35 kufanyiwa upasuaji wa ubongo, mishipa ya fahamu

Daktari wa upasuaji ubongo na mishipa hospitali ya rufaa ya Bugando, Misso Adrian (kushoto) akimfanyia upasuaji mtoto mwenye kichwa kikubwa hospitalini hapo leo. Kulia ni msaidizi wake Diana Adrian. picha na Jesse Mikofu
Muktasari:
Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza kwa kushirikiana na daktari kutoka Uganda watawafanyia upasuaji wagonjwa 35 wenye tatizo katika ubongo na mishipa ya fahamu
Mwanza. Wagonjwa 35 wa wenye tatizo katika ubongo na mishipa ya fahamu watafanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza.
Upasuaji huo unafanywa na daktari bingwa kutoka Uganda kwa kushirikiana na hospitali hiyo.
Akizungumza leo Alhamisi Novemba 29, 2018 wakati upasuaji huo ukiendelea hospitalini hapo, mkurugenzi wa huduma za upasuaji, Dk Fabian Massawe amesema hatua hiyo inalenga kutatua changamoto za upasuaji.
Amesema watakaofanyiwa upasuaji ni wale waliopata ajali na kuumia kichwani na watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.
Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji kutoka Uganda, Alex Muhindo amesema tangu awasili Bugando wiki mbili zilizopita, ameshafanya upasuaji kwa wagonjwa 24.
“Kazi inaendelea vizuri kwa kipindi nilichofika hapa Bugando. Tumeshafanya upasuaji kwa watu 24, lengo ni kuwafanyia upasuaji wagonjwa 35. Naamini wote tutawafanyia kwa kipindi cha wiki moja iliyobaki,” amesema Dk Muhindo.