Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

14 waliotuhumiwa kwa mauaji huru

Mabaki ya gari lililochomwa moto ambalo liliwabeba watafiti wa Chuo cha Utafiti wa Udongo na Maendeleo ya Ardhi cha Selian mkoani Arusha likiwa katika kijiji cha Iringa-Mvumi wilayani Chamwino Mkoa wa Dodoma. Picha na Maktaba

Arusha/Dodoma. Vilio vya furaha vilitawala nje ya Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma baada ya washtakiwa 14 wa kesi ya mauaji ya watafiti wa udongo waliouawa katika kijiji cha Iringa Mvumi, Chamwino mwaka 2016, kuachiwa huru.

Wakati washtakiwa hao 14 wakiachiwa huru Dodoma, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilimhukumu kunyongwa hadi kufa mfanyakazi wa ndani wa kiume Ismail Sang’wa (28), baada ya kukutwa na hatia ya kumuua kwa kumkata shingo na panga aliyekuwa mwajiri wake, Emily Kisamo (52), aliyekuwa Ofisa wa Intelijensia wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa).

Ni hukumu mbili tofauti zilizosomwa jana, moja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Jaji Joachim Tiganga na nyingine Jaji Mfawidhi Gerson Mdemu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.

Sang’wa, ambaye ni mwenyeji wa kijiji cha Sepuka wilayani Ikungi, Mkoa wa Singida, alipewa adhabu hiyo baada ya kukutwa na hatia ya kumuua kwa makusudi mwajiri wake katika kesi ya mauaji iliyokuwa ikimkabili.

Katika kesi hiyo ya mauaji namba 70/2022, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na wakili wa Serikali Mwandamizi Janeth Sekule, wakili wa Serikali Grace Madikenya na Charles Kagirwa, huku mtuhumiwa huyo akitetewa na wakili Victor Benard.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Tiganga alisema mahakama imemtia hatiani mtuhumiwa huyo baada ya kukutwa hatiani kwa kosa la mauaji kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu na kumhukumu kunyongwa hadi kufa.

Jaji alieleza upande wa Jamhuri umethibitisha pasipo na shaka shtaka lililokuwa likimkabili mtuhumiwa huyo baada ya kusikiliza mashahidi 10 na vielelezo 24 vilivyotolewa na jamhuri, hivyo haukutilia shaka ya msingi.

Jaji Tiganga alieleza mahakama haikutilia maana utetezi wa mshtakiwa huyo kwa kuwa hakuwasilisha kielelezo wala shahidi wa kuithibitishia mahakama kuwa hakuwa eneo la tukio siku mauaji hayo yalipotokea.

Alieleza kuwa kupitia ushahidi wa jamhuri, umethibitisha mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Desemba 18, 2015 nyumbani kwa marehemu eneo la Uzunguni jijini Arusha.
Alieleza kuwa kupitia mashahidi wa jamhuri na maelezo ya onyo ya mshtakiwa huyo ilithibitika mahakamani kuwa siku ya tukio marehemu alikuwa nyumbani kwake sebuleni akiwa anakunywa uji, ndipo mtuhumiwa ambaye ni mfanyakazi wake wa ndani alipomvizia na kumkata shingo na panga.

Aliendelea kuwa mshtakiwa huyo aliuchukua mwili hadi kwenye gari la marehemu aina ya Nissan Mazda lenye namba za usajili T. 435 CSY na kuuweka kwenye buti hadi eneo la Kikwakwaru “B” kata ya Lemara ambapo alilitelekeza hapo na kuondoka.

Kupitia mashahidi wa jamhuri ilielezwa mahakamani kuwa baada ya gari hilo kukaa mpaka saa mbili usiku ndipo baadhi ya wananchi wa eneo hilo walitoa taarifa polisi na askari wa doria walikwenda na kulichukua gari hilo kwa kulivuta mpaka kituoni na baada ya mshtakiwa kukamatwa alikiri kuhusika na mauaji hayo na katika maelezo ya onyo alikiri pia.

Awali ilielezwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa huyo baada ya kukiri kuhusika na mauaji hayo, alionyesha mahali alipokuwa amefukia taulo, shuka zilizokuwa na damu na panga alilokuwa ameficha stoo huku vingine akiwa ameficha kwenye migomba iliyopo nyumbani kwa marehemu.

Ilielezwa kuwa mshtakiwa huyo alionyesha sehemu nyingine ambayo ni banda la kuku, ambapo alikuwa amefukia fedha zaidi ya Sh4.2 milioni, vocha za mtandao wa vodacom zilizokuwa na thamani ya Sh 70,000 na simu nne.


Shangwe Dodoma
Jana Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, iliwaachia huru washtakiwa wote wa kijiji kimoja baada ya Jaji Mfawidhi Gerson Mdemu kusema upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha kesi dhidi ya washtakiwa hao.

Katika kesi ya msingi namba 30/2021 washtakiwa hao walishtakiwa kwa kosa la kuwaua Theresia Nguma, Faraji Mafuru na Nicas Magazine, waliokuwa watafiti kutoka Chuo cha udongo na maendeleo ya ardhi Arusha baada ya kuwakuta katika eneo la kijiji chao na kuwatuhumu kuwa ni wanyonya damu.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Mdemu alisema ushahidi uliotolewa Mahakamani hapo na mashahidi wa upande wa Jamhuri uliacha shaka kutokana na mauaji hayo yalifanyika na kundi la watu ambao baadhi ya mashahidi wameshindwa kuwatambua kwenye gwaride la utambuzi.

Jaji Mdemu alisema katika ushahidi uliotolewa pia baadhi ya mashahidi walieleza kuwa walifika eneo la tukio kwa kuchelewa, wengine wameeleza kulikuwa na watu waliozidi 80 hivyo kutia shaka utambuzi wa washtakiwa.

Mdemu alisema ushahidi mkubwa uliotumika katika kesi hiyo ni ushahidi wa gwaride la utambuzi ambao nao umeonyesha mashaka hivyo kushindwa kusimama peke yake na kuhitaji kuungwa mkono na ushahidi mwingine ambao haukutolewa Mahakamani.

Hata hivyo, Jaji Mdemu alisema baadhi ya mashahidi wa Jamhuri walieleza kuwa hawakuwaona washtakiwa eneo la tukio hivyo upande Jamhuri walipaswa kuiomba Mahakama chini ya kifungu cha 154 cha Sheria ya ushahidi ili mashahidi hao waonekane ni mashahidi kigeugeu.

Mara baada ya hukumu hiyo, Edward Lubeleje ambaye alikuwa mahabusu na mkewe alisema matokeo ya hukumu hiyo ni maombi waliyojibiwa na Mungu na sio kwa ujanja wake.
Naye Joseph Warioba aliishukuru Mahakama akidai imetenda haki kwani kitendo walichofanyiwa