Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watalii wanaokuja nchini wafikia milioni 1.2

Arusha. Sekta ya utalii nchini imeendelea kuimarika baada ya athari za janga la Uviko-19, ambapo mwaka 2022 watalii wameongezeka na kufikia milioni 1.29 ikilinganishwa na watalii 922,692 waliokuja nchini mwaka 2021.

Ongezeko hili la watalii ni asilimia 71.02 kuanzia Januari hadi Novemba 2022, ambapo Serikali imeweka lengo kuwa ifikapo mwaka 2025 ipokee watalii milioni tano kwa mwaka na mapato kufikia Dola bilioni 6.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana alitoa taarifa hiyo jana, katika mkutano wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) wa mashauriano baina ya sekta binafsi na sekta za umma katika sekta ya utalii.

Dk Chana alisema ongezeko hilo la watalii limetokana na jitihada za Serikali na wadau wa utalii, zikiwemo kukuza, kuendeleza na kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii kwa kutumia Programu ya ‘The Royal Tour.’

Alisema ongezeko hilo limechangiwa na uboreshaji wa miundombinu ya utalii, hudumaa na kuimarisha matumizi ya Tehama.

Akizungumzia mkutano wa mwisho wa baraza hilo, uliofanyika Julai, 2022 alisema yaliwasilishwa maeneo yanayohitaji maboresho katika utekelezaji wa Maazimio ya Mkutano wa 13 wa TNBC Maeneo, ambapo yaliyoainishwa ni pamoja na mapitio ya Sheria ya Utalii Namba 29 ya mwaka 2008, uboreshaji wa mifumo ya malipo ili kuwezesha kuwa na dirisha moja la malipo.

Akitoa mrejesho wa jitihada za Serikali kutatua changamoto katika sekta ya Utalii, Kaimu Mkurugenzi wa Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, Richie Wandwi alisema wizara hiyo kwa kushirikiana na wizara nyingine zimetatua baadhi ya kero na nyingine zipo katika mchakato.

Alisema kulikuwa na hoja 24 zilizotolewa katika mkutano uliopita na nyingi zimepatiwa ufumbuzi, ikiwepo kupunguza idadi ya kaguzi, kuwepo kwa dirisha moja la malipo na ada katika sekta hiyo, lakini pia kuongeza muda wa dhamana kutoka siku 30 hadi 90.

Akizungumzia changamoto ya malipo ya wapagazi na mishahara katika sekta ya utalii, alisema tayari wizara ilifanya mazungumzo na Wizara ya Kazi, ambapo idara ya kazi imepewa jukumu la kufanyia kazi changamoto ya mikataba ya wapagazi na malipo yao. Kuhusiana na malipo ya waongoza watalii kupunguzwa kutoka dola 50 hadi 20 kwa mwaka, alisema jambo hilo ni la kisheria, lakini linaendelea kufanyiwa kazi, huku pia suala la malazi katika hifadhi na kambi za kitalii linaendelea kupata ufumbuzi.

Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa chama cha wapagazi (TOP), Loshiye Mollel aliomba Wizara ya Maliasili na Utalii, kupatia ufumbuzi malipo na stahiki za wapagazi zaidi ya 20,000 wanaofanya kazi kusaidia watalii mlima Kilimanjaro, kwani ni madogo.

“Bado wapagazi wanalipwa chini ya dola 10 kwa siku kupanda mlima, bado hakuna mikataba, tunadhani jitihada zinahitajika ili wapagazi wafanye kazi nzuri na bado Idara ya Kazi imeshindwa kutukutanisha wapagazi na wenye kampuni za utalii kupata suluhu,” alisema.