‘Wanafunzi wasio na sare wasirudishwe nyumbani’
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu
Muktasari:
- Siku tatu kabla ya kuanza kwa muhula mpya wa masomo 2024, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amewaagiza wakuu wa shule mkoani humo kutowarudisha nyumbani wanafunzi wasiokuwa na sare za shule.
Moshi. Zikiwa zimesalia siku tatu kabla ya kufunguliwa kwa shule za msingi na sekondari nchini, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amewaagiza wakuu wa shule mkoani humo kutowarudisha nyumbani wanafunzi wasiokuwa na sare za shule.
Babu amesema hayo leo Ijumaa, Januari 5, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari na suala la mwanafunzi kukosa viatu au sare za shule lisimfanye mwalimu kumrudisha nyumbani kwa kuwa mengine yanazungumzika.
"Nitoe wito kwa walimu wote, mwanafunzi atakapokwenda kuripoti Januari 8, 2024 wote wapokelewe bila kujali ana viatu au hana, ana sare au hana.
“Haya mengine yanazungumzika wakati mtoto akiwa darasani anaendelea na masomo, asirudishwe nyumbani," amesema Babu.
Pia, amesema ni marufuku wakuu wa shule kuendesha michango isiyo ya lazima shuleni na kwamba kama kuna michango inafanyika kuna utaratibu wa kufuatwa.
"Sitaki kusikia michango isiyokuwa na utaratibu, michango yote lazima kamati ya shule ikae, ilete barua kwa Katibu Tawala wa Mkoa, kisha iletwe kwangu. Mimi ndiye ninayetoa kibali cha michango mbalimbali inayoendelea au wakuu wa wilaya," amesema mkuu huyo wa mkoa.
Pamoja na mambo mengine, ametoa rai kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mkoani humo wote wanaripoti shuleni bila kisingizio kwa kuwa Serikali imefuta ada.
"Wananchi wapenda elimu kwa mkoa wa Kilimanjaro, tuhakikishe kila mtoto aliyechaguliwa kuingia kidato cha kwanza anaripoti kwenye shule aliyopangiwa bila kisingizio cha aina yoyote,” amesema.
Babu amesema jumla ya wanafunzi 36, 570 wakiwemo wavulana 18, 013 na wasichana 18, 557 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule mbalimbali mkoani humo.
"Naomba niwahakikishie watoto hawa watakwenda shule zikiwa zimekamilika, tumejenga shule mpya 19 katika mkoa wetu na shule moja ni ya wasichana ambayo Serikali imetupa Sh3 bilioni kuijenga, ujenzi umefikia asimilia 80 sasa na tupo tayari kuwapokea wanafunzi,” amesema.
Kwa upande wa darasa la kwanza, amesema wameshaandikisha wanafunzi 22,207 sawa na asilimia 60.
“Baada ya sikukuu kasi ya kupeleka watoto shule imeongezeka, mpaka tukifungua tutakuwa tufika asilimia kubwa zaidi, watoto wa elimu ya awali tumeshaandikisha wanafunzi 20,261 sawa na asilimia 56," amesema huku akiwakumbusha wazazi na walezi kuchangia chakula shuleni.