124 wadakwa Katavi kwa makosa mabalimbali

Kamanda was polisi mkoa wa Katavi Caster Ngonyani ameahika ngozi ya fisi akionesha vitu vilivyokamatwa. Picha na Mary Clemence

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi mkoa wa Katavi linawashikiliwa watu 124 wakituhumiwa kufanya makosa tofauti, kati yao wanne wanahusishwa na tukio la mauaji ya watoto wawili.

Katavi. Jeshi la Polisi mkoa wa Katavi linawashikiliwa watu 124 wakituhumiwa kufanya makosa tofauti, kati yao wanne wanahusishwa na tukio la mauaji ya watoto wawili.

Akizungumza na wanahabari mkoani hapa leo Oktoba 12, 2023, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Caster Ngonyani amesema watuhumiwa hao wamekamatwa kupitia misako na doria mbalimbali zilizofanywa na jeshi hilo.

Amesema watuhumiwa Ditto Mathias (37), Moses Said (52), Yohana Leornad (35) na Kija Maige (25), wakazi wa Kabatini wilayani Tanganyika, wanatuhumiwa kuwaua watoto wawili wilayani humo.

“Maria Mtemvu (2) ambaye alikuwa mtoto wa Mwalimu wa Shule ya Msingi Kabatini Rose Kavita, lakini pia aliuawa mfanyakazi wake wa ndani Ester Enock (13), ambapo inadaiwa wauaji walitumwa na mpenzi wa mwalimu huyo,” amesema Kamanda Ngonyani na kuongeza;

“Walitumwa kwenda kumuua Mwalimu, na zoezi hilo lilikuwa lifanyike mchana hata hivyo watu hao (wauaji) hawakumkuta Mwalimu huyo, na hivyo wakaamua kuwaua watoto baada ya kupiga kelele," amesema

Kamanda amesema baada ya kuwahoji watuhumiwa walikiri kuhusika na kosa hilo wakidai kulipwa Sh400, 000 na mpenzi wa mwalimu huyo, huku wivu wa mapenzi ukitajwa kuwa ndiyo chanzo.

Aidha amesema watuhumiwa wengine watatu wamekamatwa kwa vitendo vya wizi wa pikipiki mbili aina ya Keeway na Kinglion, huku wengine 10 wakikamatwa na mali za wizi wa kuvunja nyumba.

Mbali na hilo, pia kuna watu 75 ambao wamekamatwa kwa tuhuma za kushirikiana na kikundi cha kamchape au lambalamba kilichokuwa kikifanya shughuli za upigaji ramli chonganishi katika mwambao mwa ziwa Tanganyika.

Kamanda huyo pia ametaja idadi ya watuhumiwa 31 waliokamatwa na dawa ya kulevya aina ya bangi, pombe haramu aina ya gongo lita 320, silaha moja gobore na ngozi ya fisi ambayo ni nyara za serikali.

"Baadhi yao upelelezi umekamilika tutawafikisha mahakamani muda wowote na wengine wanaendelea kuchunguzwa," amesema.