Takukuru yataka wanawake kupinga rushwa ya ngono

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Arusha,  Zawadi Ngailo akipanda moja ya miti katika Hospitali ya Jiji la Arusha, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya taasisi hiyo kuelekea siku ya kimataifa ya Mwanamke duniani itakayofikia kilele chake Machi 8.

Muktasari:

  • Wakati dunia ikielekea kwenye maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani Machi 8, 2024  Taasisi ya Kupambana na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Halmashauri ya jiji hilo, wameanza upandaji miti 100 katika hospitali mpya ya jiji kwa ajili ya utunzaji wa mazingira.

Arusha. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Arusha, imesema kuwa suluhisho la kukomesha rushwa ya ngono dhidi ya wanawake ni wanawake wenyewe.

Hayo yamesemwa leo Machi 6, 2024 na Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo, kwenye uzinduzi wa wiki ya maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani iliyofanyika katika hospitali ya jiji la Arusha iliyoko Njiro.

Katika maadhimisho hayo yaliyokwenda sambamba na upandaji miti katika mazingira ya hospitali hiyo, Zawadi amesema, ni wazi mwanamke ndio mwathirika mkubwa wa rushwa hasa ya ngono, lakini pia anaweza kuwa suluhsho la tatizo.

“Wanawake ndio kundi kubwa la uzalishaji mali, lakini mmekuwa waathirika wakubwa wa rushwa hasa ya ngono, lakini jueni kuwa utumwa huu mnajitakia wenyewe, kwani panga la kukata mnyororo huo mmelishika ninyi,” amesema Zawadi.

Zawadi amewataka wanawake kukataa utumwa huo kwa vitendo na kutoa taarifa za viashiria au utekelezaji wa rushwa kwa ajili ya usalama wao na vizazi vijavyo.

 “Rushwa haiwezi kuisha endapo tutazidi kunyamazia vitendo hivi, tena tukiwa watekelezaji wake. Jamani wanawake chukueni hatua madhubuti ya kukata mnyororo huu kwa kukataa kutekeleza na kutoa taarifa na zaidi pia ushahidi mahakamni mkihitajika muwe mstari wa mbele,” amesema Zawadi.

 “Katika shughuli hii, mbali na utunzaji wa mazingira lakini tulilenga pia kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa, dawa za kulevya lakini pia maadili ukizingatia sekta ya afya isipotolewa huduma vema inaibua malalamiko ya rushwa” amesema Zawadi.

Kwa upande wake Katibu wa Afya, jiji la Arusha Hamida Kiligaliga,  amesema kuwa kazi ya upandaji miti iliyofanywa siku hii ya leo katika hospitali hiyo, itabaki kuwa kumbukumbu njema kwa siku zote za maadhimisho ya wanawake duniani.

“Miti hii iliyoletwa mbali na kuwa vivuli, mingine   ina uwezo mkubwa pia wa kuzuia mbu,  hivyo itasaidia hata wagonjwa wanaokuja kupata huduma hapa kuwa salama zaidi lakini pia kupata hewa kutokana na mandhari nzuri iliyojengeka” amesema Hamida.

Mmoja wa wagonjwa hospitalini hapo, Anna Swai amesema kuwa maadhimisho ya siku ya wanawake yenye lengo la kuhamasisha usawa wa kijinsia, yaangazie pia fursa sawa kwenye nafasi ya uongozi na ajira kwenye taasisi mbalimbali.