Tanzania inahitaji Katiba inayotambua haki
Muktasari:
- Kilio cha Katiba Mpya bado kimeendelea kusikika nchini baada ya baadhi ya watu kueleza kuwa ndio mwarobaini wa kupatikana kwa Tume bora.
Dodoma. Mtanzania Richard Kanje amehoji kwa nini Tanzania yenye watu milioni 60 inaongozwa na utashi wa mtu mmoja , kwa nini wasitengeneze Katiba ambayo inatambua haki na wajibu na kuheshimu haki za watu.
Kanje ameyasema hayo leo Jumatano Machi Mosi, 2023 wakati wa mjadala wa Twitter Space ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), uliobeba mada ya uteuzi wa NEC utaleta mabadiliko yoyote.
Amesema ni wajibu wa Rais kufanya hivyo kwa sababu Katiba inampa madaraka hayo na kwamba pale anapotakiwa kutimiza jukumu la kikatiba ni lazima afanye hivyo.
Amesema Rais ana watu wanaowajibika kwake ambao anaweza kuwafukuza na uwezo wa kuajiri na hivyo anaangalia watu wanaoendana na sera zake.
James amesema Rais anamteua ni nani ambaye atasimamia uchaguzi ambao unaoamua ni nani awe Rais na ni nani atakuwa mbunge, nani awe diwani.
“Kwenye mfumo wa vyama vingi hii siyo haki, tunatakiwa kuwa na mfumo ambao hauingiliani na Rais ambapo Rais ahusiki kuteua mwenyekiti ama mkurugenzi anayehusika kusimamia uchaguzi, kwa sababu hapa kuna masilahi binafsi,” amesema.
Amesema kwa uteuzi huo hawategemei mabadiliko yoyote kwa muundo wa Katiba ulivyo.
“Lakini Rais Samia Suluhu Hassan yupo sahihi kabisa kufanya uteuzi lakini kulingana na muundo wa Katiba na vyama vingi, lakini wanatumia Katiba ya mwaka 1977 wakati hawajaingia katika vyama vingi.
“Kwa hiyo tunapoingia katika mfumo wa vyama vingi na Katiba inayoruhusu mfumo wa siasa za chama kimoja natumaini hatutendi haki,” amesema.
Amehoji kwa nini nchi yenye watu milioni 60 inaongozwa na utashi wa mtu mmoja, kwa nini wasitengeneze Katiba ambayo inatambua haki na wajibu na kuheshimu haki za watu.
“Kama kwenda kupiga kura ni haki yako, na kumchagua kiongozi ni haki yako, lakini unapochagua kiongozi unayemtaka, lakini kukawa na kanuni kuwa huyu sawa tunamtaka, lakini si tunamtaka huyu yaani kuna mtu anakupangia hilo taifa haliwezi kutoka vile,” amesema.