Wataalamu wa anga waitupia jicho Songwe Airport

Mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya uwezeshaji wa usafiri wa anga nchini, Daniel Malanga Akizungumza wakati wa kikao cha 54 cha kamati hiyo jijini Mbeya
Muktasari:
- Kikao hicho kitadumu kwa siku tatu jijini Mbeya kikishirikisha wataalamu mbalimbali wa anga wanaohudumu katika viwanja vya ndege kwa lengo la kuboresha huduma hiyo nchini.
Mbeya. Wakati utafiti ukitaja mazao ya Mbeya kupendwa na kufanya vizuri katika soko la kimataifa, kamati ya kitaifa ya uwezeshaji wa usafiri wa anga nchini, wajadili mkakati wa uboreshaji uwanja wa ndege Songwe ili kutoa huduma bora ya usafirishaji mizigo na abiria.
Akizungumza leo Novemba 15 katika kikao hicho cha 54, mwenyekiti wa kamati hiyo, Daniel Malanga amesema wameamua kukutana jijini hapa kutokana uwanja wa ndege Songwe kuongeza idadi ya abiria, mizigo na kuweka matarajio makubwa ya ukuaji sekta ya usafirishaji wa anga mkoani humo.
Amesema utafiti unaonesha kuwa licha ya kuwepo shughuli nyingi katika uwanja huo, lakini zipo changamoto za wakulima ambao mazao yao ambayo huharibika haraka na kwamba kupitia kikao hicho kitapata ufumbuzi wake.
"Ardhi, afya na hali ya hewa ya Mbeya vinatajwa kutoa mazao pendwa katika soko huko nje ndio maana tumeamua kuipa jicho la pekee kiwanja cha ndege Songwe ili kuendelea kutoa huduma bora kwa watanzania na nchi jirani"
"Kupitia kikao hiki cha siku tatu wajumbe watatembelea pia uwanja huo ili kujionea shughuli zinazofanyika ikiwamo uwekezaji uliofanywa na serikali kwani tunao wataalamu mbalimbali wanaohudumu kwenye viwanja vya ndege" amesema Malanga.
Malanga ameongeza kuwa Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika huduma za ndege, kwani kwenye ukaguzi wa shirika la usafiri wa anga duniani,(ICAO) nchi hiyo imekuwa ya nne katika maeneo ya usalama 'Safety na Security '.
"Lengo letu kubwa ya kuwapo kamati hii jukumu lake ni kuboresha huduma kwa ndege, abiria na marubani kwa ufanisi lakini kutoa ushauri na kufuatilia mwenendo wa huduma kwenye viwanja" amesema Malanga.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanal Denis Mwila ameiomba kamati hiyo kufanya utafiti katika mambo matatu ikiwa ni kodi, tozo na ada.
Amesema Mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa maeneo yenye uhitaji mkubwa wa huduma za usafiri wa anga kutokana na shughuli zinazofanyika husasani za kilimo kutegemea huduma hiyo kwa ajili ya soko la ndani na nje.
"Mkoa huu na kanda yetu kwa ujumla inahitaji huduma ya usafiri wa anga hivyo niombe kikao hiki kifanye tafiti kuhusu kodi, ada na tozo na kupata suluhisho ili kumrahisishia mkulima kunufaika na kilimo chake" amesema Mwila.
Mmoja wa wakulima wa zao kakao Francis Thomas amesema yapo mazao ambayo bado bei yake haijawa rafiki akiomba serikali katika kutafuta soko nje ya nchi kujumuisha mazao yote.
"Lakini kuna mazao mengine hayapaswi kukaa sana yanapaswa kusafirishwa mapema yanapotolewa shambani hivyo tunaamini kikao hicho kitakuja na maazimio yenye neema kwetu" amesema Thomas.