8,000 wajitosa ajira 42 za Bunge

Dodoma. Tume ya Utumishi ya Bunge imetangaza ajira za kada mbalimbali ambapo walioitwa kwenye usaili wako zaidi ya 8,000 kati ya nafasi za kazi 42 zilizotangazwa, huku kada zinazoongoza kwa idadi kubwa ni uchumi, udereva, sheria na uhasibu.

Kwa mujibu wa tangazo la kuitwa kwenye usaili lililotolewa Mei 19, mwaka huu na Katibu wa Bunge jijini Dodoma, liliorodhesha jumla ya majina 8,476 ya waliovuka hatua ya kwanza ya mchujo na kuitwa kwenye usaili kwa kada 21 za ajira kwenye Bunge la Muungano wa Tanzania.

Aprili 21, mwaka huu Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitangaza nafasi za kazi 42 katika kada 21 mbalimbali ili kuimarisha utendaji wake.

Juzi, Bunge lilitoa tangazo lililosomeka: “Katibu wa Bunge, kwa niaba ya Sekretarieti ya Bunge anapenda kuwataarifu waombaji kazi wote walioomba kazi kuwa usaili unatarajiwa kuendeshwa kuanzia Mei 27, 2023 hadi Juni 03, 2023 na hatimaye kuwapangia vituo vya kazi waombaji kazi watakaofaulu usaili huo.”

Kwa mujibu wa tangazo hilo, kada zinazoongoza kwa waombaji wengi ni uchumi, sheria, udereva na uhasibu, huku kada zenye waombaji walio chini ya 100 ni afya na maktaba.

Tangazo hilo liliainisha kada hizo na idadi ya walioteuliwa kwenye usaili ikiwa kwenye mabano, ofisa hesabu daraja la II (538), msaidizi wa kumbukumbu daraja la II (279), udereva daraja la II (984), mhandisi umeme daraja la II (234), ofisa usimamizi wa fedha daraja la II (492), mwandishi wa taarifa rasmi za Bunge darala la II (413), mchumi daraja la II (904), ofisa sheria daraja la II (302).

Nyingine ni ofisa Tehama daraja la II (310), msaidizi wa maktaba daraja la II (98), katibu msaidizi wa Bunge daraja la II Sheria (831), katibu msaidizi wa Bunge daraja la II uchumi (1,208), katibu msaidizi wa Bunge daraja la II (afya ya jamii/menejimenti ya huduma za afya) 47.