Polisi waimarisha ulinzi nje ya Kanisa la KKAM

Muktasari:
- Leo ni Jumapili ya tano kwa waumini wa Askofu Gwajima kufanya ibada nje ya kanisa lao ambalo limezungushiwa utepe na kuwa chini ya ulinzi wa polisi.
Dar es Salaam. Lolote linaweza kutokea! ndiyo hali halisi iliyopo katika ibada ya Jumapili ya leo Julai 6, 2025 kwa waumini wa lililokuwa kanisa la ufufuo na uzima la Askofu Josephat Gwajima na wale wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM) dhidi ya Jeshi la Polisi.
Waumini hao wameamua kufanya ibada ya pamoja tangu Jumapili iliyopita baada ya kanisa la Ufufuo na Uzima kufutwa na Serikali tangu Juni 2, 2025.
Baada ya kanisa hilo kufutwa kwa kile kilichoelezwa limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi, waumini hao wamekuwa wakisalia barabarani jirani na yalipo makao makuu ya kanisa lao, Ubungo na mara kwa mara wametawanywa na polisi kwa kupigwa mabomu ya machozi na wengine kupelekwa polisi na kuachiwa kwa dhamana.
Jumapili ya leo ni ya pili tangu waumini wa kanisa hilo kuungana na wale wa KKAM na kufanya ibada, Jumapili iliyopita baada ya ibada waliingia barabarani wakiwa wamebeba mabango wakidai uhuru wa kuabudu na kutawanywa kwa kupigwa mabomu ya machozi huku wengine 52 wakikamatwa.
Leo Jeshi la Polisi ni kama linawasikilizia waumini hao wajichanganye na kuvuka eneo la kanisa na kuingia barabarani ili kuwadhibiti.
Hiyo ni baada ya kuimarisha ulinzi zaidi, likiwa limeongeza idadi ya polisi kulinganisha na Jumapili iliyopita.
Gari nane za polisi ikiwamo basi ndogo ya jeshi hilo zenye askari ndani yake kwa ajili ya kutuliza ghasia ziko mita kama 100 kutoka lilipo kanisa la KKAM ambako ibada inaendelea.
Hata hivyo gari nyingine moja ya polisi ipo umbali wa takriban mita tano kutoka walipo waumini na mara kadhaa baadhi ya askari wenye silaha wamekuwa wakitembea tembea eneo hilo kuhakikisha ulinzi unaimarika.