ACT-Wazalendo kibaruani mrithi wa Maalim Seif Zanzibar

New Content Item (2)
ACT-Wazalendo kibaruani mrithi wa Maalim Seif Zanzibar

Muktasari:

Baada ya kifo cha Maalim Seif Sharrif Hamad, swali linalogonga vichwa vya watu hivi sasa ni nani atakayekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar?

Dar es Salaam. Baada ya kifo cha Maalim Seif Sharrif Hamad, swali linalogonga vichwa vya watu hivi sasa ni nani atakayekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar?

Chama cha ACT-Wazalendo sasa kipo kwenye mtihani mgumu wa kupendekeza jina la mwanachama wake kuziba nafasi hiyo ndani ya siku 14 kwa mujibu wa katiba.

Hilo linatokana na kifo cha Maalim Seif kilichotokea Februari 17 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na sasa nafasi hiyo iko wazi baada ya awali chama hicho kumpendekeza Maalim ambaye aliapishwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi Desemba 8, mwaka jana.

Uchambuzi wa gazeti hili umebaini kati ya makada hawa wanne wa chama hicho, huenda mmoja akapendekezwa kuchukua mikoba ya Maalim Seif ambao ni Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo-Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui; Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Juma Duni Haji; Mansour Yusuf Himid ambaye alikuwa mshauri wa Maalim Seif na Mwanasheria Mkuu wa zamani Zanzibar, Othman Masoud Othman.

Kazi kubwa iliyobaki kwa ACT-Wazalendo, kinapaswa kuketi ndani ya siku 10 zilizobaki kuteua na kuidhinisha jina moja litakalopelekwa kwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi atakayemteua kuwa makamu wa rais kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa Katiba ya ACT-Wazalendo, kamati ya uongozi ya chama ndiyo yenye mamlaka ya kuteua jina la mwanachama atayekuwa makamu wa kwanza wa rais..

Unaweza kusema huu ni mtihani mzito kwa Zitto Kabwe ambaye ni kiongozi wa ACT-Wazalendo, anayetakiwa kusimamia mchakato huo ndani siku 10 zilizobaki ili kumpata mtu sahihi atakayeweza kuziba nafasi iliyoachwa wazi na mtangulizi wake ambaye alijizolea sifa nyingi ndani ya Zanzibar na nje ya kisiwa hicho.

Wakati tukisubiri mchakato huo ndani ya ACT-Wazalendo, baadhi ya majina ya watu maarufu Zanzibar yameanza kutajwa tajwa na wadau wa siasa na wanachama wa chama hicho, kuwa ndiyo huenda mmoja wao akarithi nafasi hiyo.

Mazrui

Huyu alizaliwa mwaka 1960, ni mwanasiasa mzoefu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar. Mbali na shughuli za siasa, Mazrui anajihusisha na biashara mbalimbali ikiwamo hoteli.

Alikuwa miongoni mwa mawaziri waliofanya vizuri katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), kuanzia mwaka 2010/15 chini ya Dk Ali Mohamed Shein.

Mazrui ni mmoja wa wajumbe wawili walioteuliwa na Rais Dk Mwinyi kuingia kwenye Baraza la Wawakilishi baada ya uongozi wa ACT-Wazalendo, kukubali kuridhia maridhiano yaliyozaa SUK ya awamu ya pili.

Katika uchaguzi wa mwaka jana, Mazrui alikumbwa na misukosuko mbalimbali ikiwamo kudaiwa kutekwa na watu wasiojulikana kisha kuachiwa, lakini Oktoba 28, 2020 jioni alikamatwa na polisi akidaiwa kukutwa na vifaa vya kuingilia mfumo wa matokeo.

Duni

Ni mwanasiasa mkongwe kuliko Mazrui, alizaliwa Novemba 26 mwaka 1950, alisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Maalim Seif. Kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, pia aliwahi kufungwa jela kutokana na shughuli za kisiasa.

Kama ilivyokuwa kwa Mazrui, Duni alikuwa mmoja wa mawaziri waliofanya vizuri ndani ya SUK ya mwaka 2010-15 akisimamia sekta ya afya. Duni ni kiongozi mwenye uzoefu kwenye siasa za Zanzibar.

Mansour

Huyu alizaliwa Novemba 3 mwaka 1967, kabla ya kujiunga upinzani alikuwa CCM na mwakilishi wa Kiembe Samaki kwa miaka minane. Akiwa CCM Mansour aliwahi kuwa waziri wa sekta mbalimbali katika Serikali za marais Aman Abeid Karume na Dk Shein.

Agosti mwaka 2014 alifukuzwa CCM kwa makosa mbalimbali ikiwemo kudaiwa kukihujumu chama hicho, lakini alihamia CUF kisha ACT-Wazalendo akiwa mshauri mkuu wa Maalim Seif.Mansour anaonekana ni jasiri na anayekubalika kwa Wazanzibari.

Masoud

Ni msomi aliyebobea kwenye sheria ambaye katika miaka mitano ya kwanza ya Dk Shein aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.Anaonekana ni mtu anayependa kusimamia haki za Zanzibar ndani ya muungano.

Mwaka 2013 Masoud, akiwa bado Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar alizua sintofahamu baada ya kupiga kura ya wazi na kukataa ibara muhimu kwenye rasimu ya katiba iliyopendekezwa katika Bunge Maalum la Katiba lililokuwa likifanyika mkoani Dodoma.

Hatua hiyo ilisababisha mvutano kati yake na wajumbe wa CCM hasa kutoka Zanzibar ambao walihoji kitendo chake kupiga kura wakati muda mwingi wa uendeshaji wa vikao hivyo hakuwapo bungeni.

Gazeti hili, liliwatafuta wachambuzi wa masuala ya kisiasa ambao walitaja Mazrui, Duni na Mansour kuwa mmoja wao huenda akateuliwa kurithi mikoba ya Maalim Seif kutokana na uzoefu na ushiriki wao wa muda mrefu katika siasa za Zanzibar.

“Mzee Duni ni mkongwe katika siasa za Zanzibar, alizaliwa mwaka 1950 kwa hiyo mwaka huu mwezi Novemba anatimiza miaka 70. Ni mkubwa kwa Dk Mwinyi, lakini ana busara za kutosha kuwa kiongozi wa juu kwenye SUK,” alisema Faraja Kristomus ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Alisema Duni au maarufu kwa jina la ‘Babu Duni’ ni mtu maarufu, aliyefanya kazi na Maalim Seif kwa miaka mingi na kwamba anazijua vyema siasa za rafiki wake huyo.

“Kabla ya kuingia kwenye siasa, Babu Duni ni mwalimu kitaaluma kama alivyokuwa Maalim Seif. Alisomea shahada yake ya kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Manchester kwa shahada ya Umahiri.

Akizungumzia Mansour, Kristomus alisema ni mwingine mwenye ushawishi wa kisiasa ndani ya Zanzibar ambaye katika shughuli za kisiasa misukosuko mingi ndani ya Serikali ya Zanzibar hadi alipoachishwa kazi na Dk Shein mwaka 2012.

“Kwa kariba yake Mansour anakubalika ndani ya CCM na kwa wapinzani pia. Lakini pia viongozi wakongwe walio nje ya Serikali nao watampa ushirikiano mkubwa na hivyo hatapata shida sana endapo atateuliwa kumrithi Maalim Seif,” alisema.

Pia Kristomus alimzungumzia Mazrui, akisema ni kigogo mwingine anayepewa nafasi ya kurithi mikoba ya Maalim Seif kutokana na historia ya utendaji kazi wake huko nyuma. “Huyu ni miongoni mwa watu wawili walioteuliwa na Dk Mwinyi mwaka jana kuwa wajumbe wa baraza la uwakilishi. Hii ilimaanisha kuwa alionekana na uwezo wa kuwa Waziri ndani ya SUK, lakini pia Mazrui siyo mgeni katika siasa za Zanzibar.

Kwa mujibu wa Kristomus, Masoud ni miongoni mwa watu anaowafikiria ingawa hampi nafasi kubwa kama ilivyo kwa kina Duni, Mazrui na Mansour kuchukua nafasi hiyo

“Kitendo cha Masoud kuwa tayari kuwa na msimamo wake kuhusu masuala yenye maslahi mapana ya Zanzibar kuliwafanya Wazanzibari wengi kumpenda na kumwona shujaa wao. Wakati Kristomus akieleza hayo, mchambuzi mwingine wa masuala ya siasa Zanzibar, Profesa Abdul Sheriff alisema Mazrui, Duni na Mansour ni miongoni mwa wanaopewa kipaumbele katika mchakato huo.

Hata hivyo, msomi huyo alisema atakayechukua nafasi hiyo lazima awe na uwezo wa kusimamia madai ya wanachama wa ACT-Wazalendo na kwamba asiwe na papara, badala yake awe mpole ili kuendeleza vyema maridhiano yaliyochwa Maalim Seif.

“Mazrui ni miongoni mwa watu wanaonekana kwa urahisi, kwa sababu alikuwa karibu na Maalim Seif na mzoefu pia. Kwa upande wake Duni ni mwanasiasa mzoefu kwenye chama pia alikuwa karibu na Maalim.”

Kuhusu Mansour, Profesa Sheriff alisema ni mchanga ingawa ana mvuto kwenye medani ya siasa kwa namna alivyohama CCM kuhamia CUF kisha ACT-Wazalendo. Alisema kitendo hicho kiliweza kuwavutia wengi na kumpenda.

Hata hivyo, Profesa Sheriff aliyewahi kufundisha vyuo mbalimbali vya Zanzibar na Tanzania, alisema Mazrui na Duni ni watu watakaopewa nafasi kubwa kumrithi Maalim Seif.