Waziri Gwajima ataja dawa ya ukatili wa kijinsia kwenye familia

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima akizungumza kwenye mafunzo ya awamu ya pili ya programu ya Jukwaa la kizazi chenye usawa wa kiuchumi kwa waratibu kutoka mikoa 15 jijini Mwanza

Muktasari:

Migogoro ya kiuchumi imetajwa kuwa miongoni mwa visababishi vya ukatili wa kijinsia huku jamii ikitakiwa kutoa fursa sawa za kiuchumi kwa wanawake na wanaume ili kupunguza utegemezi.


Mwanza. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima, ameitaja migogoro ya kiuchumi kuwa moja ya sababu zinazochangia ukatili wa kijinsia hususani kwenye familia.

Akifungua mafunzo ya Programu ya Jukwaa la Kizazi chenye Usawa (GEF) leo Jumatatu Januari 15, 2024 kwa waratibu wa ngazi za halmashauri na mikoa 15 yanayofanyika siku mbili jijini Mwanza, Dk Gwajima amesema ili kuondoa migogoro hiyo ipo haja ya usawa wa kijinsia utakaofanya wanaume wanufaike na fursa za kiuchumi bila kuwaacha nyuma wanawake.

“Haki hizi ziwe na sura ya usawa wa kijinsia kwamba siyo tu jinsi ya kiume inanufaika na fursa za kiuchumi bali wanawake pia wanufaike kwani bila kufanya hivyo tukawaacha wanawake nyuma mfumo mzima wa nafasi ya wanawake kwenye kusukuma maendeleo na ustawi wa jamii, utaharibika,” amesema.

Dk Gwajima amewaelekeza waratibu kuhakikisha usawa wa kiuchumi unazingatiwa kwenye mipango na bajeti zao, kuandaa taarifa za utekelezaji, kutoa elimu ya masuala yanayotekelezwa na programu hiyo kwa wadau.

Mengine aliyowaelekeza kuhakikisha wanatekeleza, ni kushiriki vikao na mikutano mbalimbali ili kuieleza jamii na kuihamasisha kuhusiana na programu hiyo.

Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Jinsia na Wanawake, Juliana Kibonde amewataka waratibu hao kuhakikisha kunakuwa na mrengo wa kijinsia katika miradi, afua na masuala ya uongozi kwenye maeneo yao ili usawa wa kiuchumi ufikiwe.

Mshiriki wa mafunzo hayo, Gasto Didas amesema usawa wa kiuchumi katika jamii bado haujaimarika kama inavyotakiwa akishauri wadau waendelee kushirikiana na Serikali kuhakikisha unafikiwa kuondoa baadhi ya vitu ikiwemo utegemezi na migogoro ya kifamilia.

Jukwaa la Kizazi chenye Usawa ni jukwaa la kimataifa lililoitishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Wanawake na Usawa wa Jinsia (UN Women) kwa kushirikiana na Serikali za Mexico na Ufaransa lengo likiwa ni kuharakisha utekelezaji wa ahadi za usawa wa kijinsia zilizopatikana baada ya tathmini ya utekelezaji wa Azimio la Ulingo wa Beijing na kubaini vikwazo vya kufikia usawa huo.

Baadhi ya vikwazo hivyo ni unyanyasaji wa kijinsia, mabadiliko ya tabianchi, na mifumo ya kiuchumi ambayo inawaacha nyuma wanawake na wasichana, ambapo Serikali ya Tanzania ni miongoni mwa mataifa yaliyoshiriki kupitisha na kukubali kutekeleza mpango huo.