Wanawake Lindi waonywa mikopo ya ‘kausha damu’

Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga akizungumza na wanawake wafanyabiashara  kwenye ufunguzi wa mafunzo ya wajasiriamali yanayofanyika  mkoani Lindi.Picha na Bahati Mwatesa

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga amesema mikopo ya ‘kausha damu’ haina utaratibu mzuri.

Lindi. Wanawake wafanyabiashara mkoani Lindi wameonywa kuhusu uchukuaji wa mikopo ya kausha damu, badala yake wamehimizwa kwenda kukopa kwenye taasisi rasmi zinazofuata utaratibu.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Aprili 9, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya ujasiriamali yaliyoandaliwa na Chama cha Wafanyabiashara Wanawake (TWCC).

Katika mafunzo hayo, wanawake wamekumbushwa kuacha kukopa mikopo ya ‘kausha damu,’ badala yake wakope kwenye taasisi rasmi ili kuepuka kuchukuliwa mali zao na watu waliowakopesha.

Ndemanga amesisitiza kuwa mikopo ya ‘kausha damu’ haina utaratibu mzuri, jambo linalosababisha wanawake wengi kupoteza mali zao pindi wanaposhindwa kurejesha mikopo hiyo.

“Ofisini kwangu ilishakuja kesi, kuna mwanamke alichukua mkopo wa ‘kausha damu,’ akaletwa ofisini kwangu, ikabidi niongee na mwenye mkopo wake ili aweze kulipa taratibu, lakini angechukua kwenye taasisi zenye utaratibu, asingeweza hata kuletwa kwangu,” amesema Ndemanga.

Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Mwajuma Hamza amesema wanawake 100 watapatiwa mafunzo ya ujasiriamali yatakayowasaidia kupata elimu ya masoko ili kuuza bidhaa zao ndani na nje ya nchi.

“Lengo la mafunzo haya ni kuwasaidia wanawake kupata soko huru la Afrika litakalowasaidia kuuza bidhaa zao ndani na nje ya nchi, pia kujua jinsi gani ya kufungasha bidhaa zao na kuwa zenye ubora,” amesema Mwajuma.

Katibu wa TWCC Mkoa wa Lindi, Fatuma Juma amesema mafunzo watakayoyapata yatawasaidia kutoka sehemu moja na kwenda sehemu nyingine kwa kuwa, baadhi ya wafanyabiashara hawajui umuhimu wa bidhaa yenye ubora pamoja na kufungasha bidhaa kwa kufuata vipimo maalumu.

“Binafsi nilikuwa nakadiria kuweka bidhaa yangu bila kutumia vipimo maalumu, lakini mafunzo haya yatanisaidia sana,kujua jinsi ya kupima kwa uhakika na kuipeki vizuri,” amesema Fatuma.

Mwenyekiti wa TWCC Mkoa wa Lindi, Pendo Mindi amewaasa kinamama wafanyabiashara kuacha tabia ya kukata tamaa, bali wapambane na changamoto ili kufikia malengo yao.

 “Unamkuta mwanamke amepata elimu kama hii, mwenzie akimwambia nielekeze na mimi mlichojifunza huko anamkatalia, hiyo haipo sawa, kama umepata elimu ya ujasiriamali mwenzio hakuweza kushiriki amekuomba mfundishe  ili muweze kupiga hatua kwenye biashara zenu,” amesema Pendo.

Hadija Mkalindende, muuzaji wa mwani wilayani Lindi, amesema mafunzo atakayopata yatamsaidia kukuza biashara yake, kwa kuwa kuna vitu alikuwa havijui lakini kupitia mafunzo hayo atakwenda kujifunza.

“Nawashukuru sana watu wa TWCC kwa kuandaa mafunzo kwa ajili ya wanawake wa Lindi, nitakwenda kujifunza zaidi vitu nilivyokuwa sivijui hapo awali,” amesema Hadija.