‘Wakulima wapewe taarifa sahihi za hali ya hewa kukuza uzalishaji’

Muktasari:
- Ili kuoata matokeo tarajiwa katika kilimo, imeshauriwa taarifa za utabiri wa hali ya hewa zifikishwe katika ngazi ya kata waliko wakulima ili ziweze kuwasaidia.
Dar es Salaam. Ripoti za hali ya hewa zimetajwa kuwa moja ya njia inayoweza kuchochea uzalishaji katika kilimo ikiwa zitawafikia wakulima moja kwa moja.
Hayo yameelezwa leo Agosti 30 na Mhariri wa takwimu wa Mwananchi, Halili Letea wakati akichangia mjadala kwa njia ya mtandao uliandaliwa na Mwananchi, Mwananchi Twitter Space ikiwa na mada “Nini kifanyike kuboresha kilimo biashara na uhifadhi wa chakula.”
Letea amesema dunia kwa sasa inakabiliwa na mabadiliko ya tabia nchi na kuona madhara yake yameanza kuoneka hasa katika bara la Afrika hivyo ni vyema kuhakikisha usalama na uhakika wa chakula.
Amesema Tanzania ina maeneo mengi ambayo yanaweza kufanyika kilimo ila swali linalokuna ni kilimo kinachofanyika kina tija au mtu anafanya kwa ajili ya matumizi yake tu.
"Tunatakiwa kutegemea ripoti za mienendo ya hali ya hewa kwa kuwa ndizo zitakazosaidia wakulima. Kuna haja ya kuboresha upatikanaji wa taarifa hizi na zinapaswa kuwafikia walengwa," amesema Letea.
Amesema hiyo ni kutokana na kile alichokielezwa ukiwauliza watu wa vijijini taarifa ya eneo lake juu ya hali ya hewa hawajui lakini watu wa mjini wakiulizwa watakuambia.
"Kwa hiyo ni muhimu Serikali ihakikishe inafika hadi ngazi ya serikali za mitaa hata kama kuna ugumu wa kufikisha taarifa hizi kila siku wafanye hivyo hata kwa wiki au mwezi ili kila mkulima awe na taarifa hizi ajiandae kwenye kilimo," amesema Letea.
Pia amesema ni vyema ikawepo elimu ya kutosha kwa wakulima kwenye uhifadhi wa chakula kwani takwimu za chakula zinaonyesha kuwa takribani nusu ya mazao kabla ya kuvuna.
Akizungumzia Jukwaa la Mifumo ya Chakula Barani Afrika 2023 (AGRF) linalotarajiwa kufanyika Septemba 5 hadi 8, 2023, mdau wa kilimo, Audax Lukonge amesema matarajio yake ni Afrika kuonyesha kwa kiasi gani inaweza kuboresha biashara ndani ya bara la lake.
"Kwa kuwa huu mkutano watakuwepo wakuu wa nchi waliopo madarakani na wastaafu nafikiri kwa pamoja tukubaliane kusaidiana nchi gani zijikite kwenye uzalishaji wa mbolea. Lengo ni kupunguza utegemezi wa kuagiza mbolea kutoka nje ya bara la Afrika," amesema Lukonge.
Pia ameeleza kuwa kama bara linatakiwa kutathmini yale yote yanayijadiliwa kwenye mikutano hiyo ili kujua yametekelezea kwa kiasi gani ili bara lisiachwe nyuma.