Chuo cha Uhasibu Arusha kuwekeza Sh700 milioni kusaidia vijana

Arusha. Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kupitia kituo cha kiatamizi kinacholenga kuwajengea uwezo vijana wa chuo hicho kukuza mawazo yao ya biashara kimewekeza kiasi cha Sh700 milioni kwa ajili ya kusaidia vijana hao.

Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mkuu wa chuo hicho, Profesa Eliamani Sedoyeka wakati akizungumza katika maonesho ya mafunzo ya ufundi Stadi  yanayofanyika katika viwanja vya Stadium jijini Arusha.

Profesa Sedoyeka amesema fedha hizo zimetumika katika kuandaa kituo hicho sambamba na kutenga kiasi cha Sh100 milioni kwa ajili ya kuwawezesha vijana mitaji kwa ajili ya kuendeleza biashara zao.

Amesema kituo hicho kina malengo mbalimbali ya kuwatafutia mitaji, kuboresha uzalishaji, kuwasaidia kupata masoko ya uhakika na hatimaye kufikia kampuni.

Ameongeza kitendo cha kuwaandaa vijana wao kinawasaidia wao kuweza kujiajiri na kuajiri wengine huku kampuni zao zikizidi kukua na kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwa ni kuunga mkono lengo la kujenga Tanzania ya viwanda ambapo kituo kimejipanga kukuza zaidi ya biashara 40 kwa wakati mmoja.                

Amefafanua vijana wenye wazo la biashara wameweza kuwasaidia kuwa wazo la kampuni ambapo kwa mwaka huu wamewawezesha vijana hao kuanzisha kampuni sita.

"Tunachotaka sisi ni kuhakikisha wanafunzi wakihitimu wanakuwa watengeneza ajira na sio watafuta ajira na hii inasaidia sana kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira iliyopo katika maeneo mbalimbali hapa nchini" amesema

Amesema wizara imekuwa ikifanya vizuri sana katika kurekebisha mitaala mbalimbali ambayo itasaidia vijana kujiajiri na wamekuwa wakishirikiana na wizara kwa karibu sana katika maswala hayo.

Aidha ameongeza kwa mwaka huu chuo hicho kimeweza kuanzisha kozi mpya nne zitakazoanza kutumika mwaka huu ili  kuzalisha wataalamu wa kutosha ambapo amewataka vijana waliohitimu kidato cha sita ndio muda wa kuchangamkia  fursa hiyo kwa kujifunza kozi mbalimbali chuoni hapo.

"Sisi tumejipanga kwa kutoa kozi za kimkakati  ikiwemo ya uanagenzi  katika maswala ya bima, na utalii ambapo wanafunzi wetu wamekuwa wakiandaliwa  vizuri na kupata muda  mzuri  wa kujifunza zaidi," amesema Profesa Sedoyeka