Abiria wapungua uwanja wa ndege Musoma, chanzo chatajwa

Muktasari:
Idadi ya abiria wanaotumia uwanja wa ndege wa Musoma imeshuka kutoka abiria 14,000 hadi 2,500 kwa mwaka kutokana na ubovu wa uwanja huo.
Musoma. Abiria wanaotumia uwanja wa ndege wa Musoma wamepungua kutoka 14,000 kufikia 2,500 kwa mwaka baada ya kusitishwa huduma za ndege za abiria kutokana na ubovu wa uwanja huo huku ndege ndogo ndogo zikiwemo za kukodi zikiendelea kutua uwanjani hapo.
Ndege hizo zilisitishwa huduma uwanjani hapo Machi, 2018 ili kupisha maboresho.
Meneja wa uwanja huo, Frank Msofe ameyasema hayo leo Ijumaa Novemba 24, 2023 mbele ya Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile aliyefanya ziara kukagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo.
“Kwasasa uwanja huu unapokea zile ndege ndogo ambazo ni za kukodi inaweza ikaja na abiria hata mmoja na hii inatokana na uwanja kuwa mbovu hivyo ndege za abiria kushindwa kutua kwasababu za kiusalama,"amesema
Msofe amesema kutokana na ujenzi unaoendelea wa kuboresha uwanja huo kutoka kiwango cha changarawe hadi lami ndege za abiria zenye uwezo wa kubeba watu kuanzia 78 zitakuwa na uwezo wa kutua kwenye uwanja huo.
Akitoa taarifa ya mradi, Meneja wa Wakala wa barabara (Tanroads) Mkoa wa Mara, Vedastus Maribe amesema awali uwanja huo ulitakiwa kukamilika Desemba, 2023 lakini kutokana na mwenendo wa kazi mkandarasi ameoomba kuongezewa muda wa mwaka mmoja.
"Sasa mradi huu wenye thamani ya zaidi ya Sh35 bilioni utakamilika Desemba, 2024 na hadi sasa umefikia asilimia 52 za utekelezaji wake,"amesema Maribe
Ujenzi na upanuzi wa uwanja wa Musoma unahusisha kuongezwa kwa urefu wa uwa ja kutoka mita 1,600 hadi 1,705, ujenzi wa njia za kuruka na kutua ndege, maegesho ya ndege, jengo la zimamoto, jengo la umeme, uzio na miundombinu mingine.
Akizungumzia madeni ya mkandarasi anayejenga uwanja huo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema tayari Serikali imeweka utaratibu wa kulipa madeni yote ya makandarasi wa miradi mbalimbali wanayodai.
"Oktoba Waziri wa Ujenzi alifanya ziara hapa na alipokea changamoto zote za mradi huu likiwepo deni la mkandarasi, tayari utaratibu umefanyika wote wanaodai watalipwa kulingana na fedha zitakavyokuwa zinapatikana, mkandarasi wa mradi huu endelea na kazi kwa kasi na kuzingatia ubora wa kazi," amesema
Amesema mradi wa uwanja wa ndege Musoma una umuhimu mkubwa katika suala la uchumi na kijamii mkoani Mara kutokana na kuwepo kwa shughuli za kitalii, uchimbaji wa madini na pia ni eneo alipozaliwa Hayati Mwalimu Julius Nyerere.