba huwezi kufanya eneo hilo, unaweza pia kwenda kufanya.
“Kuna wizara ambazo Rais mwenyewe anawapangia majukumu makatibu wakuumoja kwa moja.
Kwa mfano Tamisemi, kunakuwa na naibu katibu mkuu afya, naibu katibu mkuu elimu, kwa hiyo Rais ameshabainisha kuwa huyu akienda kule anakuwa ana shughulikia elimu, au anashughulikia afya na huyu mwingine anashughulikia Tamisemi au naibu katibu mkuu uvuvi au naibu katibu mkuu mifugo,” alisema.
Hata hivyo, alisema kwa wizara nyingine ambazo Rais hatamki moja kwa moja, katibu mkuu au waziri ndiye anapanga majukumu.
Katibu mkuu mwingine mstaafu wa Utumishi, Ruth Mollel alitaja tatizo la kukosekana mawasiliano miongoni mwao kuwa moja ya sababu za migongano.
“Nafikiri inategemea na nadharia za kila kiongozi katika nafasi yake katika ufanyaji wa uamuzi, je, wanawasiliana au hawawasiliani? Inapendeza katibu mkuu kabla hujafanya jambo ambalo labda waziri anapaswa kulifahamu, ni vizuri kumjulisha kwanza,” alisema.
Ili kuondokana na migongano hiyo, Mollel alisema waziri hapaswi kuingilia kazi za utendaji wa katibu mkuu.
Akieleza zaidi, Mollel alisema ili kuepusha migongano, kiongozi wa chini anapaswa kuwa wazi kwa bosi wake anayempa maelekezo yasiyotekelezeka.
“Unaweza ukaambiwa utekeleze jambo, lakini unajua kwa taratibu za Serikali halitekelezeki, hivyo utamwandikia waziri kwamba ‘uliniagiza nitekeleze ABCD lakini kanuni inasema hivi na hivi, kwa hiyo nashauri hivi na hivi, unampelekea,” alisema.
Aliendelea, “kati ya katibu mkuu na naibu katibu mkuu ni muhimu sana kugawana kazi. Usimwache naibu katibu mkuu wako akija tangu asubuhi anasoma magazeti.”
Suala hilo pia linajadiliwa na Dk Eunice Nnkya, mtafiti wa utawala bora anayesema kwa kuwa Rais ana mamlaka ya kuteua, anapaswa kuwapitisha wateule wake kuelewa majukumu wanayotakiwa kufanya kwa mujibu wa Katiba.
“Ili kuepuka migongano hii, kama Taifa tunapaswa kuwachukua viongozi waandamizi wa Serikali kama mawaziri na manaibu waziri na makatibu wakuu kuchunguzwa kabla ya kuapishwa, hii itaepusha ushindani miongoni mwa mawaziri,” alisema.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Yusto Mvungi alisema kuwa na mamlaka ya uteuzi pasipo kufanya uchunguzi na usaili nalo ni tatizo.
“Inaweza kutokea kwamba, katibu mkuu anafikiria kuwa ana uwezo kiutendaji na wakati mwingine anakuwa na elimu na uzoefu, kwa hiyo kwa kuwa hakuna upembuzi wala usaili, wanafikiria kila mmoja ni bora kuliko mwenzake.
“Unaweza kukuta waziri ni profesa, naibu waziri ni daktari na katibu mkuu ni profesa, hapo bila mafunzo migongano kati yao haitakwisha,” alisema.
Juzi Dk George Kahangwa, mhadhiri mwingine UDSM alisema ofisi ya Rais inapaswa kuainisha majukumu ya kila kiongozi aliyeteuliwa.