Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wenye namba za ‘3D’ kukiona kuanzia kesho

Muktasari:

  • Kuanzia kesho Ijumaa atakayebainika gari lake kuwa namba hizo, atatozwa faini, kufikishwa mahakamani au kifungo vyote kwa pamoja.

Dar es Salaam. Wakati leo Alhamisi Machi 14, 2024 ikiwa ndio mwisho wa kuondoa kwa hiari namba zilizoongezwa ukubwa ‘3D’ kwenye magari, Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani, kimeainisha hatua zitakazochukuliwa kwa mtu ambaye gari lake litabainika kuendelea kutumia namba hizo zilizopigwa marufuku.

Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani, Kamanda Ramadhani Nga’nzi,  amesisitiza muda wa wiki mbili walioutoa kwa watu kuondoa 3D kwa hiari unakwisha leo, hivyo kuanzia kesho Ijumaa Machi 15, wataanza msako utakaohusisha watengenezaji na wanaoendelea kukaidi kuziweka.

Kamanda Nga’nzi amesema miongoni mwa hatua watakazozichukua ni kupiga faini, kuwasaka, kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watakaobainika kuendelea kuzitengeneza na watumiaji.

Februari mwaka huu, jeshi hilo lilipiga marufuku matumizi ya namba 3D katika magari kwa sababu sio namna rasmi katika nchi ya Tanzania, badala yake lilielekeza wamiliki wa magari kutumia namba za 2D zilizoidhinishwa na msajili wa magari kupitia mawakala.

Sababu nyingine ya kupiga marufuku 3D ni kwamba namba hizo haziko kwenye mfumo wa Tanzania, kwa kuwa hazina ubora unaotakiwa, zinatengenezwa na watu wasioidhinishwa kuwa mawakala wa namba za magari.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Machi 14, 2024 Kamanda Nga’nzi amesema, “Tukiwakuta wameweka namba za 3D tutaziondoa na kuwataka kuweka namba 2D au kuwaandikia faini ya Sh30,000 makosa ya papo kwa papo kwa kutembea na namba zisizoruhusiwa.

“Tukiona unarudia tutakufikisha mahakamani, ambapo utapigwa faini au kifungo kisichozidi miezi sita au vyote kwa pamoja. Namba za 3D haziruhusiwi zinaweza kutumiwa na makundi ya kihalifu, “amesema.

Kamanda Ng’anzi amesema kutumia 3D na namba zingine zisizo rasmi ni kinyume cha sheria za nchi katika usajili wa magari.

“Namba ya gari ndio utambulisho wenyewe wa gari husika, ndio maana vimewekwa vibao maalumu vilivyoanishwa pamoja na watu waliosajiliwa na msajili wa magari kwa ajili ya kutengeneza magari na kuweka vibao hivyo.

Mwezi uliopita Kamanda Nga’nzi aliliambia Mwananchi kuwa kipindi cha siku 14 cha kuziondoa kwa hiari namba hizo kikiisha wataingia kwenye utekelezaji wa sheria.

“Tumezipiga marufuku, tumewapa muda wa kuziondoa kwa hiari, ingawa Watanzania wengi wanapenda hadi wakamatwe,” amesema Nga’nzi.

Katika hatua nyingine, Kamanda Nga’nzi amesema msako wa 3D utakwenda sambamba na kukamata taa za vimulimuli zilizowekwa katika baadhi ya vyombo vya moto visivyoruhusiwa.

Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini alisema namba za 3D hazitengenezwi na wakala aliyepata kibali kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), huku akibainisha kuwa ukubwa herufi hizo unaleta ugumu wa kusomeka.