Mvutano mazishi ya Rais Lungu wahamia kwenye siasa za uchaguzi
Muktasari:
- Baada ya Mahakama ya Rufani Afrika Kusini kuruhusu familia ya Lungu kuamua mazishi, mjadala wake umehamia kwenye siasa za uchaguzi mkuu unaoendelea Zambia
Dar es Salaam. Mvutano kuhusu maziko ya aliyekuwa Rais wa Zambia, Edgar Lungu sasa umeingia kwenye siasa za kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 13, 2026, baada ya uamuzi wa Mahakama ya Rufani ya Afrika Kusini kuipa familia yake mamlaka ya kuamua mahali na namna ya mazishi yake.
Uamuzi huo umehitimisha zaidi ya mwaka mmoja wa mvutano kati ya Serikali ya Zambia na familia ya marehemu, huku serikali ikitaka mwili wake urejeshwe Lusaka kwa mazishi ya kitaifa katika makaburi ya Embassy Park, wakati familia ikisisitiza kuwa Lungu aliacha matakwa ya kuzikwa Afrika Kusini.
Lungu alifariki Juni 5, 2025 mjini Pretoria, na tangu wakati huo mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti nchini Afrika Kusini kutokana na mzozo wa kisheria uliodumu.
Baada ya uamuzi wa Mahakama, Serikali ya Zambia ilikubali matokeo hayo licha ya kutoridhishwa, ikisema haitaingilia uamuzi wa familia, ingawa ilikumbusha kuwa marais waliotangulia kama Michael Sata na Levy Mwanawasa walipewa mazishi ya kitaifa.
Hata hivyo, badala ya kuhitimisha mjadala huo, uamuzi huo umeufungua upya katika uwanja wa siasa, sasa suala la mazishi limeanza kutumika kama hoja ya kampeni kuelekea uchaguzi.
Mwanasiasa wa upinzani, Brian Mundubile amenukuliwa akisema, mwili huo utazikwa baada ya uchaguzi kupita.
“Tutamzika Lungu baada ya kushinda uchaguzi,” amenukuliwa na vyombo vya habari nchini humo, kauli ambayo imechukuliwa na wachambuzi kama kuingiza suala la mazishi kwenye ushindani wa kisiasa.
Kauli hiyo imepingwa na chama tawala cha UPND kupitia msemaji wake Cornelius Mweetwa, ambaye amesema upinzani unajaribu kutumia kifo na mazishi ya rais wa zamani kisiasa bila mafanikio.
“Wazambia tayari wameendelea mbele. Uchaguzi utaamuliwa na maendeleo, si mjadala wa mazishi,” amesema Mweetwa.
Wakati huo huo, msemaji wa familia ya Lungu, Makebi Zulu, anadaiwa kuwa hakuna tarehe rasmi ya mazishi iliyotangazwa, akiongeza kuwa uamuzi wa mwisho bado upo mikononi mwa familia kama ilivyoelekezwa na Mahakama.
Hata hivyo, taarifa mbalimbali ndani ya Zambia zinaonesha kuwa baadhi ya kauli za kisiasa zimeanza kuashiria kuwa mazishi yanaweza kufanyika baada ya uchaguzi, ingawa hakuna uthibitisho rasmi kutoka kwa familia.
Mjadala huo unaendelea kuleta mgawanyiko ndani ya Zambia kati ya wale wanaotaka heshima ya kitaifa kwa rais wa zamani na wale wanaosisitiza kuwa suala hilo lisichanganywe na siasa za uchaguzi.
Huku uchaguzi ukikaribia, mvutano huo unaendelea kuibua maswali iwapo mazishi ya Lungu yatakuwa mwisho wa mjadala huo au yataendelea kuwa sehemu ya mapambano ya kisiasa na mjadala mpana nchini humo.